Feb 28, 2021 23:06 UTC
  • Jumatatu tarehe Mosi Machi mwaka 2021

Leo ni Jumatatu tarehe 17 Rajab 1442 Hijria sawa na tarehe Mosi Machi mwaka 2021.

Siku kama ya leo miaka 206 iliyopita, ufalme wa siku mia moja wa Napoléon Bonaparte ulianza nchini Ufaransa baada ya Bonaparte kutoroka sehemu aliyokuwa amebaidishwa katika kisiwa cha Elba. Tarehe 27 mwezi Februari mwaka huohuo akiwa pamoja na wanajeshi elfu moja Napoleon Bonaparte alifanikiwa kutoroka katika kisiwa cha Elba ambako alikaa akiwa uhamishoni kwa kipindi cha miezi kumi na kurejea Ufaransa na utawala wa kifalme ukaanza nchini humo.

Napoléon Bonaparte

Siku kama ya leo miaka 129 iliyopita yaani tarehe 1 Machi mwaka 1892 Miladia, alizaliwa mjini Tokyo mwandishi na mtaalamu mkubwa wa Japan anayejulikana kwa jina la "Rhunosuke Akutagawa". Mwandishi huyo anahesabika kuwa mmoja wa waasisi wa kanuni mpya za fasihi huko Japan. Akutagawa ameacha athari muhimu na miongoni mwake ni vitabu vya "Binti wa Buibui" na "Tushi Gun." Mwandishi huyo alifariki dunia mwaka 1927.

Rhunosuke Akutagawa

Miaka 123 iliyopita katika siku kama leo, kisiwa cha Puerto Rico kilichoko katika ya Bahari ya Atlantic kaskazini mwa Amerika ya Kusini, kilikaliwa kwa mabavu na vikosi vya majeshi ya Marekani baada ya kumalizika vita vya kikoloni vya Uhispania na Marekani. Baada ya Marekani kukitwaa kwa nguvu kisiwa hicho ilikifanya ghala kubwa la silaha, kiasi kwamba Marekani iliasisi kambi 13 za kijeshi kisiwani humo. Kisiwa hicho ambacho mara kwa mara hukumbwa na ukosefu wa amani, miongoni mwa nchi zinazozungumza lugha ya Kihispania katika bara la America.

Puerto Rico