Jun 04, 2021 02:51 UTC
  • Ijumaa tarehe 4 Juni 2021

Leo ni Ijumaa tarehe 23 Mfunguo Mosi Shawwal 1442 Hijria sawa na tarehe 4 Juni mwaka 2021.

Siku kama ya leo miaka 32 iliyopita, sawa na tarehe 14 Khordad mwaka 1368 kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia sawa na mwezi Juni 1989, Imam Ruhullah Musawi Khomeini (M.A) Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliaga dunia baada ya kuishi kwa miaka 87 katika umri uliojaa juhudi zisizo na kikomo. Kwa kutangazwa kifo cha Imam ulimwengu wa Kiislamu uligubikwa na majonzi na huzuni kubwa. Imam Khomeini (M.A) alizaliwa tarehe Mosi mwezi wa Mehr mwaka 1281 Hijiria Shamsia sawa na tarehe 24 Septemba 1902 Milaadia katika mji wa Khomein ulioko katikati mwa Iran. Alianza kujishughulisha na siasa sambamba na masuala ya kielimu na kiutamaduni. Mapambano ya Imam dhidi ya utawala wa Shah na uingiliaji wa Marekani nchini Iran yalishtadi mwaka 1963 Milaadia sawa na 1342 kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia, na kupelekea Imam kubaidishwa kwa miaka 13 nchini Iraq, Uturuki na Ufaransa. Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalipata ushindi mwaka 1357 Hijiria Shamsia sawa na tarehe 1979 Milaadia kwa uongozi shupavu wa Imam Khomeini (M.A). Aidha Imam alibobea katika elimu ya dini na mbali na kuwasomesha wanafunzi wengi na kutoa hotuba nyingi za kihistoria, aliandika pia vitabu. Miongoni mwa vitabu vyake tunavyoweza kuashiria hapa ni Tahrirul Wasilah, Kashful Asrar, Misbahul Hidayah, na Utawala wa Kiislamu na Uongozi wa Faqih. Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran inatoa salamu za rambi rambi kwa mnasaba huu wa kukumbuka wakati Imam Khomeini aliporejea kwa Mola wake.

Siku kama ya leo miaka 32 iliyopita inayosadifiana na tarehe 4 Khordad mwaka 1368 kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, Baraza la Wanazuoni Wataalamu wanaomchagua Kiongozi Muadhamu lilimchagua Ayatullah Sayyid Ali Khamenei kuwa Kiongozi Muadhamu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Uchaguzi huo ulifanyika masaa machache tu baada ya kufariki dunia Imam Khomeini (M.A) ambapo wasia wa Imam ulisomwa mbele ya hadhirina. Hadi sasa Ayatullah Khamenei anaendeleza njia ya Imam Khomeini MA kwa msingi wa mafundisho ya Kiislamu na ameyaongoza Mapinduzi ya Kiislamu kwa hekima, tadbiri, uono wa mbali na ustahiki.

Siku kama ya leo miaka 32 iliyopita, sawa na tarehe 4 Juni mwaka 1989, wanafunzi kadhaa wa vyuo vikuu vya China waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa na polisi katika mji mkuu wa nchi hiyo Beijing. Siku hiyo maelefu ya wanafunzi wa vyuo vikuu vya China walikuwa wamekusanyika katika mzunguko wa Tiananmen mjini Beijing, wenye maana ya 'Amani ya Mbinguni' wakitaka kuwepo mazingira ya wazi ya kisiasa nchini humo, kupungua uwezo wa chama cha kisoshalisti, kuongezwa uwezo wa bunge na kuchaguliwa wawakilishi wake. Ingawa serikali ya China ilipiga marufuku maandamano hayo lakini wanafunzi waliendela kukusanyika na mwishowe askari polisi na vikosi vya jeshi vikatumia silaha kuwakandamiza wanafunzi hao.

Medani ya Tiananmen 

Leo ni Siku ya Kimataifa ya Watoto Wasio na Hatia Waathirika wa Unyanyasaji (International Day of Innocent Children Victims of Aggression). Siku hiyo ilitangazwa na Umoja wa Mataifa mwaka 1982 kwa ajili ya kushughulikia mashaka ya watoto wanaosumbuliwa na unyanyasaji wa kimwili, kiakili na kiroho kufuatia hali mbaya ya watoto wa Palestina na Lebanon wanaosumbuliwa na ukatili wa utawala haramu wa Israel. Ukatili na unyanyasaji dhidi ya watoto una sura na aina mbalimbali na unasababishwa na uzembe wa wazazi, viongozi wa kitaifa na kimataifa na makatili wasio na chembe ya huruma na wasiojali isipokuwa maslahi yao ya kimaada.

Siku ya Kimataifa ya Watoto Wasio na Hatia Waathirika wa Unyanyasaji

Na katika siku kama ya leo miaka 330 iliyopita alifariki dunia Sayyid Neematulllah Jazairi aliyekuwa faqihi na mpokezi mkubwa wa hadithi wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 62. Alikuwa hodari katika elimu za fiqhi, hadithi, tafsiri ya Qur'ani na fasihi ya lugha ya Kiarabu na alistahamili mashaka mengi katika njia ya kulingania sheria za dini ya Kiislamu. Sayyid Neematullah Jazairi ameandika vitabu kadhaa vya thamani kama Madinatul Hadith, Qiswasul Anbiyaa na Hidayatul Muuminin.

Sayyid Neematulllah Jazair