SAYANSI 151
Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii ambayo huangazia matukio mbali mbali ya sayansi, tiba na teknolojia nchini Iran na maeneo mengine duniani. Ni matumaini yangu kuwa utanufaika.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetangaza azma ya kutuma satalaiti zake kadhaa katika anga za mbali katika kipindi cha miezi michache ijayo.
Hayo yamedokezwa na Waziri wa Mawasiliano na TEHAMA Iran Issa Zarepour ambaye amesema satalaiti hizo zimeundwa na vijana wataalamu ndani ya nchi. Amesema Iran sasa inalenga kuwa miongoni mwa nchi chache dunaini zenye uwezo wa kutuma satalaiti katika anga za mbali katika eneo la GEO.
Baada ya kufanikiwa kufikisha satalaiti zake katika eneo la anga ya mbali lijulikanalo kama LEO ambalo liko umbali wa kilomita 2,000 sasa Iran inakusudia kufikisha satalaiti zake katika anga ya mbali zaidi ijulikanayo kama GEO yenye umbali wa kilomita 35,786.
Hivi karibuni akihutubu katika kikao cha kwanza cha Baraza Kuu la Anga za Mbali la Iran ambacho kilifanyika Ijumaa Disemba 3, Rais Ibrahim Raisi aliashiria umuhimu wa ustawi wa viwanda vya kitaifa vya sekta ya anga za mbali ambapo ametoa wito kwa taasisi zote husika kujitahidi katika uga huo.
Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, Iran imejitahidi sana katika kuunda maroketi au makombora ya kubeba sataliti. Kabla ya kuunda maroketi hayo, Iran tayari ilikuwa imeshapata uwezo wa kuunda satalaiti na hivyo ikawa inahitaji chombo cha kurushia satalaiti hizo katika anga za mbali. Hali kadhalika Iran imeweza kuunda kituo cha ardhini cha kuwasiliana na satalaiti na kupokea taarifa zote zinazotumwa na sataliti hizo. Kwa msingi huo, Iran sasa imekamilisha mzunguko kamili unaohitajika katika uga wa sataliti.
Hivi sasa ni nchi sita tu duniani zilizo na uwezo wa kuunda vituo vya kurusha sataliti katika anga za mbali na Iran sasa ni ya saba duniani katika uga huo.
Azma ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika ustawi wa kisayansi pamoja na kuwepo vikwazo na mashinikizo ya juu kabisa ya Marekani ni nukta inayoashiria kuwa, mchakato wa ustawi wa kasi katika nchi hii hautacheleweshwa na hadaa pamoja na propaganda za vyombo vya habari ajinabi.
Maabara za Kompyuta Tanzania
WAZIRI wa Nchi wa Ofisi ya Rais anayeshughulikia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) wa Tanzania Ummy Mwalimu ametangaza kwamba shule zote mpya za sekondari za umma zitakazojengwa zitawekewa maabara za kompyuta ili kuongeza taarifa za kidijitali katika nchi hiyo.
Ummy Mwalimu amesema kwamba kuundwa kwa maabara za kompyuta katika shule mpya za sekondari za umma kutawawezesha walimu kufundisha teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) somo la msingi la taarifa za kidijitali.
Mwalimu ameyasema hayo Disemba 16 wakati alipofungua mkutano wa siku tatu wa walimu wakuu wa shule za sekondari ulioandaliwa kwa pamoja na Global Education Link (GEL) na Chama cha Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSSA) katika mji mkuu wa kibiashara wa Dar es Salaam.
Mwalimu amesema, serikali inapanga kufungua maabara za kompyuta na vifaa vya TEHAMA kwenye shule mpya 1,500 za sekondari katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia Mwaka 2022.
Dawa ya COVID-19
Bara Ulaya kupitia taasisi ya usimamizi wa dawa, EMA imeidhinisha matumizi ya dawa mpya ya COVID-19, kutokana na kitisho kinachotokana na ongezeko la maambukizi ya aina mpya ya kirusi cha corona, Omicron.
Kulingana na EMA, dawa hiyo inapunguza hatari ya wagonjwa walio na dalili hatarishi kulazwa hospitalini ama kufariki. Aina ya tatu ya dawa iliyodhinishwa kutumika kwa dharura ni Xeduvy.
EMA pia imeidhinisha matumizi ya dharura ya vidonge vya COVID-19 ya shirika la Pfizer na kusema dawa hiyo inaweza kutumika kuwatibu watu wazima walioambukizwa COVID-19 na wasiohitaji Oksijeni, lakini wanaweza kupata dalili mbaya zaidi.
Kinachosubiriwa sasa ni tume ya Ulaya yenye mamlaka ya mwisho ya kuidhinisha matumizi ya dawa hizo.
Nchini Marekani, idara za kupambana na kudhibiti magonjwa imewataka raia nchini humo kuchagua kupata chanjo za aina nyingine mbili zilizoidhinishwa nchini humo, mbali na Johnson&Johnson kutokana na visa vya kuganda kwa damu. Kamati ya ushauri ya CDC ilikubaliana kwa umoja kuidhinisha chanjo za Moderna na Pfizer/Biontech, badala ya J&J. Wataalamu wa CDC wamesema hatari ya kuganda damu iko juu ikilinganishwa na ilivyodhaniwa awali kwa wanaume na wanawake, na tayari takriban watu tisa wamefariki kutokana na tatizo hilo.

Chanjo ya Pfizer ni dhaifu mkabala wa Omicron
Uchunguzi umebaini kuwa chanjo ya Kimarekani ya Pfizer imedhoofika na haizuii wagonjwa wa kirusi cha COVID-19 kulazwa hospitalini baada ya kuibuka aina mpya ya kirusi hicho ya Omicron.
Utafiti uliofanywa kwa kuchunguza data za kila siku umebani kuwa, baina ya Novemba 15 na Disemba 7 watu waliokuwa wamepata dozi mbili za chanjo ya Pfizer sasa wana uwezo wa asilimia 70 wa kutolazwa hospitalini kutokana Omicron wakati ambao katika kukabiliana na aina ya COVID-19 ijulikanayo kama Delta kiwango hicho kilikuwa ni asilimia 93.
Katika kuzuia maambukizi kwa ujumla, uchunguzi uliofanywa na Discovery Health, ambalo ni shirika kubwa zaidi la bima binafsi ya afya nchini Afrika Kusini, umebaini kuwa uwezekano wa kuambukizwa COVID-19 kwa waliodungwa chanjo ya Pfizer umeongezeka kwa kiasi kikubwa. Hapo kabla uwezekano wa kutopata maambukizi ya COVID-19 baada ya chanjo ya Pfizer ulikuwa asilimia 80 lakini sasa ni asilimia 33.
Msingi wa uchunguzi huo ni watu 211,000 waliopatikana wameambukizwa COVID-19 ambapo 78,000 walikuwa na Omicron, ambayo ni aina ya kirusi cha corona kilichoenea katika maeneo mengi duniani.
Hata hivyo shirika la Discovery limesema uchunguzi huu ni wa awali. Afrika Kusini inategemea chanjo za Kimarekani za Pfizer-BioNTech na Johnson & Johnson katika kampeni yake ya chanjo ambapo hadi sasa dozi milioni 20 za Pfizer zimetolewa.
Ebola haipo tena DRC
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imetangaza kuwa, mripuko mpya wa homa ya ebola uliozuka kwenye jimbo la Kivu ya Kaskazini mnamo mwezi Oktoba ukiwa ni wa pili kwa mwaka 2021 sasa umemalizika.
Tangazo la kumalizika mripuko huo limetolewa na mamlaka ya kitaifa ya afya nchini Kongo DR baada ya kutokuwapo mgonjwa yeyote mpya aliyeripotiwa mwishoni mwa siku 42 za kuangalia na kufuatilia ugonjwa huo, au vipindi viwili vya kusubiria tangu kuliporipotiwa mgonjwa wa mwisho na kuruhusiwa kwenda nyumbani.
Kwa jumla, kulikuwa na wagonjwa 11 ambapo wanane walithibitishwa, huku watatu wakishukiwa, ikijumuisha pia vifo sita vilivyoripotiwa katika mripuko huo uliotangazwa rasmi tarehe 8 Oktoba baada ya kisa kipya kuthibitishwa katika eneo la afya la Beni kwenye mkoa wa Kivu Kaskazini ambapo mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka mitatu alifariki katika mji huo kwa homa hiyo ya ebola.
Akitangaza kumalizika rasmi kwa mripuko huo wa ebola mnamo Alhamisi 17 Disemba, Waziri wa Afya wa Jamhuri ya Kidermokrasia ya Kongo Jean-Jacques Mbungani amesema, mripuko wa mara hii ulichelewa kugunduliwa kutokana na mgomo uliofanywa na wahudumu wa sekta ya afya katika eneo hilo.
Shirika la Afya Duniani WHO limetangaza kuwa, mripuko wa mara hii ulikuwa wa 13 na ulitokea katika eneo hilo la Kivu Kaskazini sawa na mripuko wa 2018 ambao ulidumu kwa miaka miwili.
Zaidi ya watu 1800 wamechanjwa katika kampeni iliyoanza siku tano tu baada ya mgonjwa wa kwanza kugunduliwa.
Mripuko mpya wa homa ya ebola nchini Kongo DR umefuatiwa na matumizi ya chanjo ya ugonjwa huo ya ERVEBO iliyoidhinishwa hivi majuzi kutumika nchini humo