Jumatano tarehe 3 Machi mwaka 2021
Leo ni Jumatano tarehe 19 Rajab 1442 Hijria sawa na tarehe 3 Machi mwaka 2021.
Siku kama ya leo miaka 1433 vilitokea vita vya Tabuk baina ya Waislamu na jeshi la Roma. Vita vya Tabuk ni miongoni mwa vita vya mwisho vya Mtume Muhammad (saw). Sababu ya kutokea vita hivyo ni kwamba, msafara wa kibiashara wa Sham ulimtaarifu Mtume (saw) kwamba mfalme wa Roma ametayarisha jeshi na kulituma Madina. Kwa msingi huo Mtume Muhammad (saw) aliwaanuru Waislamu kujitayarisha kwa ajili ya kukabiliana na jeshi la mfalme wa Roma. Waislamu wengi walijitayarisha kwa ajili ya vita hivyo licha ya masafa marefu, msimu wa joto kali, mashaka ya safari hiyo ngumu na kuwadia msimu wa mavuno. Hatimaye jeshi na wapiganaji elfu 30 la Waislamu liliwasili eneo la vita lakini halikukuta jeshi la mfalme wa Roma eneo hilo.
Japokuwa hakukutokea mapigano wakati huo, lakini tukio hilo lilidhihirisha nguvu ya Waislamu, utayarifu wao wa kukabiliana na majeshi vamizi na moyo wao wa kujitolea kwa ajili ya Allah. Vita hivyo vya Tabuk pia vinajulikana kwa jina la "al Fadhiha" kwa maana ya mfedheheshaji kutokana na kwamba, vililifedhehesha kundi la Waislamu wanafiki waliokataa kujiunga na msafara huo kwa ajili ya kukabiliana na jeshi la Roma.

Miaka 968 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 19 Rajab mwaka 474 Hijria Qamaria Abul Walid Sulaiman bin Khalaf Maliki, faqihi maarufu wa karne ya Tano Hijria Qamaria aliaga dunia huko Andalusia ambayo leo inajulikana kama Uhispania. Alikuwa hafidh na mfasiri wa Qur'ani Tukufu mbali na kubobea katika fasihi na mashairi. Abul Walid awali alifunza Fiqhi na taaluma ya Hadithi za Mtume SAW huko Andalusia na kisha akaendelea kufundisha huko Makka na Baghdad. Kati ya vitabu alivyoandika ni, "Tafsirul Qur'an", "An-Nasikhu wal-Mansukh" na Al-Isharah."

Miaka 318 iliyopita katika siku kama hii ya leo alifariki dunia Robert Hooke, mwanasayansi wa Uiingereza. Hooke alizaliwa mwaka 1635 huko kusini mwa nchi hiyo. Alifanya utafiti mbalimbali katika sayansi ya fizikia, na kutoa mchango mkubwa katika mapinduzi ya sayansi kupitia kazi zake za majaribio na nadharia. Hooke kwa mara ya kwanza aliweza kutumia darubini yake na kutazama chembe ndogo kabisa ya kiumbe hai na kuipa jina la seli. Mwanasayansi huyo wa Uingereza pia alivumbua vifaa kadhaa katika taaluma ya hali ya hewa.
Siku kama ya leo miaka 143 iliyopita, utawala wa Othmaniya na Russia zilisaini mkataba katika eneo lilopewa jina la mkataba huo yaani San Stefano. Makubaliano hayo yalifikiwa baada ya utawala wa Othmaniya kushindwa na Urusi katika vita. Urusi iliuvamia utawala huo kutokana na uchu wake wa kutaka kuzidhibiti ardhi zilizokuwa chini ya himaya ya Othmaniya katika eneo la Balkan.

Siku kama ya leo miaka 59 iliyopita mwafaka na leo alifariki dunia mjini Baghdad Iraq Ayatullahi Sheikh Muhammad Khalisi maarufu kwa jina la Khalisizadeh. Alipanda kwa haraka daraja za kielimu na kujishughulisha na harakati za kitamaduni na kidini, sambamba na kupambana na upenyaji wa ukoloni katika nchi za Kiislamu. Katika harakati hizo za kuwaamsha wananchi wa Iraq Ayatullahi Khalisi alikuwa na lengo la kuwashawishi wananchi wa nchi hiyo kuanzisha mapambano dhidi ya vikosi vya Uingereza vilivyokuwa vimeikalia Iraq. Hatimaye msomi huyo alikamatwa na kubaidishwa nchini Iran. Vitabu vya " Madhalim Inglis dar Baina Nahrain" na "Khodaa dar Tabiiat" ni miongoni mwa vitabu vilivyoandikwa na msomi huyo.
Miaka 29 iliyopita katika siku kama ya leo ilifanyika kura ya maoni kwa ajili ya uhuru na kujitawala Jamhuri ya Bosnia Herzegovina. Kura hiyo ya maoni iliungwa mkono na karibu asilimia 100 ya wananchi walioshiriki katika zoezi hilo na kupelekea nchi hiyo kujitenga na Yugoslavia, baada ya Slovenia na Croatia kufanya hivyo. Jamhuri ya Bosnia Herzegovina ina ukubwa na kilomita mraba karibu 51,129 na inapakana na Croatia kwa upande wa kaskazini na magharibi, Serbia upande wa mashariki na Jamhuri ya Montenegro upande wa kusini mashariki. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa mwaka 1991, asilimia 44 ya jamii ya nchi hiyo ilikuwa ni Waislamu, jamii ambayo inaunda kundi kubwa zaidi la kidini katika jamhuri hiyo ya eneo la Balkan.
Siku kama ya leo miaka 19 iliyopita, Wahindu wenye misimamo mikali walifanya mauaji makubwa dhidi ya Waislamu katika jimbo la Gujarat nchini India. Serikali ya India ilitangaza kuwa, Waislamu 790 waliuawa kwa umati katika mauaji hayo, lakini vyombo vingine huru vilisema kuwa, idadi ya Waislamu waliouawa ilikuwa ni zaidi ya 2000. Kisingizio kilichotumiwa na Wahindu kufanya mauaji ya umati dhidi ya Waislamu wa Gujarat hususan katika mji wa Ahmadabad ni moto uliotokea katika gari moshi lililokuwa limebeba Wahindu lakini baadaye ilibainika kuwa, Waislamu hawakuhusika kwa njia yoyote na tukio hilo. Katika mauaji hayo polisi na maafisa wa jimbo la Gujarat walishirikiana na Wahindu katika mauaji hayo dhidi ya Waislamu.