Jumapili, 7 Machi, 2021
Leo ni Jumapili tarehe 23 Rajab 1442 Hijria sawa na tarehe 7 Machi 2021 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 747 iliyopita, alifariki dunia mwanafalsafa wa Kitaliano Thomas Aquinas. Alizaliwa mwaka 1225 katika mji wa Napoli na kupata elimu ya dini katika mji huo hadi Chuo Kikuu. Mwanafikra huyo alibuni falsafa makhususi na kutambua kwamba saada na ufanisi mkubwa zaidi wa mwanadamu ni kupiga hatua za kuelekea kwenye ukamilifu wa kiroho na kwa Mwenyezi Mungu. Aquinas kama alivyokuwa Aristotle, aliamini kuwa ndani ya nafsi ya kila mwanadamu kuna nguvu inayoweza kumfikisha kwenye ukamilifu wa kiroho. Vilevile aliamini kwamba teolojia haipingani na sayansi kwani kila moja kati ya viwili hivyo inataka kujua hakika na ukweli. Itikadi za Aquinas na misimamo yake ya kutumia akili na mantiki ambayo ilikuwa ikipingwa vikali na kanisa katika karne za kati, ilisaidia sana kueneza elimu. ***

Miaka 256 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Nicephore Niepce mwanakemia wa Kifaransa na mmoja wa waasisi wa fani ya upigaji picha. Niepce alikuwa mtu wa kwanza aliyefanikiwa kupiga picha ya kwanza duniani. Baada ya hapo, Nicephore alitengeneza kamera ya kupiga picha kwa kushirikiana na marafiki zake. Mwanakemia huyo wa Ufaransa aliaga dunia mwaka 1833. ***

Katika siku kama ya leo miaka siku kama ya leo miaka 85 iliyopita, vikosi vya jeshi la Ujerumani ya Kinazi vilifanya mashamulizi ya kwanza baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia. Wanajeshi wa Ujerumani walipuuza makubaliano ya Warsaw na Locarno kwa amri ya Adolph Hitler na hivyo kuingia eneo la Ranani. Kwa mujibu wa makubaliano hayo ya Locarno na Warsaw, eneo la Ranani lililokuwa likigombaniwa kati ya Ufaransa na Ujerumani lilitangazwa kuwa eneo lisiloegmea upande wowote. Hata hivyo jeshi la Ujerumani liliamua kuliteka na kulikalia kwa mabavu eneo hilo katika siku kama hii ya leo. ***

Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita aliaga dunia Ayatullah Abdur Rahim Rabani Shirazi, fakihi na mwanamapambano asiyechoka. Alizaliwa mwaka 1301 Hijria Shamsia katika mji wa Shirazi moja ya miji ya kusini mwa Iran. Mwaka 1342 Hijria Shamsia, Abdur Rahim Rabani Shirazi alianza kushiriki katika harakati za mapambano dhidi ya utawala wa wakati huo wa Shah na kudumu katika harakati hizo. Mara kadhaa alikamatwa na kutiwa jela sambamba na kubaidishwa katika maeneo mbalimbali. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu alichaguliwa kuwa mwakilishi wa Majlisi ya ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran). Alimu huyu aliutumia umri wote kwa ajili ya kuuhudumia Uislamu na Waislamu. ***

Na miaka 37 iliyopita katika siku kama ya leo, aliuawa shahidi Muhammad Ibrahim Hemmat mmoja wa makamanda mahiri wa kipindi cha vita vya Kujihami Kutakatifu. Muhammad Ibrahim Hemmat alizaliwa katika familia iliyokuwa imeshikamana vizuri na dini. Baada ya kukamilisha masomo yake alianza kufundisha katika maeneo ya vijijini. Ni katika kipindi hicho ndipo alipokuwa vakiwafahamisha wanafunzi kuhusu utambulisho wa kidikteta wa utawala wa Shah. ***
