Familia Salama-3 (afya)
Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nasi katika mfululizo huu mpya wa makala kuhusu Afya ya Familia. Makala hizi huangazia masuala mbali mbali ya afya ya familia kama vile lishe, mazoezi, madhara ya matumizi ya mihadarati, umuhimu wa mahaba katika familia n.k. Katika makala yetu hii tatu katika mfululizo huu tutaangazia nafasi ya mboga na matunda katika lishe ya familia. Karibuni kujiunga nasi hadi mwisho.
Mboga na matunda ni vyakula vyenye vitamini, virutubisho viondoavyo sumu (antioxidants) na kambakamba au fiber na vyote hivyo vina nafasi muhimu sana katika kuzuia aina mbali mbali ya saratani na maradhi ya moyo.
Kiwango cha utumizi wa mboga na matunda hutegemea umri, jinsia na harakati za kila siku za mwenye kutumia vyakula hivyo. Inashauriwa kuwa mtu mzima kwa wastani ale milo miwili hadi mine ya matunda kila siku. Mlo moja kwa mfano unaweza kujumuisha tunda moja kama chungwa, nusu glasi ya matunda yenye mbegu dani (Berries) na nusu glasi ya juisi au maji ya matunda na robo glasi ya matunda makavu kama vile tende, zabibu kavu, zaituni. Pamoja na hayo ikumbuwe kuwa juisi ya matunda ina kambakamba au fiber chache ikilinagnishwa na matunda yenyewe. Aidha matunda kamili yanashibisha zaidi ikilinganishwa na juice. Kwa msingi huo inasharuiwa kuwa kadiri ianvyowezekana mtu ajaribu kula matunda moja kwa moja pasina kutengeneza juisi. Ingawa matunda ni mazuri kwa wale ambao wanataka kupunguza unene, lakini kutumia matunda kupita kiasi kunaweza pia kuongeza unene.
Mboga kama vile matango, karoti, tomato au nyanya, kabeji, vitunguu, artichoke, biringanya, saladi ya uwa au lettuce, uyoga n.k ni mboga ambazo zinapaswa kutumiwa kila siku. Kwa wastani kila siku mtu mzima atumie milo mitatu ya mboga. Kila mlo unajumuisha glasi moja ya mboga mbichi, nusu glasi ya mboga zilizopikwa na nusu glasi ya juice ya mboga.
Kutumia kiasi kidogo cha mboga na matunda yamkini kukasababisha maradhi sugu. Ripoti za kitiba zinasema kila mwaka watu wengi hupoteza maisha kwa sababu ya kutotumia kiasi cha kutosha cha mboga na matunda.
Je, wajua kuwa kambakamba au fiber katika mboga na matunda huwa na uwezo wa kupunguza cholesterol yaani lehemu au mafuta mabaya mwilini na hivyo kupunguza uwezekano wa kupata maradhi ya moyo?
Mboga na matunda ni vyakula vilivyojaa potassium, vitamin C na asidi ya foliki na vyote hivyo vina uwezo wa kuleta muujiza katika afya ya mwili.
Mboga na matunda kama vile ndizi, pichi, pea, plamu, apricot ambalo ni tunda la kizungu kama embe dodo, machungwa, viazi, tomato au nyanya na juice yake, spinachi na maharage ni vyakula ambavyo vina kiasi kikubwa cha potassium. Wataalamu wa lishe na tiba wanasema kutumia vyakula hivyo mbali na faida zinginezo pia kusaidia kudhibiti shinikizo la damu.
Mwili wa mwanadamu pia una huhitaji vitamin C ambayo hupatikana katika mboga na matunda kama vile malimau, pilipili hoho, kabichi, spinachi, zabibu na kiwi.
Vitamini C ina virutubisho viondoavyo sumu (antioxidants) na ni muhimu sana katika ustawi wa tishu mwilini. Halikadhalika vitamin C husaIdia vidonda kupona haraka sambamba na kuimarisha meno na ufizi wa meno kwa Kiingereza gum.
Vitamini hii pia husaidia mwili kuweza kutumia ipasavyo ferasi au ferrous. Asidi ya foliki pia husaidia katika kuunda seli nyekundu za damu. Inapendekezwa kuwa wanawake wajawazito watumie aside ya foliki wakati wa uja uzito ili kuzuia kijusi kupata nakisi katika maumbile.
@@@
Kile ambacho tunapaswa kuzingatia hapa ni kuwa, kabla ya kutumia mboga na matunda inapaswa kuosha vyakula hivyo kwa makini. Hii ni kwa sababu mbolea na kemikali zingine ambazo hutumika shambani hubakia katika mboga na matunda na yamkini zikasababisha maradhi au maumivu ya tumbo. Baadhi ya kemikali ambazo hutumika shambani na ambazo hubakia katika mboga au matunda zinaweza kusababisha pia saratani. Inashauriwa kuwa baadhi ya kemikali zisitumike katika mboga au matunda kwani yamkini zikabakia na kumdhuru mtumizi. Kuna baadhi ambao hutumia sabuni na kemikali zinginezo kusafisha mboga au matunda. Wataalamu wa afays wanashauri mbinu hiyo isitumike kwani yamkini ikawa na madhara mabaya kwa afya. na jambo hilo limetajwa kuwa ni hatari. Hatahivyo inashauriwa kutumia kemikali aina ya chlorine. Inafaa kuashiria hapa kuwa chlorine ni miongoni mwa elementi za kemikali muhimu ambayo hutegemewa na wanayasanyi katika kutibu maji yaani kuua vijidudu hatarishi vya magonjwa katika maji, mboga na matunda.
Mpenzi msikilizaji, Kula chakula bora kunamaanisha kula vyakula aina tofauti ya vyakula kila siku kama vile matunda, mboga, maziwa na aina ya vyakula vyenye asili ya nyama wa kufuga kama kuku, mbuzi, ngombe, samaki na na vyakula vya nafaka. Lishe bora linamaanisha pia kula chakula ambacho hakina mafuta mengi, sukari au chumvi nyingi. Aidha zingatia angalau vyakula vya nafaka kama vile mtama, mahindi, mchele, ngano, wimbi, ndegu,
njegere. n.k
Ni bora kula matunda mengi kama ‘maembe, ndizimbivu, papai, pera, chungwa, ubuyu, nanasi, pesheni, zambarau” na mbogamboga kama vile “mchicha, majani ya mboga, karoti, nyanya, mkunde, biringanya” mara kwa mara .
Halikadhalika wataalamu wa afya wanahimiza kulisha kuwalisha watoto vyakula tofauti tofauti kila siku, pamoja na matunda, mboga maziwa na aina yeyote ya vyakula vyenye asili ya nyama, samaki na maharagwe (nafaka).
Ni muhimu pia kupunguza kiasi cha sukari kwenye vinywaji vyao na ulaji wa peremende kwa watoto. Wazazi na walezi wanashauriwa pia kupunguza kiasi cha chakula ambacho hupikwa kwa mafuta ya kuchemka kama vile viazi
karai, vitumbua, kababu, sambusa, soseji na vyakula vingine vyote vya kutumbukizwa kwenye mafuta.
@@@
Wapenzi wasikilizaji kutokana na kubanwa na wakati tunafikia tamati hapa kwa leo katika Makala yetu hii ya familia salama. Ni matumaini yetu kuwa sote tutazingatia na kutunza afya zetu kwa maslahi ya familia na jamii nzima kwa ujumla. Katika Makala yetu ijayo, tutajadili umuhimu wa maziwa na bidhaa za maziwa katika lishe ya mwanadamu. Usikose kujiunga nasi wakati huo kwa majaliwa yake Mola.