Sep 27, 2021 02:20 UTC
  • Jumatatu, Septemba 27, 2021

Leo ni Jumatatu tarehe 20 Mfunguo Tano Safar 1443 Hijria sawa na tarehe 27 Septemba 2021 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1382 iliyopita, ilifanyika majlisi ya kwanza ya siku ya Arubaini tangu kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) Imam Hussein bin Ali (as) na watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume ambao waliuawa shahidi tarehe 10 Muharram mwaka 61 Hijria. Majlisi ya siku ya Arubaini hufanyika kila mwaka baada ya kupita siku Arubaini tangu tarehe 10 mwezi wa Muharram kwa ajili ya kukumbuka mauaji ya mjukuu wa Mtume na masahaba zake watiifu ambao walijisabilia roho zao kwa ajili ya kuhuisha dini ya Mwenyezi Mungu katika ardhi ya Karbala.

Siku kama ya leo miaka 72 iliyopita, mji wenye jamii kubwa ya watu wa Beijing ulichaguliwa rasmi kuwa mji mkuu wa Uchina. Mji wa kihistoria wa Beijing unapatikana mashariki mwa nchi hiyo na unahesabiwa kuwa moja ya vituo vikubwa vya kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni nchini China. Beijing ilichaguliwa kuwa mji mkuu wa China baada ya Mao Tse-tung kuchukua madaraka ya nchi na kiongozi wa wakati huo wa China Chiang Kai-shek kulazimika kukimbilia Taiwan.

Siku kama leo miaka 24 iliyopita, kundi la Taliban lilivamia na kutwaa mji mkuu wa Afghanistan, Kabul. Kundi la Taleban liliasisiwa mnamo mwaka 1994 na likateka hatua kwa hatua maeneo ya kusini na magharibi mwa Afghanistan kwa himaya ya Marekani, misaada ya kisiasa na kijeshi ya Pakistan pamoja na misaada ya kifedha ya Saudi Arabia. Jeshi la serikali ya Afghanistan lililokuwa likiongozwa na Ahmad Shah Mas'ud liliondoka mjini Kabul siku moja kabla ya Taliban kuuteka mji huo. Baada ya kuingia Kabul, kundi la Taliban lilianza kutekeleza sheria kali na zinazoshabihiana na zile za karne za kati dhidi ya wananchi. 

Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita wapiganaji shujaa wa Iran walifanikiwa kuvunja mzingiro wa mji wa Abadan katika operesheni ya haraka na iliyokuwa imeratibiwa vyema dhidi ya ngome za jeshi la Saddam Hussein wa Iraq. Operesheni hiyo ilitekelezwa na wapiganaji wa Iran kufuatia agizo la kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Imam Khomeini, Mwenyezi Mungu Amrehemu. Mji wa Abadan ulikuwa umezingirwa na wanajeshi wa Iraq kwa karibu mwaka mmoja tangu kuanza vita vya kulazimishwa vya utawala wa dikteta Saddam dhidi ya Iran.

Tarehe 27 Septemba inasadifiana na Siku ya Kimataifa ya 'Utalii. Utalii ni moja ya sekta muhimu za mabadilishano ya kiutamaduni baina ya watu wa mataifa mbalimbali. Aidha utalii unaweza kutimia kupitia safari na utalii wa ndani na nje ya nchi kwa madhumuni tofauti. Licha ya kwamba utalii umekuwa na historia ya muda mrefu katika maisha ya mwanadamu, lakini utalii wa mfumo wa kisasa ulianza mwanzoni mwa karne ya 16, wakati yaliposhika kasi mapinduzi ya kiviwanda barani Ulaya na kuvumbuliwa aina mpya ya maisha barani humo. Ni kuanzia karne ya 17 ndipo istilahi ya utalii ilipoenea zaidi hasa katika jamii ya watu wa Ufaransa.

 

Tags