Mar 17, 2021 23:15 UTC
  • Alkhamisi, tarehe 18 Machi, 2021

Leo ni Alkhamisi tarehe 4 Shaabani 1442 Hujria sawa na Machi 18 mwaka 2021.

Siku kama ya leo miaka 1416 iliyopita, yaani tarehe 4 Shaaban mwaka 26 Hijria, alizaliwa Hadhrat Abbas Bin Ali Bin Abi Talib, mashuhuri kwa lakabu ya Abul Fadhl. Mama yake ni Ummul-Banina, ambaye aliolewa na Imam Ali bin Abi Twalib (as) baada ya kufariki dunia Bibi Fatima Zahra (as). Abul Fadh al-Abbas alikulia katika familia ya watu adhimu kama vile baba yake Imam Ali (as), kaka zake Imam Hassan na Hussein na dada yake mtukufu Zaynab (as). Alimpenda sana kaka yake Hussein Bwana wa Mashahidi kiasi kwamba alisabilia katika ardhi ya Karbala kwa lengo la kumtetea yeye na risala yake kwa nguvu zake zote. Abbas alifahamika mno kutokana na elimu, ukweli na uchaji Mungu wake. Kutabahari kwake katika elimu kuliwafanya watu wengi wamrejee kwa ajili ya kutatuliwa masuala mbalimbali ya kielimu. Siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa Abul Fadhl Abbas inajulikana hapa nchini Iran kama Siku ya Vilema wa Vita. Aidha katika siku ya kuzaliwa mtukufu huyo, watu wa Iran huwa wanawakumbuka na kuwaenzi mashujaa waliosimama imara katika vita vya kulazimishwa vya utawala wa zamani wa Iraq dhidi ya Iran. Kwa mnasaba huu, Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatoa mkono wa baraka kwa Waislamu na wapigania uhuru kote duniani.

Siku kama ya leo miaka 1002 iliyopita, sawa na tarehe 4 Shaban 440 Hijiria, alifariki dunia Abu Said Abul-Khayr, mtaalamu wa elimu ya Kumjua Mwenyezi Mungu (irfan) na malenga wa Iran akiwa na umri wa miaka 83. Abu Said alizaliwa mwaka 357 Hijiria na kujifunza elimu ya hisabati na historia ya wafalme. Aidha alitabahari katika elimu za tafsiri ya Qur’ani, Hadithi na fiqhi (sheria za Kiislamu), huku akipata elimu ya irfani kutoka kwa wanazuoni mashuhuri wa elimu hiyo wa karne ya nne na ya tano Hijiria. Kitabu cha ‘Asraarut-Tawhid’ ni moja ya turathi za Abu Said Abul-Khayr. Aidha alipendelea sana kusoma mashairi.

Mahali lilipo kaburi la Abu Said Abul-Khayr

Miaka 163 iliyopita siku kama leo, alizaliwa mvumbuzi mashuhuri wa Kijerumani, Rudolf Diesel, ambaye alibuni injini ya diseli. Diesel alifanya utafiti na uhakiki mkubwa kuhusu injini za mitambo mbalimbali na akafanikiwa kuvumbua chombo ambacho kinaweza kuzalisha nishati kubwa zaidi bila ya kuhitaji umeme lakini kwa kutumia nishati ya kawaida na rahisi zaidi. Chombo hicho ambacho kilipewa jina lake mwenyewe la Diesel kilileta mabadiliko makubwa katika sekta ya viwanda na usafirishaji kwa kadiri kwamba licha ya maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia lakini injini za diseli zingalia zinatumika kwa kuwa ni zenye nguvu kubwa na zinazotumia nishati ndogo. Rudolf Diesel alifariki dunia mwaka 1913.

Rudolf Diesel

Siku kama ya leo miaka 59 iliyopita, hatimaye mapambano ya wananchi Waislamu wa Algeria yaliyoanzishwa kwa lengo la kuikomboa nchi hiyo na kukomesha uvamizi wa kikoloni wa Ufaransa yalipata ushindi baada ya miaka minane ya vita vikali. Watu milioni moja waliuawa katika vita hivyo. Kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano wa pili wa Evian, Ufaransa ilitambua uhuru wa Algeria na kuwaondoa wanajeshi wake nchini humo. Hata hivyo jeshi la siri la Ufaransa liliendeleza operesheni za kigaidi kwa muda nchini Algeria. Ni vyema kuashiria hapa kuwa, Algeria wakati huo ilikuwa ikiongozwa na Yusuf bin Khada na baadaye nchi hiyo ikawa chini ya utawala wa Ahmad bin Bella.