Ijumaa, Machi 19, 2021
Leo ni Ijumaa tarehe 5 Shaabani 1442 Hijria sawa na Machi 19 mwaka 2021 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 1404 iliyopita alizaliwa Imam Ali bin Hussein (AS) maarufu kwa laqabu ya Zainul Abidin katika mji mtakatifu wa Madina. Mtukufu huyo ni mwana wa Imam Hussein bin Ali Bin Abi Twalib, mjukuu wa Bwana wetu Muhammad (SAW). Alikuwa kinara wa elimu, uchamungu, wema ukarimu na upendo. Miongoni mwa sifa kuu za Imam Zainul Abidin ni kufanya ibada na kusali Swala za usiku. Alikuwa mwingi wa ibada na alipewa laqabu ya Sajjad kwa maana ya mwenye kusujudu sana na Zainul Abidin kwa maana ya 'Pambo la Wafanya Ibada' kutokana na sijda zake ndefu katika Swala. Imam Zainul Abidin alichukua jukumu la kuendeleza ujumbe wa mapambano ya Imam Hussein ya kupambana na ufisadi na dhulma ya watawala wa Bani Umayyah baada ya kuuawa baba yake katika medani ya Karbala. Aliishi miaka 35 baada ya tukio hilo chungu na aliuawa shahidi na mtawala wa Bani Ummayah Hisham bin Abdul Malik. Athari maarufu zaidi ya mtukufu huyo ni kitabu cha dua na miongozo ya Kiislamu cha al Sahifa as Sajjadiyya.

Miaka 1129 iliyopita katika siku kama ya leo alifariki dunia tabibu na mwanakemia mtajika wa ulimwengu wa Kiislamu na mvumbuzi wa alkoholi kwa jina la Muhammad bin Zakaria Razi. Tabibu Razi alizaliwa mwaka 251 Hijria katika mji wa Rei kusini mwa Tehran ya leo. Mwanakemia huyo mkubwa alianza kujishughulisha na kazi ya usonara na baadaye kemia. Tabibu na mkemia Muhammad bin Zakaria Razi alijifunza pia elimu nyingine kama vile tiba, mantiki na falsafa. Baadae Razi alifanikiwa kutengeneza asidi ya Sulfuriki kwa kustafidi na mada asilia. Msomi huyo wa Kiislamu Muirani alikuwa shakhsia wa kwanza kuvumbua alkoholi.
Siku kama ya leo miaka 137 iliyopita alizaliwa Sir Norman Haworth, mtaalamu wa kemia wa Uingereza. Sir Haworth alifanya utafiti na uhakiki mwingi wa kisayansi kuhusu haidrokaboni na akafanikiwa kubuni mpango mpya kwa ajili ya muundo wa molekuli ya sukari. Vilevile Sir Haworth alifanya utafiti na majaribio kuhusu vitamini C ambayo muundo wa molekuli yake unashabihiana na sukari na akatayarisha aina yake ya kutengenezwa viwandani kwa jina la asidi askobiki. Mwaka 1937 Sir Norman Haworth alitunukiwa tuzo ya kemia ya Nobel kutokana na uhakiki na utafiti wake mkubwa. Alifariki dunia mwaka 1950.
Miaka 57 iliyopita katika siku kama ya leo, Imam Khomeini mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitoa hotuba na kuwataka wananchi wa Iran wasifanye sherehe za Nairuzi za mwaka mpya wa Kiirani wa 1342 ili kulalamikia hatua zisizo za kisheria za utawala wa kifalme wa Kipahlavi. Nairuzi ni sherehe za kitaifa za Wairani ambazo hufanywa kila mwanzoni mwa mwaka wa Kiirani. Katika kipindi chote cha mwaka 1341 Hijria Shamsia utawala wa kidikteta wa Shah ulichukua hatua mbalimbali kwa ajili ya kuimarisha misingi ya utawala wake na kwa ajili ya kuyaridhisha madola ya kigeni hususan Marekani. Imam Khomeini kwa uono mpana na kutazama mustakbali wa mambo akiwa pamoja na maulama wengine aliitangaza sikukuu ya Nairuzi kuwa mambolezo ya umma ili kubatilisha propaganda za utawala wa Kipahlavi za kuhalalisha hatua zake za hiana. Kwa muktadha huo, wananchi na viongozi wa kidini walifanya vikao vya maombolezo katika pembe mbalimbali za Iran. Ubunifu huu wa Imam Khomeini ulikuwa na taathira kubwa kiasi kwamba, katika siku ya pili ya sikukuu ya Nairuzi maafisa wa utawala wa Shah walishambulia mkusanyiko wa matalaba (wanafunzi wa masomo ya dini) katika mji wa Qum waliokuwa wakifanya maombolezo na kuwauwa shahidi na kuwajeruhi baadhi yao.
Siku kama ya leo miaka 33 iliyopita inayosadifiana na tarehe 19 Machi 1987 alifariki dunia Louis de Broglie, ambaye alikuwa wa mwisho katika kizazi cha waasisi wa fizikia ya kisasa akiwa na umri wa miaka 95. Louis de Broglie alizaliwa mwaka 1892 na baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia alianza utafiti wa elimu ya fizikia. Mtaalamu huyo wa fizikia wa Ufaransa alitatua masuala mengi ya elimu hiyo kwa nadharia yake mashuhuri ya Wave Particle Duality. Mwaka 1929 alitunukiwa tuzo ya fizikia ya Nobel.