Feb 23, 2021 23:11 UTC
  • Jumatano, Februari 24, 2021

Leo ni Jumatano tarehe 12 Rajab 1442 Hijria inayosadifiana na Februari 24 mwaka 2021 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1410 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria alifariki dunia Abbas bin Abdul Muttalib, ami yake Bwana Mtume SAW na mmoja wa shakhsia wakubwa wa Kikuraishi. Alijulikana kwa tabia njema, mwenendo mzuri, busara na maarifa ya hali ya juu. Baadhi ya wanahistoria wanaamini kwamba, Abbas bin Abdul Muttalib aliukubali Uislamu kwa siri kabla ya Bwana Mtume kuhamia Madina na alikuwa akimpelekea Mtume habari za harakati za washirikina mjini Makka. Mwaka wa 8 Hijria Abbas bin Abdul Muttalib aliungana na Waislamu na baada ya Fat'hu Makka aliteuliwa na Bwana Mtume kuchukua jukumu la kutoa huduma ya maji kwa watu wanaozuru Nyumba ya Mwenyezi Mungu, al-Kaaba.

Miaka 1236 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alifariki dunia Abu Hudheifa mpokezi wa hadithi, habari za kihistoria na mwandishi wa visa vya Mitume. Kwa muda fulani aliishi katika miji ya Makka na Madina na kujishughulisha na masomo ya hadithi. Abu Hudheifa alikuwa mpokezi wa hadithi mwenye hadhi kubwa. Miongoni mwa vitabu vyake muhimu ni pamoja na kile cha "Al Mubtada" kinachohusu uumbwaji wa mwanadamu na visa vya Mitume. Kitabu chake kingine ni kile kinachohusu uchambuzi wa hadithi ya Imam Swadiq (as) kuhusu Mi'raji ya Mtume Mtukufu (saw). 

Miaka 233 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 12 Rajab, utawala wa ukoo wa Zandiye nchini Iran ulifikia tamati baada ya kuaga dunia Lotfi Ali Khan Zand. Jiwe la msingi la utawala wa ukoo wa Zandiye liliwekwa na Mohammed Karim Khan Zand mwaka 1165 Hijria na binafsi alikuwa akitambua kama mwakilishi wa wananchi na alifanya hima ili watu waishi katika utulivu. Hata hivyo aliyekuja kumrithi alijihusisha zaidi na mizozo kwa ajili ya madaraka. Ndio maana utawala wa Zandiye ukadhoofika na mahasimu wake akiwemo Agha Muhammad Khan Qajar wakapata nguvu. Lotfi Ali Khan Zand aliyekuwa mtawala wa mwisho wa ukoo wa Zandiye, alikuwa kijana shujaa na mkweli, hata hivyo kutokana na kutokuwa na tajiriba ya kutosha alishindwa na Agha Muhammad Khan na aliuawa baada ya kuteswa sana. 

Lotfi Ali Khan  Zand

Katika siku kama ya leo miaka 496 iliyopita alizaliwa Luis Vaz de Camoens, malenga mkubwa wa Kireno na mmoja wa wanafasihi wakubwa wa Ulaya huko Lisbon mji mkuu wa Ureno. Mbali na kuwa mshairi, De Camoens alikuwa mpiganaji jasiri. Moja ya kazi muhimu za utunzi za Luis Vaz de Camoens ni ile aliyoipa jina la" The Lusiads."

Luis Vaz de Camoens

Miaka 173 iliyopita utawala wa muda au duru ya pili ya Mfumo wa Jamhuri ulianza huko Ufaransa baada ya wananchi kuendesha mapambano ya ukombozi na kumuondoa madarakani Luis Phillipe Mfalme mbeberu wa nchi hiyo. Utawala wa aina hiyo unajulikana pia katika historia ya Ufaransa kwa jina la "Utawala wa Waandishi wa Habari". Hii ni kwa sababu waandishi habari 11 waliokuwa wakipigania mfumo wa jamhuri chini ya uongozi wa Alphonse de Lamartine malenga na mwandishi wa Kifaransa, ndio waliokuwa wakisimamia utawala huo.

Luis Phillipe

Siku kama ya leo miaka 72 iliyopita sawa na tarehe 24 Februari 1949 wawakilishi wa Misri na utawala wa Kizayuni wa Israel walisaini mkataba wa kusitisha mapigano kati ya pande mbili hizo huko katika kisiwa cha Rhodes ambacho ni moja ya visiwa vinavyopatikana katika bahari ya Aegean. Ni vyema kutaja hapa kuwa baada ya kuundwa serikali ya Kizayuni mwaka 1948 huko katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu, Misri ilishirikiana bega kwa bega na baadhi ya nchi za Kiarabu katika kupigana vita dhidi ya utawala wa Kizayuni. Hata hivyo wanajeshi wa utawala huo walifanikiwa kuingia katika ardhi ya Misri na Lebanon baada ya kuishambulia safu ya vikosi vya mapambano vya Waarabu ambavyo vilikuwa na zana chache za kisasa za kivita na hivyo kutoa pigo kwa vikosi vya nchi za Kiarabu.