Jan 30, 2022 02:36 UTC
  • Jumapili, Januari 30, 2022

Leo ni Jumapili tarehe 27 Mfunguo Tisa Jamadithani 1443 Hijria sawa na tarehe 30 Januari 2022 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1052 iliyopita, kwa mujibu wa riwaya mbalimbali aliaga dunia Hussein bin Ahmad Hajjaj mshairi na malenga mashuhuri wa Kishia. Hussein bin Ahmad Hajjaj aliyekuwa malenga mahiri na mwanafsihi mbobezi, aliishi zama moja na Sayyid Murtadha na Sayyid Radhi wanazuoni na wanachuoni wakubwa wa karne ya nne Hijria. Alikuwa mshairi kipenzi wa Ahlul-Baiti (as) na adui mkubwa wa maadui wa dini na ametunga beti nyingi za mashairi katika uwanja huo.  Hussein bin Ahmad Hajjaj aliaga dunia katika eneo lililopo baina ya Baghdad na Kufa na kwa mujibu wa wasia wake, Ibn  Hajja alizikwa upande wa chini wa miguu Imam Mussa al-Kadhim (as) katika mji wa Kadhmein Iraq. ***

Hussein bin Ahmad Hajjaj

 

Siku kama ya leo miaka 116 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, Muhammad Ali Shah Qajar aliomba hifadhi katika ubalozi wa Russia. Kushika kasi na kupanuka wigo wa cheche za Mapinduzi ya Katiba (Constitutional Revolution) katika maeneo mbalimbali ya Iran kulipelekea kuibuka harakati ya kuikomboa Tehran ya wapigania katiba na wakafanikiwa kupata ushindi. Vikosi vya Muhammad Ali Shah Qajar vilishindwa jirani na mji wa Tehran. Hatimaye mji wa Tehran ukadhibitiwa na wapigania Katiba. Muhammad Ali Shah Qajar baada ya kuona kuwa amezidiwa nguvu na wanaharakati hao alikimbilia katika ubalozi wa Russia na kuomba hifadhi. Siku hiyo hiyo kukafanyika kikao cha dharura na Muhammad Ali Shah Qajar akauzuliwa na badala yake mwanawe Ahmad Mirza aliyekuwa na miaka 11 akatangazwa kuwa mfalme.***

Muhammad Ali Shah Qajar

 

Siku kama ya leo miaka 88 iliyopita, kilianza kipindi cha uongozi wa Adolph Hitler, dikteta mbaguzi wa Kinazi wa Ujerumani. Chama cha Taifa cha Kisoshalisti cha Wafanyakazi wa Ujerumani ambacho kiliasisiwa na Hitler kilishinda viti 107 vya bunge katika uchaguzi wa mwaka 1930. Adolph Hitler alijitangaza kuwa kiongozi wa Ujerumani mwaka 1934 baada ya kuwa Kansela na Rais wa nchi hiyo. Hitler aliwafanya mamilioni ya wanadamu kuwa wahanga wa malengo yake ya kibaguzi. Hatua ya Adolph Hitler ya kuivamia Poland mwezi Septemba mwaka 1939 ilichochea Vita vya Pili vya Dunia na hatimaye Ujerumani na waitifaki wake walishindwa katika vita hivyo. Hitler alijiua mwaka 1945 baada ya Ujerumani kushindwa katika vita hivyo. ***

Adolph Hitler,

 

Katika siku kama ya leo miaka 74 iliyopita, kiongozi wa taifa la India na mpigania uhuru wa nchi hiyo Mohandas Karamchand Gandhi aliuawa na kijana mmoja wa Kihindu aliyekuwa na misimamo mikali. Gandhi alizaliwa mwaka 1869 na baada ya kukamilisha masomo alitunukiwa shahada ya digrii katika taaluma ya sheria nchini Uingereza. Mohandas Gandhi kwa muda fulani pia alikuwa kiongozi wa wanamapambano wa Kihindi huko Afrika Kusini. Gandhi pia aliwaongoza wananchi wa India dhidi ya serikali ya kikoloni ya Uingereza katika kupigania ukombozi wa nchi hiyo. India ilipata uhuru mwaka 1947 chini ya uongozi wa Gandhi. ***

Mohandas Karamchand Gandhi

 

Na miaka 37 iliyopita katika siku kama ya leo, Marekani iliafiki suala la kupatiwa mkopo wa dola milioni 47 nchi ya Iraq katika kipindi cha kupamba moto vita vya kichokozi vya dikteta Saddam dhidi ya Iran. Katika kipindi chote cha vita, Marekani iliiunga mkono Iraq kipropaganda na kisilaha na kufanya juhudi za kuupa ari utawala wa Baath. Si hayo tu, bali Marekani ilikuwa ikiipatia pia Iraq taarifa za kiintelijensia na za siri. Aidha wakati wa kujiri vita hivyo, mashirika ya Marekani yaliipatia Iraq teknolojia ambayo iliupa uwezo utawala wa dikteta Saddam wa kutengeneza baadhi ya silaha zikiwemo za kemikali na vijidudu. ***

Silaha za kemikali

 

Tags