Jumanne tarehe 9 Machi 2021
Leo ni Jumanne tarehe 25 Rajab 1442 Hijria sawa na tarehe 9 Machi mwaka 2021.
Siku kama ya leo miaka 1259 iliyopita, aliuawa shahidi Imam Musa Kadhim (as) mmoja kati ya wajukuu watoharifu wa Mtume Mtukufu (saw). Imam Kadhim (as) alizaliwa mwaka 128 Hijiria huko katika eneo la Ab'waa lililoko baina ya miji mitakatifu ya Madina na Makka. Mtukufu huyo kwa miaka 20 alipata malezi na elimu muhimu kutoka kwa baba yake ambaye ni Imam Jaafar as-Swadiq (as). Baada ya kuuawa baba yake huyo, Imam Kadhim (as) alipata fursa ya kuuongoza umma wa Kiislamu kwa muda wa miaka 35, ambapo alipata mateso na mashaka mengi katika njia hiyo. Katika zama zake ambazo zilisadifiana na ustawi mkubwa wa utamaduni na elimu ya Kiislamu pamoja na kuimarishwa uhusiano na mataifa ya kigeni, Imam alifanya juhudi kubwa za kueneza mafunzo ya Kiislamu katika mataifa hayo kupitia wanafunzi wake. Mbali na hayo, Imam pia aliendesha mapambano makali dhidi ya watawala dhalimu wa Bani Abbas. Hatimaye Haroun ar-Rashid kutoka ukoo wa Bani Abbas aliyehofia sana kuporomoka kwa utawala wake, alimfunga jela Imam Kadhim (as). Licha ya kufungwa jela lakini Imam (as) hakusimamisha shughuli zake za kuhubiri dini na kupambana na madhalimu bali alifundisha na kuwaelimisha watu waliokuwa pembeni yake hali halisi ya mambo iliyotawala katika zama hizo. Hatimaye Haroun ar-Rashid alifanya njama ya kumuua Imam kwa kumpa sumu. Huku tukitoa mkono wa pole kwa Waislamu wote duniani kwa mnasaba huu mchungu wa kuuawa shahidi Imam Kadhim (as), tunakunukulieni hapa moja ya semi zake zenye mafunzo na busara kubwa. Imam anasema: 'Njia bora zaidi ya kumkurubia Mwenyezi Mungu baada ya kumjua ni kusimamisha Swala, kuwatendea wema wazazi wawili na kuachana na husuda na majivuno.'

Miaka 567 iliyopita sawa na tarehe 9 mwezi Machi mwaka 1454 alizaliwa mvumbuzi na baharia wa Kiitalia kwa jina la Americo Vespucci. Vespucci alijishughulisha na kazi za melini kutokana na hamu yake kubwa ya kupenda ubaharia aliyoionyesha tangu akiwa kijana na hivyo kupewa cheo cha unahodha. Baharia Americo Vespucci alisafiri mara nne katika nchi isiyojulikana ambayo hadi wakati huo ilikuwa haina jina na baadaye ikapatiwa jina la mvumbuzi huyo wa Kiitalia yaani Amerika.
Siku kama ya leo miaka 29 iliyopita Menachem Begin mmoja wa waasisi wa utawala haramu wa Kizayuni na chama cha mrengo wa kulia cha Likud aliangamia. Begin alizaliwa huko Russia mwaka 1913 na baba yake ambaye alikuwa Mzayuni mwenye misimamo mikali alikuwa na taathira na nafasi kubwa katika malezi yake. Akiwa na umri wa miaka 12, Menachem Begin aliasisi kikosi cha vijana wa Kizayuni na miaka miwili baadaye baada ya kuhajiri huko Palestina mwaka 1942 akachaguliwa kuwa kamanda wa Taasisi ya kigaidi yenye misimamo ya kufurutu ada. Taasisi hiyo ilikuwa moja kati ya makundi makuu ya kigaidi na yenye misimamo mikali ya Kizayuni iliyoshiriki kwa kiasi kikubwa katika kuwauwa raia wa Palestina na kuwafukuza katika ardhi zao.
Miaka 25 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Sheikh Muhammad Ghazali mwanazuoni na mwanamageuzi mkubwa wa Misri. Alizaliwa mwaka 1917 huko nchini Misri. Akiwa na umri wa miaka 10 tu, tayari Muhammad Ghazali alikuwa amehifadhi Qur'ani Tukufu yote. Muhammad Ghazali alihitimu Chuo Kikuu akiwa na umri wa miaka 24. Fikra zake zilijengeka juu ya msingi wa mageuzi ya maarifa ya kidini, kukurubisha baina ya madhehebu za Kiislamu na kupinga fikra za kikaumu. Muhammad Ghazali aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 79 kwa mshtuko wa moyo na kuuzikwa katika makaburi ya Baqii mjini Madina.

Katika siku kama ya leo miaka 8 iliyopita aliaga dunia Ayatullah Sayyid Mujtaba Musavi Lari ambaye alikuwa miongoni mwa maulama wakubwa wa Kiislamu. Alizaliwa mwaka 1314 Hijria Shamsia katika eneo la Lar nchini Iran na kupata elimu ya msingi katika eneo hilo. Mwaka 1332 alielekea Qum kwa ajili ya elimu ya juu ya Kiislamu. Huko Qum, Ayatullah Musavi Lari aliasisi Kituo cha Kueneza Maarifa ya Kiislamu Duniani ambacho kilikuwa kikisambaza vitabu vyake vilivyotarjumiwa kwa lugha hai za dunia. Mwaka 1372 Hijria Shamsia Academia ya Sayansi ya Jamhuri ya Azarbaijan ilimtunuku shahada ya uzamivu kutokana na taathira kubwa ya vitabu vyake vilivyotarjumiwa kwa lugha ya Kirusi. Ayatullah Mujtaba Lari aliaga dunia siku kama ya leo tarehe 19 Esfand katika Hospitali ya Imam Ridha (as) baada ya kusumbuliwa na maradhi kwa kipindi kirefu.