Mar 04, 2021 00:46 UTC
  • Alkhamisi 4 Machi mwaka 2021

Leo ni Alkhamisi tarehe 20 Rajab 1442 Hijria sawa na tarehe 4 Machi mwaka 2021

Miaka 1429 iliyopita katika siku kama hii ya leo, vilitokea vita vya Yarmuk kati ya jeshi la Kiislamu na jeshi la utawala wa kifalme wa Roma ya Mashariki katika bonde lililojulikana kwa jina hilo huko Palestina. Ushindi wa Waislamu huko Sham, yaani Syria ya sasa ulimpelekea mfalme wa Roma kuandaa jeshi kubwa kwa ajili ya kupigana na Waislamu. Lakini, Waislamu waliweza kutoa pigo kwa wanajeshi wa mfalme wa Roma licha ya kuwa na idadi ndogo ya wapiganaji na suhula chache za kivita. Kufuatia ushindi huo Waislamu walisonga mbele na kufika eneo la Mashariki la Ufalme wa Roma na mwaka mmoja baada ya hapo Waislamu wakafanikiwa kuchukua udhibiti wa mji wa Baitul Muqaddas pasina umwagaji damu.

Tarehe 4 Machi miaka 198 iliyopita, vikosi vya jeshi la Ugiriki vilifanya mauaji makubwa ya halaiki dhidi ya Waislamu elfu 12 wakati wa vita vyao dhidi ya jeshi la ufalme wa Othmania katika mji wa Tripolitsa. Makundi ya Wagiriki waliokuwa wakiungwa mkono na nchi kadhaa za Ulaya, yaliungana na kutekeleza mauaji hayo katika muongo wa mwanzoni mwa karne ya 19, yaani mwaka 1822. Kufuatia mauaji hayo mwezi Novemba mwaka 1824 majeshi ya utawala wa Kiothmani yaliamua kulipiza kisasi kwa kuua kundi la Wagiriki.

Siku kama ya leo miaka 173 iliyopita, yalianza mapambano ya wapigania uhuru wa Hungary dhidi ya serikali ya Austria. Siasa za kibeberu za Klemens Metternich, Kansela wa wakati huo wa Austria zilisababisha mapinduzi mwaka 1848 katika ardhi zisizo za Ujerumani zilizokuwa chini ya himaya ya Austria, ikiwemo Hungary. Uasi wa wananchi wa Hungary ulioibuka kutokana na dhulma ya Waaustria, ulienea kwa kasi kote nchini humo. Licha ya kutishiwa na serikali kuu, wanamapinduzi walitangaza nchi hiyo kuwa jamhuri tarehe 4 mwezi Aprili mwaka 1849 baada ya kushtadi harakati zao huko Hungary. Hata hivyo kwa msaada wa utawala wa Tsar wa Urusi, ufalme wa Austria uliyakandamiza mapinduzi hayo na kuwanyonga viongozi wake.

Na siku kama ya leo miaka 54 iliyopita sawa na tarehe 14 Esfand mwaka 1346 kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, alifariki dunia Dakta Muhammad Musaddiq, Waziri Mkuu na mmoja wa wanasiasa mashuhuri wa Iran. Alizaliwa mjini Tehran mwaka 1261 Hijria Shamsia. Mwaka 1299 Hijria Shamsia ikiwa ni baada ya kuhudumu kama Waziri wa Fedha na Waziri wa Mambo ya Nje, Musaddiq alichaguliwa kuwa mwakilishi wa watu wa Tehran bungeni. Alifanya jitihada kubwa za kutaifishwa sekta ya mafuta nchini Iran na mwaka 1329 Hijria Shamsia alifanikiwa kupasisha kanuni ya kutaifishwa mafuta bungeni kwa himaya ya makundi ya Kiislamu chini ya uongozi wa Ayatullah Kashani. Baadaye aliondolewa madarakani katika mapinduzi yaliyoongozwa na Marekani tarehe 28 Mordad mwaka 1332 Hijria na kufungwa jela miaka mitatu. Baada ya kutumikia kifungu hicho Musaddiq alibaidishiwa katika kijiji kimoja huko magharibi mwa Tehran na alifariki dunia miaka kadhaa baadaye katika siku kama ya leo.

Dakta Muhammad Musaddiq