Jumanne tarehe 22 Februari 2021
Leo ni Jumanne tarehe 20 Rajab 1443 Hijria sawa na Februari 22 mwaka 2022.
Miaka 1430 iliyopita katika siku kama hii ya leo, vilitokea vita vya Yarmuk kati ya jeshi la Kiislamu na jeshi la utawala wa kifalme wa Roma ya Mashariki katika bonde lililojulikana kwa jina hilo huko Palestina. Ushindi wa Waislamu huko Sham, yaani Syria ya sasa ulimpelekea mfalme wa Roma kuandaa jeshi kubwa kwa ajili ya kupigana na Waislamu. Lakini, Waislamu waliweza kutoa pigo kwa wanajeshi wa mfalme wa Roma licha ya kuwa na idadi ndogo ya wapiganaji na suhula chache za kivita. Kufuatia ushindi huo Waislamu walisonga mbele na kufika eneo la Mashariki la Ufalme wa Roma na mwaka mmoja baada ya hapo Waislamu wakafanikiwa kuchukua udhibiti wa mji wa Baitul Muqaddas pasina umwagaji damu.

Siku kama hii ya leo miaka 64 iliyopita aliaga dunia Abul Kalaam Ahmad Azad, aalim, khatibu hodari na mwanasiasa wa India akiwa na umri wa miaka 70. Abul Kalaam Azad alianzisha harakati za kisiasa dhidi ya ukoloni wa Uingereza na kwa lengo la kuwaamsha Waislamu wa India akiwa na umri wa miaka 17. Mwanasiasa huyo aliwekwa gerezani mara kadhaa kutokana na kuchapisha makala na kutoa hotuba zenye kufichua njama za wakoloni wa Kiingereza.
Miaka 38 iliyopita katika siku kama ya leo oparesheni ya kijeshi ya "Khaibar" ilianza wakati wa vita vya kulazimishwa vya miaka minane vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran. Oparesheni hiyo ilitekelezwa na wapiganaji jasiri wa Iran. Oparesheni hiyo ambayo ilianza kutekelezwa katika eneo la Hurul Huwaizah huko kusini magharibi mwa Iran, wapiganaji wa Kiirani walivuka maji na vinasamasi na kukiteka nyara kisiwa chenye utajiri wa mafuta cha Majnuun karibu na mji wa Basra kusini mashariki mwa Iraq. Mbinu tata za kijeshi zilizotumika katika oparesheni hiyo ya majini na nchi kavu ya Khaibar ziliwashangaza weledi wa masuala ya kijeshi duniani.
Siku kama ya leo miaka 16 iliyopita miripuko mikubwa ya mabomu ilitokea katika haram mbili tukufu za Maimamu Hadi na Hassan al Askari (as) huko katika mji wa Samarra, kaskazini mwa Baghdad mji mkuu wa Iraq na kusababisha hasara kubwa katika eneo hilo tukufu la Waislamu. Uharibifu mkubwa uliosababishwa na miripuko hiyo katika haram hizo tukufu uliwakasirisha Waislamu duniani na hasa wa wafuasi wa madhehebu ya Shia. Maimamu hao wawili ni miongoni mwa wajukuu wa Mtume wa Mwenyezi Mungu Muhammad (saw).
