Nov 15, 2025 02:39 UTC
  • Jumamosi, 15 Novemba 2025

Leo ni Jumamosi 24 Mfunguo Nane Jamadul-Awwal 1447 Hijria mwafaka na 15 Novemba 2025 Miladia.

Siku kama ya leo miaka  409 iliyopita, aliaga dunia Shah Abbas Safavi, mmoja wa wafalme wa ukoo wa Safavi. Aliaga dunia katika mji wa Behshahr Mazandarn Iran. Kipindi cha utawala wa Shah Abbas, mfalme mashuhuri wa ukoo wa Safavi kilikuwa na umuhimu maalumu kutokana na kuweko wanazuoni, Maulamaa na wanasanii mahiri.

Shah Abbas Safavi,

 

Katika siku kama ya leo miaka 395 iliyopita, alifariki dunia Johannes Kepler, mwanahisabati, mnajimu na mtaalamu wa nyota wa Kijerumani. Kepler alizaliwa mwaka 1517 na baada ya kuhitimu masomo yake alielekea Austria na kuanza kufundisha. Baadaye Kepler alifahamiana na Tycho Brahe, mnajimu mtajika wa Denmark na kuanzia hapo taratibu akavutiwa na elimu ya nyota kutoka kwa msomi huyo. Kepler alichunguza na kufanya utafiti katika uwanja huo kwa miaka mingi. 

Johannes Kepler

 

Miaka 156 iliyopita katika siku kama ya leo alizaliwa Vasily Bartold, mustashiriki maarufu wa Russia huko Saint Petersburg. Bartold alisoma na kuhitimu elimu katika chuo kidogo cha lugha za Mashariki huko huko Saint Petersburg na kuwa hodari katika lugha za Kifarsi, Kiarabu na Kituruki. Akiwa na umri wa miaka 27, alifikia daraja la mhadhiri msaidizi katika chuo hicho kuifundisha historia ya mataifa ya Mashariki. Alifanya utafiti mkubwa katika uwanja huo. Aidha kwa kipindi fulani alifanya safari huko Turkestani kwa minajili ya kuendeleza utafiti wake na kubahatika kuandika utafiti huo katika kitabu chake alichokipa jina la 'Turkestani katika kipindi cha mashambulizi ya Mongoli.'

Vasily Bartold

 

Tarehe 24 Aban miaka 46 iliyopita, siku chache baada ya kuvamiwa na kutekwa Pango la Ujasusi la uliokuwa ubalozi wa Marekani hapa mjini Tehran, serikali ya Marekani katika radiamali yake kali dhidi ya hatua hiyo ya kimapinduzi, ilizuia fedha za kigeni za Iran katika mabenki yake yote duniani. Kufungwa kwa akaunti za Iran, kulipelekea mashinikizo ya kiuchumi ya serikali ya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuchukua mkondo mpana zaidi. Siku chache kabla ya hatua hiyo, Iran ilikuwa imesimamisha uuzaji wa mafuta yake kwa Marekani kutokana na hatua na misimamo ya chuki ya Washington dhidi ya Jamhuri ya kiislamu ya Iran.

 

Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita, utungaji na upasishaji wa katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ulikamilishwa na Baraza la Wataalamu. Katiba hiyo ilianisha na kuupasisha mfumo wa Kiislamu uliojengeka juu ya misingi ya mafunzo na matukufu ya Kiislamu hasa uadilifu katika jamii na kuheshimiwa haki za binadamu. Baada ya katiba hiyo kupasishwa kulifanyika kura ya maoni ya wananchi wote na katiba hiyo ikapasishwa kwa wingi wa kura.

 

Siku kama ya leo miaka 44 iliyopita, alifariki dunia mwanafalsafa, mfasiri mkubwa wa Qur'ani na msomi mashuhuri wa Kiislamu Allamah Muhammad Hussein Tabatabai akiwa na umri wa miaka 80. Mwanazuoni huyo mkubwa alizaliwa katika mji wa Tabriz, kaskazini magharibi mwa Iran. Msomi huyo wa Kiislamu alikuwa hodari sana katika elimu za falsafa, irfani, tafsiri ya Qur’ani na vilevile katika masuala ya fasihi, hisabati na fiqhi. Allamah Tabatabai ameandika vitabu vingi na miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni tafsiri ya Qur'ani ya al-Mizan.

Allamah Muhammad Hussein Tabatabai

 

Tarehe 15 Novemba mwaka 1988  yaani miaka 37 iliyopiota, lilitolewa tangazo la kuundwa taifa huru la Palestina, na siku hiyo ikapewa jina la Siku ya Uhuru wa Nchi Palestina. Katikati ya Novemba 1988, Baraza la Kitaifa la Palestina, ambalo lilianzishwa mwaka mmoja kabla, lilifanya mkutano nchini Algeria na kutangaza uwepo wa "nchi huru ya Palestina" mnamo Novemba 15, 1988. Baitul Muqaddas pia iliteuliwa kuwa mji mkuu wa nchi hiyo. Siku 10 baada ya mkutano huo, nchi 54 za dunia zilitambua kuwepo kwa taifa huru la Palestina. Hata hivyo kuna vikwazo vingi vya ya kuweko utawala wa taifa huru la Palestina katika ardhi ya taifa hilo, kubwa zaidi ni utawala wa Kizayuni wa Israel. 

 

Katika siku kama ya leo miaka 25 iliyopita aliaga dunia Muislamu wa Italia, Mahdi Edoardo Agnelli. Edoardo Agnelli alikuwa mtoto wa kiume wa pekee wa seneta mashuhuri wa Italia na mmiliki wa kiwanda cha magari ya Fiat, Gianni Agnelli. Alizaliwa mwaka 1954 katika mji wa New York nchini Marekani na akahitimu chuo kikuu katika taaluma ya dini na falsafa za Mashariki. Alipokuwa na umri wa miaka 20, Edoardo Agnelli alipata kitabu cha Qur'ani kwa sadfa katika maktaba za Marekani na akaikumbatia dini tukufu ya Uislamu baada ya kufanya uchunguzi kuhusu dini hiyo. Alichagua jina la Hisham Aziz na baadaye kidogo alikhitari kufuata madhehebu ya Ahlulbait na kubadili jina lake na kuwa Mahdi Edoardo Agnelli. Miaka ya awali ya baada ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, Edoardo Agnelli alifanya safari nchini Iran na kukutana na Imam Ruhullah Khomeini. Kusilimu mtoto huyo wa seneta wa Italia, mmiliki wa kiwanda cha magari ya Fiat na klabu ya soka ya Juventus kulitambuliwa kuwa kosa kubwa kwa familia yake kiasi kwamba alitishiwa kuwa atanyimwa urithi kwa kosa hilo. Alikuwa akisema mara kwa mara kwamba anahofia kuuliwa na Wazayuni. Hatimaye tarehe 15 Novemba mwaka 2000 maiti ya Mahdi Edoardo Agnelli ilikutwa chini ya daraja moja la mji wa Turin nchini Italia ikiwa na alama za kupigwa na kujeruhiwa. Maiti yake ilizikwa harakaharaka bila ya kufanyiwa uchunguzi wa kubaini sababu ya kifo chake kilichotokea katika mazingira ya kutatanisha.

Mahdi Edoardo Agnelli.