Jumatano tarehe 17 Feberuari 2021
Leo ni Jumatano tarehe 5 Rajab 1442 Hijria sawa na Februari 17 mwaka 2021.
Tarehe 5 Rajab miaka 1198 iliyopita aliuawa shahidi Abu Yusuf Yaqub ibn Is'haq, maarufu kwa jina la Ibn Sikkit, msomi wa Kiislamu na mtaalamu mkubwa wa lugha ya Kiarabu. Alizaliwa katika mji wa Khuzestan unaopatikana kusini magharibi mwa Iran. Ibn Sikkit alielekea mjini Baghdad na familia yake na kusoma kwa walimu wakubwa wa zama hizo. Umaarufu wa Ibn Sikkit katika elimu ulimfanya Mutawakkil, mmoja kati ya watawala wa Abbasia kumwalika kwa lengo la kuwafundisha watoto wake. Ibn Sikkit alikuwa na mapenzi makubwa kwa Watu wa Nyumba ya Mtume (SAW); jambo hilo lilimkasirisha sana Mutawakkil na alichukua hatua ya kumuua. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyu ni kile kiitwacho "Islahul Mantik."
Katika siku kama ya leo miaka 212 iliyopita, vilimalizika vita vya umwagaji damu vya Zaragoza vilivyopiganwa kati ya wanajeshi wa Ufaransa na wale wa Uhispania, huku Ufaransa ikipata ushindi na kuukalia kwa mabavu mji wa Zaragoza ulioko mashariki mwa Uhispania. Vita hivyo vilianza Novemba 15 mwaka 1808, kufuatia uvamizi wa jeshi la Napoleon.
Siku kama ya leo miaka 194 iliyopita, aliaga dunia Johann Heinrich Pestalozzi, msomi wa Uswisi na mmoja wa walimu mashuhuri. Pestalozzi alikuwa mjuzi wa elimu nyingi hasa hisabati na tiba na alizungumza lugha kadhaa za kimataifa. Msomi huyo wa Uswisi alikuwa na mtindo wake makhsusi wa kufundishia ambapo aliweza kutoa mafunzo ya masuala mbalimbali kwa watoto kwa wakati mmoja.
Miaka 43 iliyopita katika siku kama hii ya leo, wananchi Waislamu wa Tabriz huko kaskazini magharibi mwa Iran walikutana katika msikiti mmoja mkubwa katika mji huo kwa lengo la kuwakumbuka wananchi waliouawa shahidi tarehe 19 mwezi Dei mwaka 1356 Hijria Shamsiya huko Qum kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani. Wenyeji wa Tabriz walikutana hapo kufuatia wito uliotolewa na maulamaa na wanazuoni wa kidini. Mkutano huo ulibadilika na kuwa uasi wa kijamii kutokana na ukandamizaji mkubwa uliofanywa na askari wa utawala wa kidhalimu wa Shah. Harakati hiyo ya kimapinduzi iliutia kiwewe utawala wa Shah ambao ulitumia urongo kuhadaa wananchi kwa kudai kuwa, waliohusika na harakati hiyo walitoka nje ya Iran.
Tarehe 17 Februari miaka 10 iliyopita ilianza harakati ya wananchi wa Libya dhidi ya utawala wa kidikteta wa Kanali Mummar Gadafi. Libya ilikuwa nchi ya tatu kukumbwa na wimbi la mwamko wa Kiislamu na kuziangusha tawala kadhaa za kidikteta. Baada ya kuondolewa madarakani serikali ya Zainul Abidin bin Ali nchini Tunisia na ile wa dikteta wa zamani wa Misri, Husni Mubarak, wananchi wa Libya pia walianzisha harakati kubwa dhidi ya dikteta wa nchi hiyo, Muammar Gaddafi. Awali Gaddafi alidhani kwamba angeweza kuzima harakati hiyo ya wananchi kwa kutumia jeshi na vyombo vya usalama na kwa msingi huo alianza kutumia mkono wa chuma na kuua wananchi waliokuwa wakiandamana. Wanachama wa shirika la kijeshi la nchi za Magharibi NATO pia walipanda mawimbi ya harakati ya mapinduzi ya wananchi wa Libya na kushambulia vituo vya kijeshi na viwanda vya Libya. Hatimaye dikteta Muammar Gaddafi aliyeitawala Libya kwa kipindi cha miongoni minne kwa mkono wa chuma aliondolewa madarakani kwa madhila na kuuawa kwa kudhalilishwa na kisha akazikwa sehemu isiyojulikana.
