Dec 16, 2021 05:09 UTC
  • Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (36)

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wasikilizaji wapenzi wa Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran popote pale yanapokufikieni matangazo haya.

 

Karibuni kutegea sikio sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu ili tuweze kupekua ukurasa mwingine katika kurasa za historia ya Maulamaa wa Kishia pamoja na mchango wao katika Uislamu. Kipindi chetu cha juma lililopita kilimzungumzia Allama Faydh Kashani, mmoja wa wasomi watajika wa Kishia aliyekuwa amebobea katika elimu za falsafa, tafsiri na utambuzi wa hadithi. Tulisema kuwa, mwanazuoni huyu alizaliwa mwaka 1007 Hijria katika mji wa kihistoria na kiutamaduni wa Kashan moja ya miji ya Iran. Tulitaja vitabu viwili mashuhuri vya alimu huyu ambavyo ni al-Wafi na Tafsir al-Safi. Kipindi chetu cha juma hili ambacho ni sehemuu ya 36 kitamzungumzia Sheikh al-Hurr al-Amili mwanazuoni na msomi mwingine maarufu wa Kishia mwandishi wa kitabu cha Wasa'il al-Shia. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

 

 Muhammad bin al-Ḥassan bin Ali bin al-Ḥussei al-Ḥurr al-ʿĀmili al-Mashghari ni msomi na mwanazuoni mkubwa wa Kishia aliyekuwa amebobea katika elimu za hadithi na fikihi na aliishi katika karne ya 11 Hijria. Sheikh al-Hurr al-Amili anahesabiwa kuwa mmoja wa wanazuoni wakubwa na mahiri mno katika ulimwengu wa Kishia na ametunga vitabu vingi. Aidha msomi huyu anahesabiwa kuwa moja ya viunganishi imara na madhubuti vya Shia na riwaya na hadithi za Bwana Mtume (saw) na Maimamu watoharifu (as).

 

 

Sheikh Hurr Amili alizaliwa usiku wa kuamkia Ijumaa tarehe 8 ya mwezi Rajab Hijria katika kijiji cha Mashghara katika viunga vya Jabal Amil nchini Lebanon. Familia yake ilikuwa imeshikamana barabara na dini na ilikuwa na mapenzi makubwa na dhuria na watu wa nyumba ya Bwana Mtume (saw). Eneo alilozaliwa Sheikh Hurr lilikuwa moja ya ardhi ambazo wakazi wake walikuwa Mashia na miongoni mwa maeneo yaliyokuwa yakilea na kutoa Maulamaa na wanazuoni wakubwa.

 Baadhi ya wanahistoria wanamtaja na kumtambua Sheikh Hurr Amili kama anayetokana na kizazi cha Hurr bin Yazid al-Riyahi mmoja wa masahaba wa Imam Hussein (a.s) aliyeuawa shahidi katika tukio la Karbala. Familia ya Sheikh Hurr Amili ilikuwa mashuhuri kwa elimu, maadili mema na kubobea katika taaluma ya fikihi na utambuzi wa masuala ya sheria za Kiislamu. Baba yake Sheikh Hurr Amili alikuwa msomi mahiri wa fikihi na mwanafasihi stadi na mahiri na ambaye alichukua yeye mwenyewe jukumu la kuwafuundisha watoto wake. Mama yake alikuwa mwanamke mwema na mcha-Mungu ambapo shakhsia wakubwa walikuwa wakimtambua kuwa mtu mwenye fadhila na maadili mema.

 

 

Sheikh Amili alisoma masomo ya msingi kwa baba na babu yake pamoja na mjomba na ami yake ambao wote walikuwa mafakihi yaani waliobobea katika elimu ya fikihi na wasomi wakubwa katika zama hizo.

 Baadaye alielekea Jbaa na kusoma kwa Sheikh Zeinuddin mjukuu wa Shahidi Thani na Sheikh Dhuhairi. Sheikh Hurr Amili anafahamika miongoni mwa mafakihi kwamba, kwa upande wa mtazamo wa kielimu ni mtu anayefuata mrengo wa Akhbariyuun. Jina hili limepewa kundi la wanazuoni wa kifikihi wa Kishia ambao wakiwa na lengo la kufikia hukumu za sheria na taklifu za Mwenyezi Mungu wanaamini kuwa kufuata habari na hadithi za Mtume (saw) na Maimamu watoharifu (as) kunatosha.

 Mkabala na kundi hili kuna mrengo unaojulikana kama Usuliyuun ambao wao wanaamini kuwa, ili kunyambua hukumu na maamrisho na makatazo ya dini, mbali na kuhitajia Qur'ani na hadithi tunahitajia pia istinbaat na unyambuzi wa kiakili. Licha ya tofauti hizo, Maulamaa wa Usuliyuun na Akhbariyuun itikadi yao ni moja katika masuala ya teolojia na kiimani, tofauti yao ipo tu katika mbinu na namna ya kielimu ya kufikia hukumu hizo. Hivyo hii ndio tofauti ya Akhbariyuun na Usuliyuun na Sheikh al-Hurr al-Amili anahesabiwa kuwa ni katika kundi la Akhbariyuun.

Muhammad bin al-Ḥassan bin Ali bin al-Ḥussei au Sheikh al-Ḥurr al-ʿĀmili kama anavyojulikana zaidi kwa jina hilo, alibakia katika mji wa Jabal Amil hadi alipofikisha umri wa miaka 40 na mwaka 1073 Hijria alifunga safari na kuelekea katika mji wa Mash'had Iran kwa ajili ya kuzuru Haram ya Imam Ali bin Mussa al-Ridha (as). Baadaye alikata shauri kubakia katika mji huo mtakatifu jirani na Haram ya Imam Ridha (as) hadi mwishoni mwa uhai wake na hivyo kuwa katika kivuli cha utulivu kilichokuwa kwa Mashia nchini Iran. Katika kipindi hicho alianza kufundisha na kuandika vitabu.

 

Kikao na darsa za Sheikh al-Hurr al-Amili katika mji wa Mash'had zilihudhuriwa kwa wingi na wanafunzi waliokuwa na kiu ya elimu ya Ahlul-Baiti (as). Katika kipindi cha kuishi kwake Mash'had alifanikiwa kufanya ziara mara mbili katika miji mitakatifu ya Najaf na Karbala huko Iraq. Alifanya safari mara moja pia katika mji wa Isfahan na ni katiKa safari hiyo ndipo alipokutana na Allama Majlisi na kuchukua idhini kutoka kwake ya kunukuu hadithi.

Sheikh Hurr Amili alikuwa mashuhuri pia kwa ushujaa na uhuru wa kusema kile alichokuwa akikiamini. Siku moja mwanazuoni huyu alialikwa katika kikao cha Shah Suleiman Safavi huko katika mji wa Isfahan. Mtawala Suleiman Safavi hakuwa kiongozi mwema na anayestahiki. Alitambulika kwa ulevi na unywaji mvinyo, mtenda dhulma na asiye na mipango ya uongozi. Kuweko mwanazuoni na msomi wa Kiislamu kama Hurr Amili katika kikao cha kiongozi mwenye sifa kama hizi halikuwa jambo zuri na la kupendeza. Hata hivyo, uwepo wa Sheikh al-Hurr al-Amil katika kikao hicho ulikuwa kwa namna ambayo aliwaonyesha wote kuhusu itikadi ya mfalme huyu na kupelekea kuumbuka kiongozi huyo.

Sheikh Hurr Amili aliingia katika kikoa hicho na kwenda kukaa katika eneo la juu la kukkaa waheshimiwa bila ya kuomba idhini kutoka kwa mfalme Shah na kisha akaegemea kiti cha mfalme. Hii ni katika hali ambayo, baina yake na mfalme kulikuwa na umbali wa mto mmoja wa kuegemea. Mfalme akawauliza watu wa karibu yake, Bwana huyu ni nani ambaye anaonyesha utovu wa adabu? Wakamwabia, huyu ni alimu na msomi mkubwa na mtajika.

 

Mfalme yule akamgeukia Sheikh Hurr na kumuuliza kuna umbali gani wa tofauti baina ya Hurr na Kharr? Katika lugha ya Kifarsi maneno mawili ya Hurr na Kharr uandishi wake ni mmoja isipokuwa kuna tofauti ndogo tu ambayo ni nukta katika Khe. Ambapo Khar ina maana ya punda. Hivyo Sheikh akajibu kwa kusema, umbali baina ya Hurr yaani yeye na Kharr yaani punda (akimkusudia mfalme) ni mto ulioko baina yao. Kwa jibu lake akawa amemuumbua Shah Suleimani Safavi.  Baada ya tukio hilo, mfalme huyo alipata udadisi wa kujua zaidi kuhusia na Sheikh Amili. Wakati alipofahamu daraja na elimu ya sheikh Hurr Amili akamualika Isfahan lakini Sheikh alikataa mwaliko huo na kuubakia Mash;had. Shah akamteua na kufanya Kadhi Mkuu na Sheikhul Islami.

 

 

Sheikh Hurr Amili ameandika vitabu vingi vilivyokuwa na mbinu ya uhakiki na umakini. Hata hivyo kitabu chake mashuhuri zaidi ni cha Wasa'ail al-Shia. Kitabu hicho mashuhuri ni moja ya marejeo muhimu katika taaluma ya hadithi ambacho kina itibari maalumu baina ya vitabu vya hadithi.

Hatimaye Sheikh Hurr Amili aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 72 na kuzikwa jirani na Haram ya Imam Ali bin Mussa al-Ridha mjini Mash'had.

Wapenzi wasikilizaji kwa leo nakomea hapa, nikitaraji kwamba, mumenufaika vya kutosha na yale niliyokuandalieni kwa leo, basi hadi tutakapokutana tena wiki ijayo panapo majaliwa yake Mola karima, ninakuageni nikikutakieni kila la kheri.

Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh