Feb 22, 2021 23:19 UTC
  • Jumanne tarehe 23 Februari 2021

Leo ni Jumanne tarehe 11 Rajab 1442 Hijria sawa na Februari 23 mwaka 2021.

Siku kama ya leo miaka 1171 iliyopita sawa na tarehe 11 Rajab mwaka 271 Hijiria, alizaliwa Abubakr Muhammad maarufu kama Ibin Anbari mwanafasihi, mtaalamu wa lugha na mfasiri wa Qur'ani Tukufu katika mji wa Baghdad. Alijifunza lugha na elimu ya Qur'ani na baadaye hadithi. Ibn Anbari alikuwa na uwezo mkubwa wa kuhifadhi mambo na pia alifanya kazi ya kufundisha kwa unyenyekevu. Miongoni mwa vitabu vyake ni Adabul Katib na Dhamairil Qur'ani. Ibn Anbari alifariki dunia mwaka 328 Hijiria.

Miaka 871 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia mjini Damascus, Syria mwanahistoria mkubwa na mtaalamu wa hadithi Ibn Asakir. Alisoma elimu za Qur'ani, hadithi, fiq'hi na usulu fiq'hi kwa wasomi wakubwa wa mjini Damascus. Baada ya hapo Ibn Asakir alianza safari ndefu yenye lengo la kukamilisha masomo yake na kupata kusoma katika vituo vya kielimu vya mijini Baghdad, Kufa, Musil, Nishabur, Marv, Isfahan na Hamadan. Msomi huyo ameandika vitabu 134 ambapo miongoni mwavyo ni kile cha "Tarikh Dimeshqi."

Siku kama ya leo miaka 222 iliyopita, baada ya Napoleon Bonaparte, kamanda wa jeshi la Ufaransa kuidhibiti Misri, alianza kufanya mashambulio dhidi ya Sham, ambayo wakati huo ilikuwa ikundwa na nchi za Syria, Jordan, Lebanon na Palestina. Mashambulio ya Bonaparte dhidi ya Misri ilifanyika kwa lengo la kutoa pigo kwa Uingereza iliyokuwa mkoloni wa Misri. Lakini sababu ya mashambulio ya Napoleon Bonaparte dhidi ya Sham iliyokuwa sehemu ya ardhi ya utawala wa Othmania, ni hatua ya mfalme wa utawala wa Othmania ya kutangaza vita dhidi ya Ufaransa. Katika mashambulio hayo, licha ya kuwa awali Bonaparte alipata ushindi, lakini baadaye alilazimika kuacha vita na kurejea kwao kutokana na uungaji mkono wa Uingereza na Urusi kwa utawala wa Othmania bila kusahau kuharibika hali ya mambo ndani ya Ufaransa.

Napoleon Bonaparte

Na siku kama ya leo miaka 135 iliyopita mvumbuzi na mwanakemia wa Marekani Charles Martin Hall alivumbua aluminiamu. Aluminiamu ni chuma cheupe na chepesi kinachoweza kukunjwa kwa urahisi. Aluminiamu hii ambayo ni nyepesi kuliko chuma, leo hii imekuwa na matumizi mengi katika shughuli za viwanda kadhalika.