Mar 28, 2021 05:23 UTC

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni katika sehemu nyingine mfululizo huu wa Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu ambao huwatambulisha na kuwazungumzia Maulamaa wakubwa wa Kishia, mchango wao katika Uislamu pamoja na vitabu na athari zao.

Kipindi chetu kilichopita kilimzungumzia Sheikh Jamal al-Din Hassan bin Yusuf Hilli mashuhuri kwa lakabu ya "Allama Hilli" fakihi na mwanateolojia wa Kishia aliyeishi katika karne ya Nane Hijria na ambaye ameandika zaidi ya vitabu 120 katika taaluma mbalimbali za elimu ya dini.  Tulisema kuwa,  mwanazuoni huyu mashuhuri alikuwa na mchango mkubwa katika kueneza madhehebu ya Kishia pamoja na maarifa na mafundisho ya Ahlul-Baiti (AS) na anaweza kutajwa kama ni mhuishaji wa athari za Kishia.

Kadhalika tuliashiria kwamba, Allama Hilli alifanya midahalo na mijadala mingi mno na Maulamaa wa Kisuni ambapo vitabu vyake vingi vinavyobainisha misingi ya Ushia na majibu yenye hoja na mantiki kwa wapinzani wa Ushia katika kipindi chote cha maisha yake ni ushahidi wa wazi wa jambo hili. Tulibainisha pia kuwa, Allama Hilli alizaliwa usiku wa tarehe 29 ya mwezi mtukufu wa Ramadhani 648 Hijria katika familia ya kielimu na iliyosifika kwa maadili mema na aliaga dunia mwezi Muharram mwaka 726 Hijria katika mji wa Hillah na amezikwa katika mji wa Najaf Iraq jirani na Haram ya Imam Ali bin Abi Twalib as. Sehemu ya 22 ya kipindi chetu juma hili, itamzungumzia alimu na msomi mwingine wa Kishia ambaye ni Muhammad bin Makki mwenye lakabu ya al-shahid a-Awwal mmoja wa wanazuoni mashuhuri wa Jabal Amil nchini Lebanon. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi.

Muhammad bin Makki mashuhuri kwa lakabu ya al-Shahid al-Awwal alizaliwa mwaka 734 Hijria katia eneo la Jabal Amil nchini Lebanon. Jabal Amil ni eneo lenye milima na mandhari nzuri nchini Lebanon ambalo licha ya kuwa na masafa na kilomita mrada ndogo, lakini liliondokea kuwa kitovu cha Maulamaa wengi wakubwa ambapo inanukuliwa kwamba, katika marasimu moja ya kidini zaidi ya Mamujitahidi sabini walikuwa wakihudhuria. Hii ni ishara na uthibitisho wa kuweko maulamaa wengi wa Kishia huko Jabal Amil katika zama zile.

Sheikh Abu Abdullah Muhammad Jamal ad-Deen al-Makki au Shahidi wa Kwanza kama anavyojulikana alizaliwa na kuondokea katika eneo kama hili na katika familia ambayo watu wake wote walikuwa wakijishughulisha na elimu. Alilelewa na kukulia katika mji huo hadi alipofikisha umri wa miaka 16. Alisoma masomo ya awali na ya msingi na ya hatua ya juu kidogo kwa baba yake na kwa Maulamaa wa wakati huo wa Jabal Amil na kisha baadaye akaeleke Hillah Iraq, lengo likiwa ni kwenda kujiendeleza zaidi kielimu.

 

Mwaka mmoja tu tangu alipowasili katika mji wa Hillah alifanikiwa kupata daraja ya Ijtihadi akiwa na umri wa miaka 17. Mwanazuoni huyo alibakia katika mji huo kwa muda wa miaka mitano. Elimu na uwezo mkubwa wa kielimu aliokuwa nao uliwafanya wanazuoni na wasomi wa zama hizo wastaajabishwe naye na kutaja wasifu wa elimu yake. Hata walimu wakubwa wa zama hizo katika mji wa Hillah kama Fakhrul-Muhaqiqin aliyekuwa mtoto wa Allama Hilli alimsifia mno Shahidi wa Kwanza ambapo licha ya kijana huyo kuwa na umri wa miaka 17 tu alikuwa akimuita na kumtaja kama Imam, Allama mkubwa na mwanazuoni bora wa ulimwengu.

Akiwa na umri wa miaka 21, alimu huyo alirejea katika kijiji alichozaliwa cha Jizzin huko Jabal Amil nchini Lebanon na baada ya muda mfupi akaanzisha chuo ambacho baadaye kilitoa wanafunzi mahiri waliohitimu hapo ambao baadaye waliondokea kuwa wasomi na wanazuoni wa kutegemewa. Mbali na kufundisha, al-Shahid al-Awwal alikuwa akijihusisha pia na kazi ya kuandika na kualifu vitabu ambavyo akthari yake vilikuwa ni majibu ya matatizo ya kimadhehebu, kiitikadi na kijamii ya wananchi. Alikuwa marejeo na kimbilio la Mashia na mbeba bendera ya sharia. 

Mwanazuoni huyu alikuwa na ufahamu mkubwa pia na vyanzo vya kidini vya madhehebu ya Kisuni kiasi kwamba, hata Masuni walikuwa wakimrejea na kumuuliza maswali kuhusiana na masuala mbalimbali ya kiibada yanayohusiana na madhehebu yao na yeye aliwakuwa akiwajibu na kuwapatia Fatuwa kwa mujibu wa madhehebu yao. Kutokana na kubobea kwake na kuwa na uwezo mkubwa kuhusiana na madhehebu ya Kisuni na kutoa Fatuwa kwa mujibu wa madhehebu ya Kisuni, baadhi ya watu walikuwa wakimtambua kama alimu na msomi ya madhehebu ya Shafi.

Al-Shahid al-Awwal alifanya safari katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kustafidi na tajiriba ya wanazuoni tofauti kama vile Damascus, Misri, Palestina, Makka na Madina. Katika zama hizo miji na maeneo hayo yalikuwa vituo vya elimu vyenye itibari katika Ulimwengu wa Kiislamu.

Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni Dhikra al-Shia fi Ahkaam al-Sharia. Kitabu hiki kinachohusiana na masuala ya tohara, kilichapishwa mwaka 1271. Kitabu kingine cha mwanazuoni huyu ni al-Duruus al-Shariah fi fiqh al-Imamiyah ambacho ndani yake kimebainisha masuala mengi ya kifikihi. Hata hivyo Shahidi wa Kwanza alikufa shahidi kabla ya kukamilisha kitabu hiki.

Aidha alimu huyo ana vitabu vingine alivyoandika katika maudhui za Hija, Swaumu, Swala na vilevile katika uga wa itikadi, Usuul na kadhalika ambapo uthibitisho wa umuhimu wa vitabu hivyo, ni hatua ya maulamaa waliokuja baada yake ya kuvisherehesha vitabu hivyo. Aidha ana kitabu au risala ambayo ni maswali na majibu.

Hata hivyo, kitabu chake mashuhuri zadi ni Lum’a Dimishqiah ambacho kimeeleza kwa mapana na marefu hukumu za ibada na amali (za kivitendo) katika Uislamu.

Mbali na Shahidi wa Kwanza kuwa mwanazuoni ambaye hakuwa na mithili katika zama zake alikuwa na nafasi athirifu pia katika kuongoza jamii ya Waislamu na kulinda mipaka ya itikadi ya Ushia.

Katu hakuwa akinyamazia bidaa, uzushi na upotovu katika dini na alifanya juhudi kutetea hadhi na heshima ya dini na madhehebu kwa nguvu zake zote. Wakati fulani mwanazuoni huyu alifungwa jela mwaka mmoja huko Damasvus baada ya kusingiziwa kwa chuki na uadui kwamba, itikadi zake ni potofu. Hatimaye alimu huyu aliuawa shahidi kwa kwa kukatwa shingo baada ya kutolewa hukumu dhidi yake katika tuhuma ambazo katu hakuhusika nazo. Alikufa shahidi mwaka 786 akiwa na umri wa miaka 52.

Wapenzi wasikilizaji muda wetu uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki kwa leo umefikia tamati, hivyo sina budi kukuageni nikikutakieni kila la kheri maishani. Tukutane tena juma lijalo katika sehemu nyingine ya mfululizo huu.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.