May 31, 2021 02:26 UTC
  • Jumatatu, Mei 31, 2021

Leo ni Jumatatu tarehe 19 Mfunguo Mosi Shawwal 1442 Hijria sawa na Mei 31 mwaka 2021 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1492 iliyopita, sawa na tarehe 31 Mei 529, dini ya Ukristo ilitambuliwa rasmi huko Roma kwa amri ya Constantine, mfalme wa wakati huo wa Roma. Kabla ya hapo Wakristo walikuwa wakifanya ibada kwa siri huko Roma. Mwaka 324 Miladia Mfalme Constantine aliamua kuhamia Byzantine, mji ambao alikuwa ameutangaza kama mji mkuu wa ufalme wake ambao uliojengwa na Wagiriki yapata karne nane kabla ya kuzaliwa Nabii Isa (as). Miaka sita baadaye na baada ya kuhamia huko mfalme huyo, dini ya Ukristo ikatangazwa na kutambuliwa rasmi na wafuasi wake wakaruhusiwa kuabudu kwa uhuru. 

Siku kama ya leo mmiaka 1008 yaani tarehe 19 Shawwal 434 iliyopita alizaliwa Abu Zakaria Yahya bin Muhammad mashuhuri kwa jina la Ibn Mandeh ambaye alikuwa mwanahadithi, faqihi na mwanahistoria wa Kiirani. Alikuwa wa mwisho katika kizazi cha Ibn Mandeh na baada ya kupata elimu za zama zake alianza kufunza na kuandika vitabu. Mwanahistoria huyo wa Kiislamu ameandika vitabu vingi kikiwemo kile cha Maisha ya Tabarani.

Siku kama ya leo miaka 189 iliyopita alifariki dunia Évariste Galois, mwanahisabati aliyekuwa na kipawa cha juu wa Ufaransa. Alizaliwa tarehe 26 Oktoba mwaka 1811 karibu na mji wa Ufaransa. Hadi anafikia umri wa miaka 12 hakuwa na mwalimu mwingine ghairi ya mama yake na kutokana na kipawa cha hali ya juu cha elimu alianza kusoma vitabu mbalimbali vya historia  na hivyo kuinukia kielimu. Baada ya hapo alijiunga na chuo, ambapo alikuwa akishika nafasi ya kwanza darasani katika kila somo. Baadaye Évariste Galois alianza kutalii elimu ya hisabati. Akiwa na umri wa miaka 18 alikamilisha kazi ya uandishi wa kitabu cha Ukweli wa Hisabati na baada ya hapo akaandika vitabu vitatu vipya katika taaluma hiyo na kujipatia umashuhuri mkubwa. Galois aliuawa akiwa na umri wa miaka 21 sawa na tarehe kama ya leo mwaka 1832 Miladia, baada ya kutiwa jela wakati wa harakati zake za kisiasa nchini Ufaransa. Weledi wanaamini kuwa, kama Galois hangeuawa mapema, basi angepiga hatua kubwa katika uga wa hisabati duniani.

Évariste Galois

Katika siku kama ya leo miaka 111 iliyopita, yaani tarehe 31 Mei mwaka 1910, nchi ya Afrika Kusini iliundwa katika eneo la kusini mwa Afrika kwa kuunganishwa makoloni mawili ya Uingereza na kupewa uhuru. Muungano huo ulipata uhuru kamili mwaka 1931. Hata hivyo hatamu za madaraka ya nchi zilikuwa mikononi mwa wazungu wachache. Mwaka 1991 wazungu makaburu walilazimika kuhitimisha mfumo wa ubaguzi wa rangi wa Apartheid katika nchi hiyo baada ya mapambano ya miaka mingi ya Waafrika Kusini wazalendo wakiongozwa na shujaa Nelson Mandel.

Bendera ya Afrika Kusini

Miaka 26 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Sheikh Muhammad Ghazali mwanazuoni na mwanamageuzi mkubwa wa Misri. Alizaliwa mwaka 1917 huko nchini Misri. Akiwa na umri wa miaka 10 tu, tayari Muhammad Ghazali alikuwa amehifadhi Qur'ani Tukufu yote. Muhammad Ghazali alihitimu Chuo Kikuu akiwa na umri wa miaka 24. Fikra zake zilijengeka juu ya msingi wa mageuzi ya maarifa ya kidini, kukurubisha baina ya madhehebu za Kiislamu na kupinga fikra za kikaumu. Muhammad Ghazali aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 79 kwa mshtuko wa moyo na kuuzikwa katika makaburi ya Baqii mjini Madina. 

Sheikh Muhammad Ghazali

Siku kama ya leo miaka 11 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 31 Mei 2010, wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel walishambulia msafara wa meli zilizosheheni misaada ya kibinadamu kwa ajili ya wananchi wa Ukanda wa Ghaza waliozingirwa na utawala huo. Shambulio hilo lilipelekea watu 9 kuuawa na wengine zaidi ya 50 kujeruhiwa. Msafara huo uliokuwa na wanaharakati 663 kutoka nchi 37 duniani, ulikuwa umebeba shehena ya misaada ya  dawa na chakula kwa ajili ya wananchi wa Ukanda wa Ghaza wanaokabiliwa na mzingiro wa kidhulma wa Wazayuni. Shambulio hilo la kinyama lililaaniwa vikali na mataifa mbalimbali duniani, na hatimaye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likatoa azimio la kufanyika uchunguzi wa haraka na usiopendelea upande wowote kwa lengo la kubaini na kuwekwa wazi wahusika wa jinai hizo.