Mar 16, 2021 01:42 UTC
  • Jumanne tarehe 16 Machi mwaka 2021

Leo ni Jumanne tarehe Pili Shaabani mwaka 1442 Hijria sawa na Machi 16 mwaka 2021.

Katika siku kama ya leo miaka 26 iliyopita, sawa na tarehe 26 mwezi Esfand mwaka 1373 Hijria Shamsiya aliaga dunia Hujjatul Islam Walmuslimin Sayyid Ahmad Khomeini, mwana wa Imam Ruhullah Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Sayyid Ahmad Khomeini alizaliwa mwaka 1324 Hijria Shamsiya katika mji mtukufu wa Qum nchini Iran na kuanza kujifunza elimu ya kidini kwa baba yake. Sayyid Ahmad Khomeini alikuwa na nafasi muhimu katika kuwaunganisha wanamapinduzi na Imam Khomeini wakati wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.

Sayyid Ahmad Khomeini

Siku kama ya leo miaka 44 iliyopita, Kamal Fouad Jumblatt mwanasiasa mahiri wa Lebanon aliuawa.  Alizaliwa Disemba 6 mwaka 1917 huko Moukhtara kusini mwa Beirut. Mwaka 1952 na kuendelea, Kamal Fouad Jumblatt  alikuwa mwanasiasa wa mrengo wa upinzani na akafanikiwa kumuondoa madarakani Bechara El Khoury Rais wa muda wa wakati huo wa Lebanon. Hatimaye Kamal Fouad Jumblatt  aliuawa na wapinzani wake katika siku ma ya leo  akiwa na umri wa miaka 60. 

Kamal Fouad Jumblatt

Siku kama ya leo miaka 81 iliyopita, alifariki dunia Bi Selma Lagerlof mwandishi wa Sweden. Lagerlof alizaliwa mwaka 1858 na baada ya kumaliza masomo yake akaanza kujishughulisha na ukufunzi na uandishi wa hadithi na hekaya. Lagerlof alikuwa mwanamke wa kwanza kutunukiwa tuzo ya Nobel katika fani ya fasihi mwaka 1909.

Bi Selma Lagerlof

Miaka 82 iliyopita katika siku kama ya leo, katika hali ambayo Vita vya Pili vya Dunia havikuwa vimeanza, nchi ya Czechoslovakia ilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na Ujerumani ya Kinazi. Kwa utaratibu huu, Jamhuri ya Czechoslovakia ikawa nchi ya pili baada ya Austria kukaliwa kwa mabavu na Adolph Hitler.

Czechoslovakia 

Na siku kama ya leo miaka 1046 iliyopita alizaliwa malenga na arif mkubwa wa Kiislamu wa karne ya tano Hijria Khaja Abdullah Ansari katika mji wa Herat nchini Afganistan. Alipewa lakabu ya Mzee wa Herat. Khaja Abdullah Ansari ameandika vitabu vingi vya elimu ya irfani kwa lugha za Kiarabu na Kifarsi kwa sura ya mashairi na nudhumu, mashuhuri zaidi vikiwa ni "Munajat Nameh", "Mahabbat Nameh" na "Zadul Arifin". Vilevile ameandika tafsiri ya Qur'ani Tukufu aliyoipa jina la "Kashful Asrar."

Khaja Abdullah Ansari