Jumamosi, Februari 27, 2021
Leo ni Jumamosi tarehe 15 Rajab 1442 Hijria mwafaka na tarehe 27 Februari mwaka 2021 Miladia.
Tarehe 15 Rajab miaka 1447 iliyopita kundi la kwanza la Waislamu lilianza safari ya kuondoka Makka na kuhamia Uhabeshi barani Afrika. Hijra hiyo iliyokuwa na taathira kubwa katika harakati za Uislamu ilifanyika miaka 8 kabla ya Mtume (saw) kuhamia Madina. Baada ya kushadidi mashaka ya Waislamu waliokuwa wakiteswa na kusumbuliwa na washirikina wa Makka, Mtume Muhammad (saw) aliwaamuru baadhi ya maswahaba zake waelekee katika ardhi ya Uhabeshi barani Afrika kwa ajili ya kujilinda na adha na mateso ya washirikina. Kundi hilo la Waislamu lililojumuisha wanaume 11 na wanawake 4 likiongozwa na Uthman bin Madh'un, lilihamia Uhabeshi na kutayarisha uwanja na mazingira mazuri ya Hijra ya pili ya Waislamu kuelekea katika ardhi hiyo ya Afrika. Kundi hilo la pili liliongozwa na binamu wa Mtume wetu Muhammad (saw), Ja'far bin Abi Twalib. Hijra hizo mbili zilikuwa na mchango mkubwa wa kueneza zaidi dini ya Uislamu barani Afrika. ***
Miaka 1440 iliyopita katika siku kama ya leo, mnamo tarehe 15 Rajab mwaka wa Pili Hijria, Kibla cha Waislamu kilibadilishwa kutoka Baitul Muqaddas na kuelekea Makka kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Mayahudi daima walikuwa wakiwakebehi Waislamu kwa vile walikuwa nao wakielekea kwenye kibla hicho hicho cha Baitul Muqaddas. Hali hiyo iliwatia unyonge Waislamu na hasa Mtume Mtukufu SAW, na kwa minajili hiyo, katika siku kama ya leo Mwenyezi Mungu aliteremsha wahyi kwa Mtume SAW kupitia Malaika Jibrail AS akimtaka aelekee Makka wakati wa ibada ya Swala, badala ya Baitul Muqaddas. ***
Siku kama ya leo miaka 1382 iliyopita mwafaka na tarehe 15 Rajab mwaka 60 Hijria, alifariki dunia Muawiyah bin Abu Sufiyan, adui mkubwa wa Ahlibaiti wa Mtume Muhammad (saw) na mwasisi wa utawala wa Bani Umayyah. Muawiyah alizaliwa miaka 15 kabla ya kuhama Mtume SAW kutoka Makka na kuelekea Madina, na alisilimu wakati wa kukombolewa Makka na jeshi la Kiislamu katika mwaka wa 8 Hijria. Muawiyah alishika Uliwali wa Sham wakati wa Ukhalifa wa Omar bin Khattab na wakati wa uongozi wa Imam Ali bin Abi Twalib (A.S) alianzisha vita vya Siffin kwa kisingizio cha kulipiza kisasi cha kuuawa Othman bin A'ffan. ***
Siku kama ya leo miaka 1380 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, alifariki dunia Bibi Zaynab (AS) mjukuu wa Mtume Mtukufu SAW baada ya kuvumilia mateso na machungu mengi. Bibi Zaynab AS alizaliwa mwaka wa 6 Hijiria na alipata malezi bora kutoka kwa baba yake Imam Ali AS na mama yake Bibi Fatimat Zahra AS. Mwaka 61 Hijria, Bibi Zaynab AS alishiriki katika tukio la Karbala pamoja na kaka yake Imam Hussein AS na watu wengine wa familia ya Mtume SAW. Baada ya kuuawa shahidi Imam Hussein (AS) na wafuasi wake, Bibi Zaynab alikuwa mfikisha ujumbe wa hamasa ya kudumu ya Imam Hussein na wafuasi wake. ***

Tarehe 27 Februari miaka 119 iliyopita alizaliwa mwandishi wa riwaya wa Kimarekani, John Steinbeck katika jimbo la California. Alijiunga na chuo kikuu akiwa na umri wa miaka 17 na kuacha masomo kabla ya kupata shahada yake. Katika kipindi cha ujana wake alijishughulisha na kazi mbalimbali kabla ya kuchagua kazi ya uandishi. Kitabu cha kwanza cha riwaya cha mwandishi huo ni Cup of Gold akichokiandika akiwa na umri wa miaka 27. Mashaka ya kimaisha yalimtayarishia John Steinbeck mazingira mazuri ya kueleza kwa ufasaha maisha ya watu dhaifu na maskini katika jamii ya Marekani. Alikuwa hodari mno katika kueleza mandhari tofauti, matukio na hali mbalimbali. Steinbech ameandika vitabu vingi kama Of Mice and Men, Bombs Away, Travels with Charley, East of Eden, A Russian Jornal na Burning Bright.***
Na katika siku kama ya leo miaka 10 iliyopita, alifariki dunia Waziri Mkuu wa zamani wa Uturuki Necmettin Erbakan (Najmuddin Erbakan) akiwa na umri wa miaka 84. Baada ya kuhitimu katika Chuo Kikuu cha Istanbul, Erbakan alijiunga na Chuo Kikuu cha Aachen nchini Ujerumani ambako alipata shahada ya uzamivu. Mwaka 1969 Erbakan aliingia katika uwanja wa siasa na kuchaguliwa kuwa mbunge. Mwaka 1987 aliongoza chama chenye mielekeo ya Kiislamu cha Refah ambacho kilipata viti vingi vya bunge na kumteuwa kuwa Waziri Mkuu mwaka 1996. Tukio hilo liliwakasirisha mno wanasiasa wa kilaiki wa Uturuki, Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel. Serikali ya Erbakan ilipigwa vita na jeshi la Uturuki na miezi 10 baadaye chama cha Refah kilivunjwa na wanajeshi, na mwanasiasa huyo akapigwa marufuku kujishughulisha na masuala ya kisiasa kwa kipindi cha miaka 5. Profesa Necmettin Erbakan anatambuliwa kuwa baba wa harakati ya Kiislamu ya Uturuki. ***