Jan 03, 2022 02:33 UTC
  • Jumatatu, Januari 3, 2022

Leo ni Jumatatu tarehe 29 Mfunguo Nane Jamadil Awwal 1443 Hijria sawa na Januari 3 mwaka wa 2022.

Katika siku kama ya leo miaka 35 iliyopita, Sayyid Mahdi Hakim aliyekuwa mjumbe muhimu wa Baraza Kuu la Kiislamu la Iraq na mwana wa Ayatullah Sayyid Muhsin Hakim mmoja wa marajii wakubwa wa Kiislamu aliuawa shahidi na makachero wa utawala wa Saddam Hussein dikteta wa zamani wa Iraq, huko Khartoum mji mkuu wa Sudan. Sayyid Mahdi Hakim alikuwa mmoja wa wanafunzi wa shahidi Ayatullah Sadr na mmoja wa wapinzani wakuu wa utawala wa Saddam Hussein.

Ayatullah Sayyid Mahdi Hakim

Siku kama ya leo miaka 33 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 13 Dei 1367 Hijria Shamsia, ujumbe wa Imam Ruhullah Khomeini, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran uliwasilishwa kwa Mikhail Gorbachev kiongozi wa mwisho wa Umoja wa Kisovieti akimlingania dini ya Kiislamu na kumtaka aachane na fikra za Kimaksi. Katika sehemu moja ya ujumbe huo Imam Khomeini alisema: "Tatizo kuu la nchi yako si suala la umiliki, uchumi wala uhuru, bali ni kutokuwa na imani ya kweli juu ya Mwenyezi Mungu; na tatizo hilo ndilo lililoitumbukiza au litakaloitumbukiza Magharibi katika mporomoko wa kimaadili na kuifanya igonge ukuta. Tatizo lenu kubwa ni kupigana vita visivyokuwa na faida dhidi ya Mwenyezi Mungu." Mwishoni mwa ujumbe huo Imam Khomeini alisema: "Tokea sasa Ukomonisti unapaswa kutafutwa kwenye majumba ya makumbusho ya kisiasa duniani; kwani hauwezi kukidhi mahitaji halisi ya mwanadamu." Imam Khomeini alimuusia Gorbachev akisema: "Nakutaka ufanye uchunguzi wa kina kuhusu Uislamu, sio kwa sababu Uislamu na Waislamu wanakuhitajia wewe, hapana, bali kutokana na thamani za hali ya juu na za ulimwengu mzima za dini hiyo ambayo inaweza kuwa wenzo wa ufanisi na uokovu wa mataifa mbalimbali na kukidhi matatizo makubwa ya mwanadamu."

Mikhail Gorbachev

Katika siku kama ya leo miaka 29 iliyopita, inayosadifiana na Januari 3, 1993 kulitiwa saini makubaliano ya Start-2 kati ya Marais wa zamani wa Russia na Marekani, Boris Yeltsin na Bill Clinton. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, nchi hizo mbili zinapaswa kupunguza theluthi mbili za silaha zao za nyuklia. Makubaliano ya Start-1 yenye lengo hilohilo yalitiwa saini mwaka 1987 kati ya Marais Mikhael Gorbachev wa Russia na Ronald Reagan wa Marekani. Hata hivyo badala ya kuanza kuharibu silaha zake za nyuklia, Marekani ilijilimbikizia sialaha zaidi za aina hiyo suala ambalo liliilazimisha pia Russia kusitisha mpango wa kuanza kuharibu silaha zake za atomiki.

Start-2

Katika siku kama hii ya leo miaka 2 iliyopita Kamanda wa Kiislamu, Haj Qasem Soleimani, fahari na kinara wa Iran katika mapambano dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh (ISIS), aliuawa shahidi katika shambulio la kikatili na la kigaidi la ndege za kivita za Marekani huko Iraq. Shahidi Qasem Soleimani alizaliwa tarehe 11 Machi 1957 katika kijiji cha milimani cha Raboor katika mkoa wa Kerman. Kamanda Soleimani alitumia kipindi cha utoto akakiwa pamoja na baba yake na wakati wa ujana alikua mkandarasi katika Shirika la Maji la Kerman. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu alijiunga na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH). Baada ya kuanza vita vya Saddam Hussein dhidi yay Iran, Qasem Soleimani alianza kutoa mafunzo kwa vikosi vya askari wa Kerman na kuwatuma kwenye maeneo ya vita kwenye mipaka ya kusini; na muda mfupi baadaye, yeye mwenyewe alitumwa huko Susangard akiongoza kikosi cha jeshi ili kuzuia kusonga mbele jeshi la utawala wa Baath. Mwaka 1360 Hijria Shamsia aliteuliwa na kamanda mkuu wa wakati huo wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Mohsen Rezaei kuwa kamanda wa kikosi cha 41 cha Tharullah. Alishiriki katika operesheni nyingi na jeshi lake ikiwa ni pamoja na Walfajr 8, Karbala 4, Karbala 5 na Tak Shalamcheh. Mwishoni mwa vita, Kamanda Qasem Soleimani aliteuliwa na Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuwa Kkamanda wa Kikosi cha Quds na mwaka 1389 Hijria Shamsia, alipandishwa cheo na kuwa Meja Jenerali (cheo cha juu zaidi cha kijeshi nchini Iran). Baada ya kudhihiri kundi la kigaidi la ISIS huko Iraq na Syria, Shahidi Soleimani, kwa ombi la serikali za Iraq na Syria, alielekea kwenye nchi hizo akiwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Iran na kuongoza mapambano dhidi ya magaidi hao na alikuwa na nafasi na mchango wa aina yake katika kuliangamia kundi hilo. Hata hivyo maadui wa Iran ya Kiislamu hawakuweza kustahimili mafanikio na ushindi huo, na hatimaye Jenerali Qasem Soleimani asubuhi ya Ijumaa, tarehe 3 Januari 2020 aliuawa shahidi akiwa pamoja na Abu Mahdi al -Mohandes, Naibu Kamanda wa Jeshi la Wananchi wa Iraq, Al-Hashd al-Shabi na wenzao kadhaa katika shambulio la kigaidi la helikopta za Kimarekani katika uwanja wa ndege wa Baghdad. Shahidi Soleimani alikuwa safarini nchini Iraq kwa mwaliko wa waziri mkuu wa wakati huo wa Iraq. 

Haj Qasem Soleimani

 

Tags