Jumatano tarehe 31 Machi mwaka 2021
Leo ni Jumatano tarehe 17 Shaabani 1442 Hijria sawa na tarehe 31 Machi mwaka 2021.
Miaka 425 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 31 Machi mwaka 1596, alizaliwa Rene Descartes mwanafalsafa, mwanahisabati na mwanafizikia wa Kifaransa. Descartes alifikia daraja ya uhadhiri wa chuo kikuu baada ya kuhitimu masomo ya falsafa na hisabati. Msomi huyo wa Kifaransa alifanya safari kwa kipindi fulani katika nchi mbalimbali na baadaye aliishi Uholanzi na kuanza kufanya utafiti. Rene Descartes aliitambua hisabati kuwa ni elimu kamili miongoni mwa elimu nyinginezo na kutaka kutumiwa elimu hiyo katika taaluma nyinginezo. Miongoni mwa vitabu vya mwanafalsafa huyo ni Principles Of Philosophy, The Passions of the Soul na Discourse on the Method.
Katika siku kama ya leo miaka 81 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, aliaga dunia Sheikh Hassanali Isfahani, arif, msomi na mwanazuoni aliyekuwa amebobea katika taaluma ya fiqhi. Alizaliwa mwaka 1279 Hijria huko Isfahan katikati mwa Iran na akaanza mapema mno kusoma elimu mbalimbali kama fiqhi, usul, mantiki na falsafa. Ayatullah Isfahani akiwa na lengo la kujiendeleza zaidi kielimu, alielekea Najaf nchini Iraq na baadaye Mash’had, Iran na kubakia huko hadi mwisho wa umri wake. Ayatullah Isfahani alibobea pia katika elimu za hisabati, nujumu na tiba. Hata hivyo alikuwa mashuhuri zaidi katika baadhi ya elimu kama irfan na akhlaq.
Umashuhuri mkubwa zaidi wa msomi huyo unatokana na uchamungu wake mkubwa na karama zake ambazo ni matokeo ya kujipinda katika ibada, kuitakasa nafsi na uchamungu mkubwa. Baadhi ya karama za Ayatullah Isfahani zimenukuliwa mwanaye katika kitabu alichokipa jina la "Alama za Wasio na Alama".
Siku kama ya leo miaka 73 iliyopita, garimoshi lililokuwa likitoka Cairo, Misri likielekea katika bandari ya Haifa huko Palestina lililipuriwa kwa bomu, ikiwa ni katika mwendelezo wa mauaji ya umati yaliyokuwa yakifanywa na Wazayuni maghasibu dhidi ya Wapalestina. Wapalestina 40 waliuawa na wengine 60 kujeruhiwa katika jinai hiyo iliyofanywa na kundi moja la Kizayuni. Siku nne kabla ya mlipuko huo, garimoshi jingine lililipuliwa huko Palestina na Wazayuni waliokuwa na silaha na kuuwa Wapalestina 24. Wapalestina wengine 61 walijeruhiwa.
Na siku kama ya leo miaka 42 iliyopita, nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu zilisimamisha uanachama wa Misri katika jumuiya hiyo na nchi nyingi wanachama zikakata uhusiano wao na Cairo. Nchi za Kiarabu zilichukua msimamo huo mkali baada ya rais wa zamani wa Misri, Anwar Sadat, kusaini hati ya mapatano ya Camp David na utawala wa Kizayuni wa Israel mwezi Januari mwaka 1978.