Iran yamjibu waziri wa mambo ya nje wa Saudia
-
Esmaeil Baghaei
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza umuhimu wa hatua za haraka kutoka kwa nchi za eneo la Asia Magharibi ili kuzuia kuendelea kwa matumizi ya ardhi na miundombinu yao na Marekani pamoja na utawala wa Kizayuni katika mashambulizi dhidi ya Iran.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la IRIB, Esmaeil Baghaei alielezea kauli za Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Faisal bin Farhan, zilizotolewa katika mkutano wa nchi za Kiarabu na Kiislamu kuwa hazina usawa, ni za upande mmoja, na zinakinzana na wajibu wa kuchukua msimamo wa kuwajibika kuhusu masuala ya eneo hili.
Msemaji huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje amesema hakuna upande wowote unaoweza kupuuza ukweli ulio wazi kwamba chanzo kikuu cha mgogoro katika eneo hili ni vita vilivyolazimishwa na Marekani pamoja na utawala wa Kizayuni. Ameongeza kuwa pande hizo mbili zinatumia kambi na miundombinu ya kijeshi iliyoko katika baadhi ya nchi za eneo hili kupanga, kutekeleza na kuunga mkono mashambulizi yao dhidi ya Iran.
Bwana Baghaei pia amesisitiza haki ya kiasili ya Iran ya kujilinda dhidi ya mashambulizi ya Marekani na utawala wa Kizayuni. Amebainisha kwamba kwa mujibu wa kanuni za Mkataba wa Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa, ikiwemo maazimio 2625 na 3334 ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, hakuna nchi inayoruhusiwa kuruhusu ardhi au rasilimali zake zitumike na upande wa tatu kufanya mashambulizi dhidi ya nchi nyingine.