Jan 30, 2022 06:50 UTC
  • Mchango wa Maulamaa wa Kishia (38)

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wasikilizaji wapenzi wa Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran popote pale yanapokufikieni matangazo haya, kutoka hapa Tehran.

Karibuni kutegea sikio sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu ili tuweze kupekua ukurasa mwingine katika kurasa za historia ya Maulamaa wa Kishia pamoja na mchango wao katika Uislamu. Kipindi chetu cha juma lililopita kilimzungumzia Sayyid Hashim Bahrani au Allama Bahrani. Alizaliwa katika nusu ya kwanza ya karne ya 11 Hijria katika kijiji cha Gatkan moja ya viunga vya mji wa Tubli ambao kkatika zama hizo, ulikuwa mji mkuu wa kisiasa na kielimu wa Bahrain Allama Bahrani alikuwa na mbinu na mtindo makini na maalumu katika kuandika vitabu vya hadithi na riwaya. Moja ya athari muhimu ya Allama Bahrani ni tafsiri mashuhuri ya Qur'ani Tukufu ya al-Burhan fi Tafsir al-Qur'ani. Kipindi chetu la wiki hii ambacho ni sehemu ya 38 ya mfululizo huu tutamzungumzia Muhammad Taqi Majlisi, baba wa Allama Majlisi, mmoja wa Maulamaa wakubwa na watajika wa Kishia katika karne ya 11 Hijria. 

 Tuliwahi kuashiria katika vipindi vyetu vilivyotangulia kwamba, kudhihiri na kushika hatamu za uongozi ukoo wa Safavi nchini Iran kulipelekea Ushia kutangazwa kuwa madhehebu rasmi ya nchi na kwa utaratibu huo, Mashia kwa kiwango kikubwa wakawa katika hali ya usalama na utulivu huku Maulamaa wa Kishia wakipata fursa nzuri ya kueneza mafundisho ya Ahlul-Baiti (as) sambamba na vikao vya masomo. 

 Msomi huyu alizaliwa katika mji mkubwa na mzuri wa Isfahan uliokuwa mji mkuu wa utawala wa Safavi nchini Iran wakati huo. Baba yake yaani Mullah Ali Majlisi alikuwa akihesabiwa kuwa msomi na mwanazuoni mahiri na aliyetambulika kwa fadhila na adabu na ni mmoja wa wapokezi wa hadithi. Alimpa mwanawe jina la Muhammad Taqi kwa mapenzi na huba kubwa kwa Imam wa Tisa wa Mashia na alianza kumfundisha misingi ya dini na itikadi ya madhehebu ya Ahlul-Baiti (as) tangu akiwa kijana mdogo. Alikuwa akimchukua pamoja naye katika vikao vya Kidini. 

Kutokana na malezi aliyoyapata Muhammad Taqi kutoka kwa baba yake pamoja na kusoma kwa mzazi wake aliondokea na kuchomoza kipaji chake tangu akiwa katika rika la utoto ambapo alipokuwa katika mikusanyiko ya watoto wenzake alikuwa akitoa mawaidha kwa kutumia Aya za Qur’ani na hadithi wakati akiendelea na mchezo. Alikuwa akiwaeleza watoto wenzie kuhusu pepo na moto wa jahanamu na kuwaonya kuhusiana na matendo mabaya. 

Hii inaonyesha kuwa, baba mtu alikuwa amefanikiwa kumjenga mwanawe huyu kinafsi na kuwa na nafsi njema na safi tangu akiwa katika umri wa utoto. Hii nafasi aliyokuwa nayo akiwa bado kijana mdogo na katika rika la utoto, ni jambo lililomfanya Muhammad Taqi awe katika mkondo wa kutumia umri wake katika njia ya kuinua Maktaba ya Ahlul-Baiti (as) na kuondokea kuwa mmoja wa Maulamaa wakubwa na watajika katika Ulimwengu wa Kishia.

 

Baada ya Muhammad Taqi kumaliza masomo ya msingi na ya utangulizi na dini kwa baba yake, alianza kuhudhuria masomo ya walimu wakubwa na waliokuwa mashuhuri katika zama hizo kama mjini Isafahan. Akipata mwongozo wa baba yake, alikuwa akihudhuria darsa na masomo yaliyokuwa yakifundishwa na Allama Maula Abdallah Shushtari mmoja wa Maulamaa wakubwa wa Hawza ya Najaf ambaye alikuwa amehajiri na kuelekea Isfahan. Kwa miaka mingi Muhammad Taqi alikuwa pamoja na mwalimu huyu na kusoma kwake elimu za fikihi, hadithi, Usulul-fikihi, teolojia na tafsiri ya Qur’ani. Baada ya mwalimu wake huyo kuaga dunia, Muhammad Taqi alifahamiana na Sheikh Bahai msomi na mwanazuoni mkubwa wa fikihi na arif mahiri na kuanza kuhudhuria masomo yake. Muhammad Taqi alianza safari yake ndefu ya Kiirfani kwa mwalimu huyu mahiri wa falsafa.

Muhammad Taqi au Majlisi awali alikuwa na mapenzi maalumu na elimu ya irfan na baada ya kufahamiana na Sheikh Bahai akawa amepata kile alichokuwa akikitafuta. Mbali na kwa Sheikh Bahai, Muhammad Taqi Majlisi alikuwa akihudhuria pia darsa za wasomi na wanazuoni wengine kama Qadhi Abu al-Surur, Amir Is’haq Astarabadi, Sheikh Abdallah bin Jabir Amili na Mulla Muhammad Qassim Amili .

Mwaka 1034 Hijria wakati Muhammad Taqi Majlisi akiwa na umri wa miaka 31 huku ikitarajiwa kuwa angeanza kufanya kazi ya kufundisha katika Hawza na Chuo Kikuu cha Isfahan, alihajiri na kuelekea Najaf Iraq.

 

 

Allama Majlisi ameandika na kutunga vitabu vingi ambavyo ni turathi na urithi kwa vizazi vilivyokuja baada yake. Hadithi na riwaya ni miongoni mwa maudhui mashuhuri vya utunzi na uandishi wake wa vitabu. Kitabu mashuhuri zaidi cha Muhammad Taqi Majlisi ni Raudhat al-Mutaqin. Kitabu hiki kimechapishwa mara nyingi.

Vitabu vingine vya alimu huyu ni Sahifeh Sajadiyeh ambacho kinajumuisha dua 54 kutoka kwa Imam Ali bin Hussein Zeinul Abidin. Muhammad Taqi Majlisi alitumia sehemu kubwa ya umri wake kwa ajili ya kueneza mafundisho ya Ahlul-Baiti (as).

 

Mulla Muhammad Taqi Majlisi aliaga dunia tarehe 11 Shaaban mwaka 1070. Alifariki dunia katika mji wa Isafahan na kuzikwa katika mji huo huo. Kifo chake kilikuwa pigo kubwa kwa vyuo vya kidini hususan chuo cha Isfahan. Hii ni kutokana na kuwa, Isfahan ilikuwa imepoteza mmoja wa walimu bora kabisa wa hadithi.

Na hadi hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia tamati ya kipindi chetu kwa juma hili, tukutane tena wiki ijayo katika sehemu nyingine ya mfululizo huu wa Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu.

Wassalaamu Alaykum Warahhmatullahi Wabarakaatuh