Jumatatu tarehe 21 Februari 2022
Leo ni Jumatatu tarehe 19 Rajab 1443 Hijria sawa na Februari 21 mwaka 2022.
Siku kama ya leo miaka 1434 vilitokea vita vya Tabuk baina ya Waislamu na jeshi la Roma. Vita vya Tabuk ni miongoni mwa vita vya mwisho vya Mtume Muhammad (saw). Sababu ya kutokea vita hivyo ni kwamba, msafara wa kibiashara wa Sham ulimtaarifu Mtume (saw) kwamba mfalme wa Roma ametayarisha jeshi na kulituma Madina. Kwa msingi huo Mtume Muhammad (saw) aliwaanuru Waislamu kujitayarisha kwa ajili ya kukabiliana na jeshi la mfalme wa Roma. Waislamu wengi walijitayarisha kwa ajili ya vita hivyo licha ya masafa marefu, msimu wa joto kali, mashaka ya safari hiyo ngumu na kuwadia msimu wa mavuno. Hatimaye jeshi na wapiganaji elfu 30 la Waislamu liliwasili eneo la vita lakini halikukuta jeshi la mfalme wa Roma eneo hilo.
Japokuwa hakukutokea mapigano wakati huo, lakini tukio hilo lilidhihirisha nguvu ya Waislamu, utayarifu wao wa kukabiliana na majeshi vamizi na moyo wao wa kujitolea kwa ajili ya Allah. Vita hivyo vya Tabuk pia vinajulikana kwa jina la "al Fadhiha" kwa maana ya mfedheheshaji kutokana na kwamba, vililifedhehesha kundi la Waislamu wanafiki waliokataa kujiunga na msafara huo kwa ajili ya kukabiliana na jeshi la Roma.

Miaka 969 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 19 Rajab mwaka 474 Hijria Qamaria Abul Walid Sulaiman bin Khalaf Maliki, faqihi maarufu wa karne ya Tano Hijria Qamaria aliaga dunia huko Andalusia ambayo leo inajulikana kama Uhispania. Alikuwa hafidh na mfasiri wa Qur'ani Tukufu mbali na kubobea katika fasihi na mashairi. Abul Walid awali alifunza Fiqhi na taaluma ya Hadithi za Mtume SAW huko Andalusia na kisha akaendelea kufundisha huko Makka na Baghdad. Kati ya vitabu alivyoandika ni, "Tafsirul Qur'an", "An-Nasikhu wal-Mansukh" na Al-Isharah."

Siku kama ya leo miaka 202 iliyopita, alizaliwa Reinhart Dozy, mtaalamu wa masuala ya mashariki mwa dunia aliyekuwa raia wa Uholanzi. Dozy alizamili katika fani za historia na lugha huku akifikia daraja ya PHD katika fani ya fasihi akiwa na umri wa miaka 24. Reinhart Dozy alipendelea sana kusomea tamaduni za Kiislamu ambapo mbali na kuwa mahiri katika lugha ya Kiingereza, Kifaransa na Kijerumani, alikuwa pia mtaalamu katika lugha ya Kiarabu. Msomi huyo wa Uholanzi alifanya utafiti mwingi wa tamaduni za Kiarabu na historia ya Kiislamu, hususan Waislamu wa Andalusia, kusini mwa Uhispania. Miongoni mwa athari za msomi huyo ni pamoja na kitabu cha 'Historia ya kisiasa na tamaduni za Kiarabu katika Andalusia' 'Historia ya Uislamu kuanzia mwanzo wake hadi katikati ya karne ya 19' na 'Tamaduni za mavazi ya Kiislamu.' Reinhart Dozy alifariki dunia mwaka 1883.
Siku kama ya leo miaka 106 iliyopita, inayosadifiana na 21 Februari 1916 vilianza vita vikubwa vya umwagikaji damu vilivyojulikana kwa jina la 'Verdun' kati ya Ujerumani na Ufaransa. Vita hivyo vilivyoendelea kwa muda wa miezi kumi vilimalizika kwa kushindwa vikosi vya jeshi la Ujerumani na wanajeshi karibu milioni moja wa nchi hizo mbili kuuawa. Tukio hilo ni miongoni mwa sababu za kushindwa Ujerumani kwenye Vita vya Kwanza vya Dunia.
Siku kama ya leo miaka 64 iliyopita, wananchi wa Misri na Syria walishiriki kwenye kura ya maoni ya kuunganisha nchi mbili hizo chini ya Jamhuri ya Muungano wa Kiarabu. Wananchi wa nchi hizo mbili walimchagua Jamal Abdul-Nasser kiongozi wa wakati huo wa Misri, kuwa rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Kiarabu. Baada ya kupita miezi kadhaa, Yemen nayo ilijiunga kwenye muungano huo. Hata hivyo muungano huo haukudumu kwa zaidi ya miaka mitatu, kwani Syria ilitangaza kujitoa kwenye muungano huo kutokana na kutoridhishwa na uongozi wa Jamal Abdul-Nasser.

Katika siku kama ya leo 57 iliyopita, Malcolm X, Mmarekani mweusi aliuawa baada ya kushambuliwa na magaidi nchini humo. Malcolm X alizaliwa mwaka 1925, na wakati alipokuwa kwenye rika la ujana alifahamiana na makundi ya vijana wa Kiislamu na hatimaye kusilimu. Itikadi za mwanaharakati huyo wa Kiislamu ziliwachukiza watawala wa Marekani na makundi ya ubaguzi wa rangi nchini humo. Malcolm X aliuawa akihutubia mkutano. Alikuwa akisisitiza mara kwa mara kuwa, Wamarekani weusi ambao wanakandamizwa na kubaguliwa na serikali ya Marekani wanaweza kujipatia uhuru na uadilifu chini ya mwavuli wa utawala wa Kiislamu.
Na miaka 22 iliyopita kwa mara ya kwanza "Siku ya Kimataifa ya Lugha ya Mama" iliadhimishwa. Uamuzi wa kuitangaza siku hii kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Lugha ya Mama ulichukuliwa Novemba 1999 na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) ambapo mwaka 2008 ulipewa pia jina la 'Mwaka wa Kimataifa wa Lugha". Sisitizo la kulinda na kuimarisha lugha ya mama linatokana na kuwa, takribani nusu ya lugha 6,000 zinazotambulika duniani zimo katika hatari ya kutokomea kutokana na sababu mbalimbali hususan uingiaji na utwishaji wa lugha za kimataifa kwa kutumia mbinu mbalimbali.
