Dec 27, 2021 02:38 UTC
  • Jumatatu, Disemba 27, 2021

Leo ni Jumatatu tarehe 22 Mfunguo Nane Jamadil Awwal 1443 Hijria sawa na Disemba 27 mwaka 2021 Milaadia.

Miaka 199 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa tabibu na mwanakemia wa Kifaransa, Louis Pasteur. Akiwa shuleni alisoma kwa bidii na jitihada kubwa. Baada ya kumaliza masomo yake alifanikiwa kupata shahada ya uzamivu katika kemia na kuanza kufundisha katika Chuo Kikuu cha Strasbourg huku akijihusisha pia uhakiki na utafiti kuhusiana na masuala mbalimbali ya kielimu.

Louis Pasteur

Miaka 67 iliyopita katika siku kama ya leo, Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) ulianzishwa. Miongoni mwa yaliyokuwa malengo muhimu ya mfuko huo, ni kuandaa nafasi zaidi za ajira, udhibiti wa thamani ya sarafu za kigeni na kuhakikisha kwamba, kunakuweko ukuaji wenye uwiano katika masoko ya kimataifa. Makao Makuu ya Mfuko wa Fedha wa Kimataifa yako mjini New York, Marekani.

Siku kama ya leo miaka 14 iliyopita, Benazir Bhuto, mkuu wa chama cha Wananchi cha Pakistan aliuliwa na magaidi kwa kupigwa risasi na kwa mripuko wa bomu huko Rawalpindi, kaskazini mashariki mwa Pakistan. Wanachama wengine wasiopungua 20 wa chama cha Benazir Bhutto nao waliouawa kwenye shambulio hilo la kigaidi. Benazir Bhutto alizaliwa mwaka 1953 katika mji wa bandari wa Karachi, kusini mwa Pakistan. Alipata elimu yake ya juu katika Vyuo Vikuu vya Harvard, Marekani na Oxford, Uingereza na alirejea Pakistan mwaka 1977. Muda mfupi baadaye, Zulfikar Ali Bhutto, baba wa Benazir Bhutto ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa Pakistan alivuliwa madaraka na miaka miwili baadaye watawala wa kijeshi walimnyonga kwa tuhuma za mauaji. Wakati huo Benazir Bhutto alikuwa na umri wa miaka 26 na alichukua uongozi wa chama hicho mara baada ya kuuawa baba yake. Mwaka 1988 Benazir Bhutto alifanikiwa kuwa Waziri Mkuu wa Pakistan baada ya kupinduliwa utawala wa wanajeshi ulioongozwa na Jenerali Muhammad Zia-ul-Haq.

Benazir Bhuto

Siku kama ya leo miaka 13 iliyopita, alifariki dunia Ayatuhil Udhma Muhammad Taqi Behjat Foumani, mmoja wa Marajii Taqlidi na maurafaa wakubwa wa Kishia. Alizaliwa mwaka 1294 Hijria Shamsia katika mji wa Fouman ulioko katika mkoa wa Gilan kaskazini mwa Iran. Baada ya kupata elimu ya msingi ya kidini, mwaka 1308 Hijria Shamsia alielekea katika Chuo Kikuu cha Kidini cha Najaf nchini Iraq. Ayatullah Bahjat alikuwa mashuhuri sana kutokana na uchaji Mungu wake. Kitabus Swalat, Jamiul Masail na Wasilatun Najat ni baadhi ya vitabu mashuhuri vya msomi huyo.

Ayatuh Muhammad Taqi Behjat 

Katika siku kama ya leo miaka 13 iliyopita, jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel lilianzisha hujuma kubwa na ya pande zote katika Ukanda wa Gaza magharibi mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Wakazi wa eneo hilo waliwakasirisha viongozi wa Kizayuni kutokana na kupambana kwao kishujaa dhidi ya uchokozi na mashambulizi ya Wazayuni na pia hatua yao ya kuiunga mkono serikali halali ya Palestina iliyokuwa ikiongozwa na harakati ya Hamas. Ni kwa sababu hiyo ndio maana Ukanda wa Gaza ukawekwa chini ya mzingiro wa kiuchumi wa utawala haramu wa Israel kwa karibu mwaka moja na nusu kabla ya mashambulizi hayo, mzingiro ambao unaendelea kuwasababishia Wapalestina wa eneo hilo matatizo chungu nzima kama vile ukosefu wa chakula na dawa.

Mashambulizi ya Israel dhidi ya watu wa Gaza

 

Tags