Mar 07, 2021 23:05 UTC
  • Jumatatu, Machi 8, 2021

Leo ni Jumatatu tarehe 24 Rajab 1442 Hijria sawa na tarehe 8 Machi mwaka 2021 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1435 iliyopita, ngome ya Khaibar ambayo ilikuwa moja ya ngome madhubuti na imara zaidi za Mayahudi ilitekwa na kudhibitiwa na Imam Ali (as), mkwewe Mtume Mtukufu (saw). Mayahudi ambao hawakuacha kueneza uadui wao wa jadi dhidi ya Uislamu walikuwa wakiendeshea njama zao huko Khaibar kaskazini mwa mji mtakatifu wa Madina, ambako walikuwa wamejenga ngome saba muhimu, ambazo waliamini kuwa hazingepenyeka wala kudhibitiwa na adui. Katika mwaka wa saba Hijiria Mtume (saw) alibashiri kutekwa kwa mji wa Khaibar. Muda si mrefu na baada ya kuvunja mzingiro uliokuwa umewekwa na maadui, jeshi la Kiislamu lilifanikiwa kudhibiti ngome kadhaa kati ya hizo saba isipokuwa mbili. Hatimaye Mtume aliwahutubu makamanda wa jeshi hilo kwa kusema: 'Kesho nitampa benderea mtu ambaye anampenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake, naye Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanampenda pia, na Mwenyezi Mungu ataiteka ngome hii kupitia mikono yake. Siku iliyofuata, Mtume alimpa Imam Ali (as) uongozi wa jeshi ambapo alipigana vita vya kishujaa na hivyo kuweza kudhibiti ngome ya mwisho ya Mayahudi huko Khaibar.

Mabaki ya ngome ya Khaibar

Siku kama ya leo miaka 1103 iliyopita, Abu Nasr Muhammad Farabi, Mwanafalsafa, mwanahesabati na msomi mashuhuri wa Iran aliaga dunia. Alizaliwa mwaka 259 Hijiria katika mji wa Farab ilioko kusini mwa nchi ya Kazakhstan  ya leo. Baada ya kupata masomo ya msingi katika mji huo, Farabi aliamua kwenda mjini Baghdad huko Iraq ili kuendeleza masomo yake na hasa ya mantiki na falsafa. Werevu mkubwa aliokuwanao ulimuwezesha kusoma masomo mengi ya zama zake lakini alizingatia zaidi somo la falsafa. Mwanafalsafa huyo  mashuhuri aliyefahamika zaidi kwa majina ya  Muallim ath-Thani, Ustadh wa Falsafa na Malik al-Hukamaa alifanya juhudi kubwa za kuunganisha fikra za wanafalsafa tofauti na hasa za Aristotle na Platon, akiamini kulikuwa na falsafa moja tu.

Abu Nasr Muhammad Farabi

Siku kama ya leo miaka 230 iliyopita alifariki dunia Sayyid Muhammad Mahdi Bahrul-Ulum, mtaalamu wa elimu ya irfan na msomi mkubwa wa Kiislamu. Alizaliwa mwaka 1155 Hijiria katika mji mtukufu wa Karbala, Iraq na kusoma elimu za dini ya Kiislamu katika mji huo kwa baba yake mzazi ambaye alikuwa mmoja wa maulama wakubwa wa zama hizo na kwa wasomi wengine. Akiwa kijana, Allamah Bahrul-Ulum alifanikiwa kukwea daraja za juu za elimu na kufikia ijtihadi, na baada ya hapo akaelekea Najaf. Akiwa mjini hapo haraka alifikia daraja ya umarjaa sambamba na kuteuliwa kuwa mkuu wa hauzana chuo kikuu cha kidini cha mji huo mtakatifu. Alifanya mabadiliko katika chuo hicho kikongwe. Msomi huyo alijishughulisha na kazi mbalimbali za kijamii na alipendwa sana na watu. Sayyid Bahrul-Ulum aliiishi miaka saba mjini Mash’had, Iran na miaka miwili huko Hijaz, Saudia ambapo pia aliendelea kujishughulisha na kazi za kielimu kiasi cha kumfanya imam wa Msikiti wa Makkah wakati huo, kujiunga na madh’hab ya Kishia. Aidha aliwalea wanafunzi wengi, bila kusahau kazi ya kufafanua vitabu. Maulama kama vile Sheikh Jafar Kashif al-Ghitaa, Mulla Ahmad Naraqi, Muhammad Baqir Shafati, Sayyid Muhammad Jawad Aamili…ni baadhi ya wanafunzi wa Sayyid Bahrul-Ulum. Vitabu vya ‘Al-Maswaabih’ ‘Mishkaatul-Hidaayah’ ‘Fawaaidulr-Rijaaliyah’ na diwani ya mashairi ni miongoni mwa athari za msomi huyo.

Sayyid Muhammad Mahdi Bahrul-Ulum

Siku kama ya leo miaka 124 iliyopita, aliuawa Sayyid Jamaluddin Asadabadi mwanazuoni na mmoja wa viongozi wa mapambano dhidi ya ukoloni wa kimaitaifa dhidi ya Waislamu. Sayyid Jamaluddin alizaliwa huko Asadabad magharibi mwa Iran na kupata elimu katika fani za falsafa, nujumu na historia. Mbali na kufahamu lugha za Kiarabu, Kifarsi na Kituruki, Sayyid Jamaluddin Asadabad alikuwa pia mtaalamu katika lugha za Kiingereza, Kifaransa na Kirusi.

Sayyid Jamaluddin Asadabadi (Afghani)

Siku kama ya leo miaka 53 iliyopita, inayosadifiana na 8 Machi 1968 ilianza Harakati ya Ukombozi ya Moro dhidi ya utawala wa dikteta Ferdinand Marcos nchini Ufilipino. Dikteta Marcos alikuwa mshirika na muitifaki mkubwa wa Marekani na katika utawala wake wa kidikteta, maelfu ya Waislamu wa Ufilipino waliuawa au kufungwa jela. Harakati ya Ukombozi ya Moro ilipambana kwa ajili ya kupigania haki za Waislamu, na ilihesabiwa kuwa harakati kubwa zaidi iliyopinga utawala wa Marcos nchini Ufilipino. Baada ya Marcos kuondoka madarakani mwaka 1986, harakati ya Moro ilikubali kutia saini makubaliano ya amani na serikali ya Manila.

Dikteta Ferdinand Marcos

Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 8 Machi 1985, ulitokea mlipuko mkubwa wa bomu la kutegwa garini mjini Beirut, Lebanon ambapo watu wasiopungua 45 waliuawa na wengine 175 kujeruhiwa. Mlipuko huo ulitokea karibu na msikiti unaotumiwa na Waislamu wa madhehebu ya Shia. Mlipuko huo ulifuatilia mlipuko mwengine mkubwa zaidi uliotokea mwaka 1983, ambapo watu wasiopungua 61 waliuawa kusini mwa bandari ya Tyre, nchini Lebanon.

Katika siku kama hii ya leo mwaka 10 uliopita alifariki dunia Dakta Iraj Afshar mtaalamu wa masuala ya Iran na mwandishi wa Kiirani. Dakta Afshar alizaliwa mwaka 1304 Hijria Shamsiya huko Yazd katikati mwa Iran. Iraj Afshar alisomea fani ya sheria katika Chuo Kikuu cha Tehran na kuwasilisha tasnifu yake ya duru ya udaktari chini ya anwani ya "Jamii ya waliowachache nchini Iran". Mwaka 1331 Hijria Shamsiya Dakta Afshar alianzisha jarida alililolipa jina la "Utamaduni wa Iran". Mbali na kufundisha, msomi huyo wa Kiirani alifanya utafiti wa thamani kuhusu masuala ya Iran na kuhusu masuala ya uandishi ambapo utafiti wake huo ulichapishwa katika majarida yenye itibari ya nchini Iran na nje ya nchi.

Dakta Iraj Afshar

Na leo tarehe 8 Machi inatambuliwa kuwa Siku ya Kimataifa ya Mwanamke. Awali siku hii ilianzishwa kama tukio la kisiasa la kisoshalisti lakini baadaye liliingia katika utamaduni wa nchi nyingi duniani. Siku ya Kimataifa ya Mwanamke inayoadhimishwa katika nchi nyingi duniani imepoteza sura yake ya kisiasa na sasa limekuwa tukio linalotumiwa na wanaume kudhihirisha upendo wao kwa wanawake. Mwaka 1977 Umoja wa Mataifa iliitangaza rasmi siku hiyo kama Siku ya Haki za Wanawake na Amani ya Kimataifa.