Feb 28, 2021 03:23 UTC
  • Jumapili, 28 Februari 2021

Leo ni Jumapili 16 Rajab 1442 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 28 Februari 2021 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 499 iliyopita, ilianza harakati ya mapinduzi ya wananchi wa Sweden dhidi ya utawala wa Christiane wa Pili, mtawala wa Denmark ambaye alizikalia kwa mabavu Sweden na Norway. Kiongozi wa harakati hiyo alikuwa Gustav Vasa. Hatimaye kwa msaada wa wakulima, wananchi na wafuasi wa Uprotestanti, Vasa alifanikiwa kuikomboa nchi hiyo kutoka mikononi mwa mtawala Christiane wa Denmark. Baada ya mapinduzi hayo, Gustav Vasa akawa kiongozi wa Sweden. Silsila ya utawala wa Vasa ulioendelea kwa karibu karne tatu, iliondolewa madarakani mwaka 1818 na Marshall Baptiste Bernadotte, mmoja wa makamanda wa jeshi la Ufaransa. ***

Gustav Vasa

 

Siku kama ya leo miaka 488 iliyopita, alizaliwa Michel de Montaigne, mtaalamu wa falsafa wa Ufaransa. Akiwa kijana mwenye umri wa miaka 13, Montaigne alijiunga na chuo kikuu cha Toulouse na kusomea taaluma la sheria. Baada ya masomo yake alianza kufanya kazi za mahakama huku akifanya utafiti juu ya falsafa. Montaigne ameandika vitabu kadhaa, muhimu zaidi kikiwa ni kitabu cha ‘Makala’ chenye juzuu tatu kinachozungumzia masuala mbalimbali. Michel de Montaigne alifariki dunia mwaka 1592. ***

 

Siku kama ya leo miaka 99 iliyopita sawa na tarehe 28 Februari 1922, nchi kongwe ya Misri ilipata uhuru. Misri ilikombolewa na Waislamu miaka 20 baada ya kudhihiri dini tukufu ya Kiislamu. Mwaka 969 nchi hiyo ilidhibitiwa na kutawaliwa na silsila ya wafalme wa Fatimiyya hadi mwaka 1172 ambapo utawala huo ulipinduliwa na Maayyubi. Baada ya hapo Misri ilidhibitiwa na tawala tofauti. Waingereza walianza kuwa na ushawishi huko Misri katika miongo ya mwishoni mwa karne ya 19. Hata hivyo wananchi wa Misri walikabiliana na ukoloni wa Uingereza na mwanzoni mwa Vita vya Kwanza vya Dunia hapo mwaka 1914 Uingereza iliitangaza Misri kuwa chini ya himaya yake. Wananchi wa Misri walidumisha mapambano ya uhuru baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia na kuilazimisha Uingereza kuutambua rasmi uhuru wa nchi hiyo hapo mwaka 1922. ***

Bendera ya Misri

 

Katika siku kama ya leo, miaka 42 iliyopita, hayati Imam Ruhullah Khomeini kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran aliwasili katika mji wa kidini wa Qum baada ya kuwa uhamishoni kwa kipindi cha miaka 15. Imam alipelekwa uhamishoni na utawala wa Shah hapo mwaka 1343 Hijria Shamsia baada ya matukio ya umwagaji damu ya tarehe 15 Khordad mwaka 1342. Tarehe 12 Bahman mwaka 1357 Imam alirejea nchini akitokea Ufaransa na katika siku kama ya leo baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu aliwasili katika mji mtakatifu wa Qum na kuishi huko. Miezi kadhaa baadaye Imam Ruhullah Khomeini alihamia Tehran kutokana na udharura wa kuongoza Mapinduzi.***

Imam Ruhullah Khomeini

 

Miaka 40 iliyopita katika siku kama ya leo, Kamati ya Nia Njema ilianza kazi zake mwanzoni mwa vita vya kichokozi vilivyoanzishwa na utawala wa Baath wa Iraq dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kamati hiyo ilianzishwa kwa pendekezo la Mawaziri wa Jumuiya ya Kiislamu na baada ya kupasishwa na wakuu wa jumuiya hiyo ya OIC. Kamati ya Nia Njema ilikuwa na jukumu la kuhitimisha vita vya Iraq dhidi ya Iran kupitia njia ya amani. Kamati hiyo baadaye ilibadilishwa jina na kufahamika kama Kamati ya Amani. ***

Vita vya Saddam dhidi ya Iran

 

Miaka 35 iliyopita katika siku kama ya leo, inayosadifiana na tarehe 28 Februari 1986, aliuawa Olof Palme Waziri Mkuu wa zamani wa Sweden baada ya kufyatuliwa risasi tumboni kwenye shambulio lililofanyika barabarani katikati mwa Stockholm, mji mkuu wa nchi hiyo. Katika shambulio hilo, Bi. Lisberth mke wa Olof pia alijeruhiwa mgongoni. ***

Olof Palme

 

Katika siku kama ya leo miaka 33 iliyopita, baada ya utawala wa Saddam Hussein wa Iraq kushindwa mtawalia katika medani ya vita na Iran, utawala huo wa Baath ulishambulia kwa makombora ya masafa ya mbali makazi ya raia katika mji wa Tehran. Mashambulio hayo dhidi ya makazi ya raia mjini Tehran katika miji mingine ya Iran yalidumu kwa muda wa mwezi mmoja ambapo mamia ya watu waliuawa na kujeruhiwa. Sababu ya kutekelezwa mashambulio hayo dhidi ya makazi ya raia ilikuwa ni kufidia kushindwa kwake utawala wa Saddam Hussein katika medani ya vita na Iran, na kutoa mashinikizo dhidi ya raia na viongozi wa Iran ili wakubaliane na matakwa yake ya kidhalimu na yasiyo ya kiadilifu. ***

Picha inayoonyesha mashambulio ya anga dhidi ya Tehran

 

Na siku kama ya leo miaka 30 iliyopita inayosadifiana na 28 Februari 1991, George Bush "baba" alitangaza usitishaji vita vya Ghuba ya Uajemi vilivyoendelea kwa muda wa siku 40. Mgogoro huo ulianza mwezi Agosti 1990 baada ya majeshi ya Iraq kushambulia ghafla sehemu ya ardhi ya Kuwait na kuikalia kwa mabavu. Ndege za kijeshi za Marekani, Uingereza na Ufaransa zilianza kuyashambulia majeshi ya Iraq baada ya utawala wa Saddam Hussein kukataa amri ya kuyaondoa majeshi yake nchini Kuwait.

 

Tags