Apr 19, 2021 02:26 UTC
  • Jumatatu tarehe 19 Aprili mwaka 2021

Leo ni jumatatu tarehe 6 Ramadhhani 1442 Hijria sawa na Aprili 19 mwaka 2021.

Miaka 2054 iliyopita kwa mujibu wa baadhi ya nadharia za wanahistoria, yaani tarehe 19 Aprili mwaka 33 kabla ya kuzaliwa Nabii Issa (as), kulianzishwa maktaba ya kwanza ya umma duniani 'Public Library' huko Roma ambayo kila mwenye elimu alikuwa na haki ya kuingia humo na kusoma vitabu alivyotaka. Kabla ya Waroma, Wasumeri, Waashuri, Wababeli na Wairani walikuwa na maktaba zao ingawa maktaba hizo hazikuwa zikitumika na watu wote, huku maktaba ya Waashuri ikiwa ndio maarufu zaidi. Ni vyema kuashiria hapa kuwa, nchi ya kwanza ambayo ilianzisha asasi za uandishi na tarjama za vitabu duniani, ilikuwa ni Iran, ambapo karne 15 zilizopita zilikuwa zikifanya kazi hizo katika utawala wa Khosrow Anushirvan.

Maktaba ya umma 

Siku kama ya leo miaka 129 iliyopita yaani 19 Aprili mwaka 1882, alifariki dunia mtaalamu wa elimuviumbe wa Uingereza Charles Darwin. Alizaliwa Februari 12 1809 nchini Uingereza. Msomi huyo alifanya utafiti kuhusu manma ya kudhihiri viumbe mbalimbali na alifanya safari ya muda mrefu duniani kwa ajili ya kukamilisha uchunguzi wake wa kielimu na baada tu ya kurejea aliandika kitabu maarufu cha "On the Origin of Species". Kwa mujibu wa nadharia ya Darwin ambaye ndiye aliyeanzisha mfumo wa Darwinism, chanzo cha viumbe vya leo ni viumbe vidogovidogo ambavyo vilibadilika kutokana na mazingira tofauti kwa miaka mingi na kufikia hali ya sasa. Fikra za Darwin zinapingana na mafundisho ya dini za mbinguni kuhusu namna ya kuumbwa mwanadamu lakini zimetumiwa kama msingi wa mifumo ya kiilhadi (isiyoamini uwepo wa Mwenyezi Mungu) kama ule wa Umaxi. Aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 73 na alizikwa pembizoni mwa Isaac Newton katika kanisa la Westminster Abbey mjini London.

Charles Darwin

Siku kama ya leo miaka 26 iliyopita yaani tarehe 19 Aprili 1995, kulitokea mlipuko mkubwa ulisababisha mauaji katika mji wa Oklahoma City nchini Marekani. Katika siku hiyo Timothy McVeigh alilipua bomu mbele ya jengo la Federali la mji wa Oklahoma City ambalo liliua watu 168. Mauaji hayo yalitambuliwa kuwa tukio kubwa zaidi la kigaidi katika historia ya Marekani kabla ya kutokea mashambulizi ya Septemba 11 mwaka 2001. McVeigh alisema kuwa sababu ya kuchukua hatua hiyo ni upinzani wake dhidi ya serikali ya federali ya Marekani na kulipiza kisasi tukio la kuchomwa moto makao ya kundi la Davidian katika mji wa Waco mwaka 1993 lililopelekea kuuawa wafuasi 76 wa kundi hilo. Hujuma  hiyo dhidi ya jengo la Federali ni tukio ambalo liliwaingiza woga na wahka Wamarekani na kubaini kuwa jamii ya nchi hiyo inakabiliwa na tishio kubwa la ugaidi wa ndani ya nchi.

Oklahoma City

Na siku kama ya leo miaka 16 iliyopita, Kadinali Joseph Ratzinger alikabidhiwa uongozi wa Kanisa Katoliki Duniani baada ya kufariki dunia Papa John Paul wa Pili na kuchagua jina la Papa Benedict wa 16. Ratzinger alizaliwa mwaka 1927 nchini Ujerumani na alipanda daraja na kuwa askofu mwaka 1977 na hatimaye kufikia daraja ya ukadinali. Papa Benedict wa 16 alikabiliwa na matatizo mbalimbali akiwa kiongozi wa kanisa hilo ikiwa ni pamoja na mgogoro wa masuala ya kiroho katika nchi za Magharibi, ufisadi na utovu wa maadili pamoja na vitendo vya ubakaji na ulawiti vinavyofanywa na maaskofu na makasisi dhidi ya watoto wadogo. Papa Benedict wa 16 alilazimika kuachia uongozi wa Kanisa Katoliki Februari mwaka 2013 baada ya kuzongwa na kashfa nyingi za viongozi wa ngazi za juu ndani ya kanisa hilo.

Kadinali Joseph Ratzinger

 

Tags