Ijumaa tarehe 21 Januari 2022
Leo ni Ijumaa tarehe 18 Jamadithani 1443 Hijria sawa na Januari 21 mwaka 2022.
Siku kama ya leo miaka 424 iliyopita aliuawa shahidi Kadhi Sayyid Nurullah Shushtari, faqihi, mwanatheolojia na alimu mkubwa. Alizaliwa mwaka 956 Hijiria katika familia bora na ya kielimu mjini Shushtar, kusini magharibi mwa Iran. Sayyid Nurullah Shushtari alijifunza masomo ya awali ya kidini kwa baba yake na kisha akaelekea mjini Mash’had, kaskazini mashariki mwa Iran na kuweza kustafidi na elimu kutoka kwa maulama wakubwa wa mji huo. Yapata mwaka 993, Kadhi Sayyid Nurullah Shushtari alielekea India kwa ajili ya kufanya tablighi ambapo wakati huo nchi hiyo ilikuwa chini ya utawala wa Mfalme Akbar Shah katika silsila ya Mongolia. Hadhi yake, elimu na uadilifu wa Sayyid Shushtari vilimfanya ateuliwe kuwa kadhi wa mji wa Lahore nchini humo. Baada ya kufariki dunia Mfalme Akbar Shah, wapinzani wa alimu huyo walimwendea mfalme aliyechukua uongozi kwa jina la Jahangir Shah na kumwambia maneno ya uongo na ya uchonganishi ambapo kwa kutumia kisingizio cha madhehebu ya Shia ya alimu huyo mkubwa akauawa shahidi katika siku kama ya leo. Sayyid Nurullah Shushtari aliandika vitabu kadhaa miongoni mwavyo ni ‘Majaalisu-Mu’miniina’ ‘Ihqaaqul-Haqqi’ na ‘Tuhfatul-Uquul.’

Katika siku kama ya leo miaka 278 iliyopita tufani kubwa ililikumba eneo la Ghuba ya Bengali mashariki mwa India na kuua watu laki tatu. Tufani hiyo ilitambuliwa kuwa kimbunga kilichosababisha maafa makubwa zaidi katika eneo hilo.
Ghuba ya Bengali iko kaskazini mwa Bahari ya Hindi na kusini mwa Asia na ni miongoni mwa maeneo ambayo hukumbwa na mafuriko na vimbunga vya mara kwa mara vinavyosababisha maafa makubwa ya nafsi na mali.

Siku kama ya leo miaka 229 iliyopita Mfalme Louis XIV wa Ufaransa alinyongwa. Alichukua hatamu za uongozi mwaka 1774 na kuathiriwa mno na mkewe Marie-Antoinette. Mwaka 1789 wananchi wa Ufaransa walianzisha mapambano dhidi ya Mfalme Louis XIV kutokana na hali mbaya ya kiuchumi na kijamii na miaka mitatu baadaye serikali ya kifalme ilifutwa rasmi nchini Ufaransa. Hata hivyo kutokana na kuwa mfalme Louis alikuwa ameomba msaada wa nchi za kigeni kwa siri alituhumiwa kuwa amefanya uhaini na kuhukumiwa kifo. Watu kadhaa wa familia ya Mfalme Louis XIV akiwemo mkewe Marie-Antoinette pia walinyongwa.

Tarehe 18 Jumadithani miaka 162 iliyopita aliaga dunia faqihi na msomi mkubwa wa Kiislamu, Sheikh Murtadha Ansari katika mji mtakatifu wa Najaf huko Iraq. Alizaliwa mwaka 1214 Hijria Shamsia katika mji wa Dezful nchini Iran na baada ya kupata elimu ya msingi kwa baba yake alielekea katika miji mitakatifu ya Karbala na Najaf huko Iraq kwa ajili ya elimu ya juu. Miaka kadhaa baadaye Sheikh Ansari alitambuliwa kuwa miongoni mwa wanazuoni na walimu mashuhuri wa zama hizo. Msomi huyo wa Kiislamu ameandika vitabu vingi vikiwemo vile vya Rasail na Makasib ambavyo vingali vinatumiwa hadi sasa kufundishia katika vyuo vikuu vya kidini.

Na siku kama ya leo miaka 43 liyopita sambamba na kuanza kutetereka nguzo za utawala wa Shah nchini Iran mkabala wa wimbi kubwa la mashinikizo ya wananchi na harakati za Mapinduzi ya Kiislamu, serikali ililazimika kuwaachia huru wafungwa waliokuwa katika jela za Shah na wananchi Waislamu wa Iran wakawapokea watoto wao waliokuwa wakiteseka kwa miaka mingi katika jela hizo. Alasiri ya siku hiyo maafisa wa Jeshi la Anga la Iran walifanya maandamano na kutangaza uungaji mkono wao kwa harakati ya taifa la Kiislamu la Iran. Siku hiyo hiyo pia magazeti ya Iran yaliandika habari iliyokuwa na kichwa kilichokolezwa wino kwamba: "Imam Khomeini Kurejea Iran Siku Kadhaa Zijazo". Habari hiyo ilizusha wimbi la hamasa na furaha kubwa kati ya wananchi wanamapinduzi wa Iran na kila mtu alianza kujitayarisha kwa ajili ya kwenda kumpokea kiongozi wa kihistoria wa Mapinduzi ya Kiislamu Imam Ruhullah Khomeini.
