Jul 18, 2021 05:42 UTC

Karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu ambacho huwatambulisha na kuwazungumzia Maulamaa wakubwa wa Kishia, mchango wao katika Uislamu pamoja na vitabu na athari zao.

 

Vipindi vyetu viwili vilivyotangulia vilitupia jicho kwa mukhtasari historia na maisha ya msomi mwingine wa Kishia ambaye si mwingine bali ni Ali bin Hassan Karaki mashuhuri zaidi kwa lakabu ya Muhaqqiq Thani au Muhaqqiq Karaki. Tulibainisha pia kuwa, baada ya Khaje Nassirddin Tusi, Muhaqqiq Karaki anahesabiwa kuwa mtu aliyefanya juhudi kubwa mno kwa ajili ya kuinua jina la madhehebu ya Shia na maktaba ya Ahlul-Baiti (as) nchini Iran. Sehemu ya 26 ya mfululizo huu juma hili, itamzungumzia alimu na  msomi mwingine mashuhuri katika ulimwengu wa Kishia ambaye naye ni kutoka huko Jabal Amil nchini Lebanon. Huyu ni Zeinuddin bin Ali bin Ahmad Amili Juba’i ambaye anajulikana pia kwa lakabu ya Shahidi Thani. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

 

Shahidi wa Pili, fakihi na mwanazuoni mkubwa wa Kishia na ulimwengu wa Kiislamu alizaliwa 13 Mfunguo Mosi Shawwal 911 Hijria katika familia ya kielimu na ya kifikihi. Akthari ya mababu na familia ya Shahidi Thani walikuwa katika orodha ya wanazuoni na wasomi wakubwa. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana ukoo wa Shahidi Thani ukaondokea kuwa mashuhuri kwa lakabu ya Silsilat al-Dhahab yaani mlolongo wa dhahabu. Sheikh Hassan, mtoto wa Shahidi Thani ni mmoja wa wanazuoni na wasomi wakubwa na ndiye aliyeandika kitabu mashuhuri cha Ma'alim al-Usul katika uga wa elimu ya Fikihi, kitabu ambacho katika zama hizi kinahesabiwa kuwa moja ya vitabu vya kufuindishia katika vyuo vikuu mbalimbali vya Kiislamu (Hawza). Ni kwa msingi huo ndio maana akatambulishwa pia kwa jina la Swahib Maalim. Mjukuu wa binti ya Shahidi Thani ambaye anajulikana kwa jina la Sayyid Muhammad Musawi Amili naye ni fakihi mwanazuoni mashuhuri wa elimu ya fikihi. Yeye amendika kitabu muhimu cha Madarik Al-Ahkam ambacho ni moja ya vitabu vyenye itibari kubwa katika masuala ya fikihi. Aidha yeye pia anatambulika kwa lakabu ya Swahib Madarik. Kadhalika familia na ukoo wa Sadr kama Imam Mussa Sdr, Shahidi Sayyid Muhhammad Baqir Sadr na dada yake shahidi Bintul al-Huda wanatokana na kizazi cha Shahidi Thani.

 

Zeinuddin bin Ali bin Ahmad Amili Juba’i ambaye anajulikana pia kwa lakabu ya Shahidi Thani yaani Shahidi wa Pili, kama alivyokuwa Shahidi wa Kwanza, yeye pia asili yake ni Jabal Amil eneo ambalo kijiografia linapatikana kusini mwa Lebanon. Wawili hao wanatambulika kama wanazuoni waliokuwa na kipaji kikubwa na ni katika fakhari za mafakihi na mamujitahidi wa Kishia na wote wawili waliuawa shahidi katika njia ya dini kwa kosa la kuwa Mashia.

 

Shahidi Thani ambaye aliishi katika karne ya 10 alifanya hima na idili isiyo ya kifani sambamba na jitihada zisizochoka na kufanikiwa kueneza fikihii ya Aal Muhammad (saw) katika pembe mbalimbali za dunia. Kuna athari zipatazo 80 za vitabu na makala za mwanazuoni huyu ambapo kila moja ya athari hiyo ni mlango kwa wanafakihi baada yake. Kitabu chake mashuhuri cha al-Rawdhat al-Bahiyyah ni johari muhimu sana ya kielimu ambayo hadi leo wasomi na watafuta elimuu wamekuwa wakifaidika nayo. Kitabu hiki kiliandikwa ili kutoa ufafanuzi wa kitabu cha al-Lum'a al-Dimishqiyah cha Shahidii wa Kwanza. Kitabu kingine muhimu na mashuhuri cha Shahidi Thani ni Masalik al-Afham ambacho ni ufafanuzni wa kitabu cha Sharai'i cha Muhaqqiq Hilli.

Shahidi Thani kama walivyokuwa aktharii ya Mmaulamaa na wasomi wakubwa wa Ulimwengu wa Kiislamu, yeye pia alianza kusoma akiwa angali kijana mdogo ambapo alianza kwa kujifunza Qur'ani. Mwalimu wake wa kwanza alikuwa baba yake. Baada ya hapo akaanza kusoma kwa shakhsia na wasomi wakubwa katika zama hizo. Baada ya kufanikiwa kukamilisha elimu na masomo yaliyokuwa mashuhuri katika zama hizo katika eneo lake la asili yaani Jabal Amil alifanya safari katika miji na maeneo mengine ya viunga vya eneo hilo.

Eneo la Jabal Amil lilikuwa bahari ya kulelea wasomi na wanazuoni ambalo lilikuwa na vyuo vizuri vya kielimu ambapo wanazuoni wakubwa walikuwa wakifundisha katika vyuo hivyo.

Kiu na shauku ya kutaka kujifunza na kupata ukamilifu katika elimu aliykuwa nayo Shahidi Thani, vilimfanya na kumsukuma afanye safari za mbali sio kwa ajili ya biashara au utalii bali kwa ajili ya kutoa huduma kwa Uislamu wa kweli na maktaba ya Ahlul Baiti (as).

 

Katika hali ambayo mazingira ya kisiasa na kijami katika zama hizo na utawala wa Othnmania katika ulimwengu wa Kiarabu hayakuwa mazuri kwa Mashia hususan wanazuoni na Maulamaa wa zama hizo wa Kishia na hata maziigira yalikuwa yametawaliwa na hofu na wasiwasi, lakini kutokana na mapenzi makubwa kwa Ahlul-Baiti aliyokuwa nayo Shahidii Thani alifanikiwa kuleta azma na irada thabiti ya kushinda mambo magumu miongoni mwa wapenzi na wafuasi wa Ahlu-Baiti. Shahidi Thani alifanya safari Damascus na baadaye Misri na kusoma elimu mbalimbali kama jiometri, fikihi, mantiki, tafsiri ya Qur'ani na kadhalika kwa walimu mahiri wa zama hizo.

Katika mwendelezo wa safari zake, Shahidi Thani alielekea Baytul-Muqaddas na Roma ya Mashariki ambapo baada ya kukutana na kufahamiana na maulama wakubwa wa maeneo hayo na kufanya nao mazungumzo ya kielimu, alijishulisha pia na kufundisha katika shule za miji hiyo.

Kipindi fulani mwanazuoni huyo alibakia katika mji wa Baalbek moja ya miji muhimu na ya kihistroria ya Lebanon na kuchukua jukumu la kiongozi wa chuo cha kielimu cha mji huo. Katika zama hizo Shahidi Thani alipata umashuhuri mkubwa ambapo wanazuoni na wasomi wa kutoka maeneo mbalimbali ya dunia wakaanza kumiminika na kwenda kwa alimu huyo kwa ajili ya kunufaika na bahari yake ya elimu aliyokuwa nayo. Miongoni mwao walikuwemo pia hata wanazuoni wa madhehebu mbalimbali.

Nyumba na Msikiti wa Shahidi thani nchini Lebanon

 

Shahidi Thani alikuwa na ufahamu mkubwa wa kielimu katika madhehebu matano ya Jaafariya, Hanafi, Shafii, Maliki na Hanbali. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana akiwa Baalabek Shahidi Thani alikuwa akifundisha madhehebu zote tano elimu mbalimbali na itikadi zinazohusiana na madhehebu hizo. Kama ambavyo alikuwa akitoa majibu ya maswali na hata fatuwa kwa wafuasi wa madhehebu mbalimbali kwa mujibu wa vyanzo, itikadi na vitabu vyao.

Kwa upande wa upole, uchajii Mungu, maadili mema, tabia njema na sifa nyingine nzuri za ukamilifu wa mwanadamu, Shahidi Thani alikuwa amekamilika katika uga huo na aliondokea kufahamika baina ya watu kama mtu mwema na mwenye tabia na aali na kamilifu.

Shahidi Thani aliuawa kwa tuhuma kwamba, ni Mshia na kafiri. Makachero wa utawala wa Othamania wakati huo walimtia mbaroni akielekea katika ibada ya Hija na kumuua shahidi kwa kutenganisha kichwa chake. Mwili wake mtoharifu ulibakia pasina kuzikwa kwa muda wa siku tatu. Baadhi ya wanahistoria wanasema, watu waliupata mwili wake usio na kichwa na kumzika pasina ya kumjua ni nani. Mtawala wa wakati huo alikasirishwa na kitendo cha makachero wake kutekeleza mauaji hayo bila ya idhini yake na ni kutokana na hasira alizokuwa nazo mtawala huyo ndio maana akatoa amri ya kuuawa yule aliyemuua Shahidi Thani. Tukio hilo lilijiri mwaka 966 Hijria.

Wapenzi wasikilizaji kwa leo nakomea hapa, nikitaraji kuwa mtakuwa pamoja nami juma lijalo. Siku na wakati kama wa leo.

Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabakaatuh

Tags