Ansarullah ya Yemen: Iran inahami mustakbali wake na Umma wa Kiislamu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i137480-ansarullah_ya_yemen_iran_inahami_mustakbali_wake_na_umma_wa_kiislamu
Msemaji wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema kuwa yoyote atakayepuuza haki ya Iran ya kujihami atakuwa amemhudumia adui.
(last modified 2026-03-20T08:10:16+00:00 )
Mar 20, 2026 08:10 UTC
  • Mohammad Abdulsalam
    Mohammad Abdulsalam

Msemaji wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema kuwa yoyote atakayepuuza haki ya Iran ya kujihami atakuwa amemhudumia adui.

Mohammad Abdulsalam mkuu wa timu ya mazungumzo ya Serikali ya Sana'a ambaye pia ni msemaji wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen, ametilia mkazo wajibu wa kidini wa Waislamu na kuwataka kushikamana na kudhihirisha msimamo wa pamoja dhidi ya mashambulizi ya utawala wa Kizayuni Israel na Marekani na kwamba kitisho hiki kimezilenga nchi zote za Kiislamu.

Abdulsalam pia ameashiria matukio ya karibuni na kusema, msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni wa kiulinzi na kwamba Tehran inajihami dhidi ya mashambulizi na hatua za kiuhasama dhidi yake na dhidi ya Umma wa Kiislamu. 

Abdulsalam amebainisha kuwa oparesheni ya kuwauwa kigaidi makamanda wakiwemo viongozi wa ngazi ya juu imepelekea Iran kuchukua hatua za kujibu na kuongeza kuwa: Jibu lililotolewa na Jamhuri ya Kiislamu dhidi ya vituo na maeneo yanayotumiwa kufanyia mashambulizi dhidi yake ni matokeo ya moja kwa moja ya vitendo vya pande vamizi.

Msemaji wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen pia amesema: Matamshi yoyote yanayopuuza haki ya Iran ya kujilinda yanamhudumia adui, na yana lengo la kuibua fitna haribifu kati ya watoto wa Umma wa Kiislamu. 

Kiongozi huyo wa Yemen mwishoni mwa hotuba yake amesisitiza udharura wa kulindwa maslahi ya Umma wa Kiislamu na kukomeshwa mashambulizi dhidi ya Iran na Lebanon. Vilevile ametoa wito wa kukomeshwa vitendo vya kutumiwa kambi za kijeshi katika eneo la Magharibi mwa Asia kwa ajili ya kufanyia hujuma za mashambulizi dhidi ya nchi za eneo hilo.