Jumatano tarehe Pili Februari 2022
Leo ni tarehe 30 Jamadithania 1443 Hijria inayosadifiana na Februari Pili mwaka 2022.
Miaka 230 iliyopita katika siku kama ya leo, mkataba wa kihistoria wa Berlin, ulitiwa saini baina ya Leopold II mfalme wa wakati huo wa Austria na Frederick William aliyekuwa mfalme wa Prussia. Mkataba huo ulikuwa natija ya maafikiano baina ya viongozi hao wawili yaliyofikiwa tarehe Pili Agosti mwaka 1791 huko Pillnitz kwa ajili ya kukabiliana na mapinduzi ya Ufaransa. Hii ilitokana na kuwa, watawala wa Ulaya walikuwa wameingiwa na woga mkubwa kutokana na baadhi ya nadharia za wapigania uhuru wa Ufaransa. Licha ya kuweko mkataba huo na hata mashambulio ya pamoja ya Austria, Prussia na Uingereza dhidi ya Ufaransa na himaya yao kwa wapigania mfumo wa utawala wa Kifalme wa nchi hiyo, harakati hizo hazikuwa na natija kwani hatimaye wanamapinduzi wa Ufaransa waliibuka na ushindi.
Katika siku kama ya leo miaka 115 iliyopita, Dmitri Ivanovich Mendeleev msomi na mwanakemia wa Kirusi alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 73 huko Saint Petersburg uliokuwa mji mkuu wa Russia wakati huo. Dmitri alizaliwa mwaka 1834 na kusoma taaluma ya kemia. Msomi huyo alifanya utafiti na uhakiki mwingi muhimu katika taaluma ya kemia ambapo baadaye ulikuja kujulikana kwa jina la jedwali la Mendeleev.
Siku kama ya leo miaka 102 iliyopita alizaliwa Ayatullah Murtadha Mutahhari, msomi na mwanafikra mkubwa wa Kiislamu wa zama hizi. Alizaliwa katika eneo la Fariman tarehe 13 Bahman, 1298 Hijiria Shamsia, na baada ya kupata elimu ya msingi alijiunga na chuo kikuu cha kidini cha Qum nchini Iran na kuhudhuria darsa za wasomi wakubwa kama Ayatullahil Udhma Boroujerdi, Allameh Tabatabai na Imam Ruhullah Khomeini. Katika kipindi cha kutafuta elimu ya juu, Shahidi Murtadhaa Mutahhari alifanya jitihada kubwa za kutakasa nafsi na kuruzukiwa kipaji cha aina yake katika masuala ya elimu.
Mwanzoni mwa harakati ya Kiislamu ya Iran mnamo 1341 na 1342, Shahidi Mutahhari alijiunga na safu ya harakati hiyo na kilele cha harakati zake kilikuwa tarehe 5 Juni 1963, wakati alipokamatwa na kufungwa na shirika la ujasusi la Shah, SAVAK. Baada ya kuachiwa huru aliendeleza mapambano kwa kuunda makundi ya wanaharakati na kulinda harakati hiyo ya mapinduzi ya kiislamu. Aliendeleza harakati zake kupitia njia ya kuwazindua vijana na matabaka mengine ya jamii kupitia kumbi na majukwaa mbalimbali hususan misikiti na vituo vya kidini. Alikamatwa tena na kufungwa na utawala wa Shah na kupigwa marufuku kuhutubia umma. Wakati wa kukaribia ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Shahidi Mutahhari alikuwa mmoja kati ya shakhsia muhimu wa kidini, kielimu na kisiasa katika harakati ya Kiislamu. Imam Khomeini, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alimteua Shahid Mutahhari kuwa mwanachama na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ya Kiislamu. Ayatullah Murtadha Mutahhari ameandika karibu vitabu 80 katika nyanja mbalimbali.
Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, ambayo ilikuwa muungaji mkono mkubwa wa utawala wa kidhalimu wa Shah nchini Iran, iliitambua hotuba ya hamasa iliyotolewa na hayati Imam Khomeini MA mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu katika makaburi ya Beheshti Zahra mnamo tarehe 12 Bahman, baada ya kurejea kwake nchini kuwa, ilikuwa dhidi ya Marekani. Katika hotuba hiyo Imam Khomeini alibainisha misimamo yake mkabala wa siasa za kibeberu na uingiliaji wa Marekani katika masuala ya Iran. Kwa upande wake utawala wa Kizayuni wa Israel ulielezea wasiwasi wake kuhusu kurejea Imam Khomeini nchini Iran kwa sababu ulitambua kwamba, Imam na wananchi Waislamu wa Iran ni wapinzani wakubwa wa utawala huo ghasibu na vamizi. Aidha shirika la habari la Russia, Itar-Tass liliripoti kuwa kurejea Ayatullah Ruhullah Khomeini nchini Iran, kumeyafanya mapambano ya wananchi wa nchi hiyo kuingia katika hatua yenye kuainisha mustakbali.