Mar 20, 2021 23:01 UTC
  •  Jumapili, Machi 21, 2021

Leo ni tarehe Mosi Farvardin mwaka 1400 Hijria Shamsiya sawa na tarehe Saba Shaaban 1442 Hijria inayosadifiana na 21 Machi 2021

Wapenzi wasikilizaji tunafungua ukurasa mpya wa mwaka 1400 Hijria Shamsiya kwa kuwapa salamu za kheri na fanaka kwa mnasaba huu.

Leo ni tarehe Mosi Farvardin inayosadifiana na siku ya kwanza ya mwaka wa Kiirani ya Hijria Shamsiya. Siku hii ambayo ni mwanzo wa msimu maridadi wa machipuo hapa nchini ni maarufu kwa jina la Sikukuu ya Nowruz. Nowruz ni moja kati ya sherehe za kale zaidi duniani na ilianza kusherehekewa zaidi ya miaka 3000 iliyopita. Mbali na Iran nchi ambazo husherehekea Nowruz ni pamoja na Afghanistan, Jamhuri ya Azerbaijan, Albania, Kyrgyzstan, Turkmenistan, Macedonia, India, Uturuki, Jamhuri ya Tatarstan nchini Russia, Sudan na Zanzibar nchini Tanzania. Mwaka 2010 Umoja wa Mataifa ulitangaza rasmi tarehe Mosi Farvardin kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Nowruz. Umoja wa Mataifa umeitambua Siku ya Nowruz kama siku kuu ya kale ambayo huadhimishwa wakati wa kuwadia msimu wa machipuo na kuhuishwa tena mazingira.

Meza ya 'Haft Seen' ambayo huandaliwa wakati wa sherehe za Nowruz

Siku kama ya leo miaka 2194 iliyopita, Bunge la kwanza la Iran lililokuwa likijulikana kwa jina la Mahestan liliasisiwa. Wajumbe wa Bunge hilo lililoasisiwa katika zama za Mehrdad wa Kwanza mfalme wa ukoo wa Ashkanian walikuwa ni wana wafalme na shakhsia wakubwa wa Iran. Miongoni mwa yaliyokuwa mamlaka ya Bunge la Mahestan ni kumchagua mfalme na kumuondoa madarakani endapo angekumbwa na maradhi mabaya, kuwa kichaa, kushindwa kufanya kazi au kuisaliti nchi. Aidha Bunge hilo lilikuwa na jukumu la kutangaza vita au kupendekeza amani na suluhu. 

Ramani ya Iran katika zama za utawala wa Mehrdad wa Kwanza mfalme wa ukoo wa Ashkanian

Siku kama ya leo miaka 254 iliyopita inayosadifiana na 21 Machi 1768, alizaliwa Joseph Baron Fourier mwanahisabati na mwanafizikia mashuhuri wa Ufaransa. Baron Fourier alikuwa miongoni mwa wahadhiri wa mwanzoni kabisa waliofundisha somo la hesabati mara baada ya kuanzishwa Chuo Kikuu cha Paris.

Baron Fourier

 

Katika siku kama ya leo miaka 53 iliyopita, kulitokea mapigano makubwa kati ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO na majeshi ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika mji wa Karama ulioko Jordan. Kwa uchache wanajeshi 1,230 wa Kizayuni waliangamizwa na makumi ya vifaru kutekelezwa au kuchukuliwa ngawira na wanamapambano wa Kipalestina kwenye mapigano hayo. Harakati ya PLO ilianza kupoteza hadhi yake ya kimapambano baada ya kulegeza misimamo yake ya kimapinduzi mwaka 1991 na kukubali kuketi kwenye meza ya mazungumzo ya amani na utawala ghasibu wa Israel; mazungumzo ambayo hayajawa na matunda yoyote kwa wananchi wa Palestina. 

Nembo ya PLO

 

Siku kama ya leo miaka 55 iliyopita Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) liliitangaza siku ya mauaji ya umati dhidi ya wazalendo weusi nchini Afrika Kusini yaliyotokea mwaka 1960 kuwa "Siku ya Kimataifa ya Kufuta Ubaguzi wa Rangi". Waafrika weusi wapatao 69 waliuawa na wengine 180 kujeruhiwa katika siku kama ya leo, baada ya askari makaburu kuwafyatulia risasi watu hao waliokuwa wakiandamana kwa amani huko Sharpeville nchini Afrika Kusini kupinga siasa za ubaguzi wa rangi. Japokuwa sera za ubaguzi wa rangi zimefutwa nchini Afrika Kusini lakini ubaguzi na ukosefu wa usawa vingali vinashuhudiwa kwa sura mbalimbali katika maeneo tofauti ya dunia na hivyo kunahisika haja ya kusimama na kukabiliana na miamala hii isiyo ya kibinadamu.*

 

Miaka 31 iliyopita nchi ya Namibia ilipata uhuru wake kutoka kwa Afrika Kusini. Mwishoni mwa karne ya 19, wakoloni wa Kijerumani, Uingereza na Ureno walianza kuvutana kwa minajili ya kudhibiti na kupora utajiri na maliasili za Namibia. Uhuru wa Namibia ulipatikana kutokana na mapambano ya harakati ya SWAPO chini ya uongozi wa Sam Nujoma. 

Bendera ya Namibia