Jumanne, Machi 22, 2022
Leo ni Jumanne tarehe 19 Shaabani 1443 Hijria sawa na Machi 22 Mwaka 2022 Milaadia.
Miaka 1437 iliyopita katika siku inayosadifiana na hii ya leo, vilitokea vita vya Bani Mustalaq. Bani Mustalaq lilikuwa kabila miongoni mwa makabila ya Khaza'ah ambalo lilihamia katika vitongoji vya Makka miaka mingi iliyopita. Viongozi wa kaumu hiyo walikuwa wakiabudu na kueneza ibada ya masanamu huko Makka. Bani Mustalaq walijiandaa kupigana vita na Waislamu baada ya Uislamu kushika madaraka huko Madina. Kwa msingi huo, Mtume Muhammad (saw)aliingia vitani pamoja na wafuasi wake kadhaa na kutoa pigo kubwa kwa kabila hilo.

Siku kama ya leo miaka 141 iliyopita ulianzishwa Muungano wa Soka wa Kimataifa kwa shabaha ya kusimamia mashindano ya mpira wa miguu kote duniani. Kabla ya kuundwa muungano huo, mashindano ya soka yalikuwa yakifanyika katika nchi mbalimbali kwa muundo usiokuwa rasmi. Muungano huo ulibadilisha muundo wake na kujulikana baadaye kwa jina la Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) na liliandaa pambano rasmi la kwanza la kimataifa mwaka 1901, kati ya Uingereza na Ujerumani.

Miaka 77 iliyopita sawa na tarehe 22 mwezi Machi mwaka 1945 Jumuiya ya Nchi za Kiarabu iliundwa huko Cairo mji mkuu wa Misri kufuatia pendekezo la mfalme Farouq, mtawala wa kifalme wa wakati huo wa Misri kwa kutiwa saini makubaliano kati ya serikali za Syria, Iraq, Saudi Arabia, Misri na Yemen. Mpango wa kuundwa jumuiya hiyo ulipasishwa katika kikao kilichofanyika katika bandari ya Alexandria huko Misri.

Katika siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, ilianza operesheni kubwa ya 'Fat-hul Mubiin' ya wapiganaji shujaa wa Kiislamu huko kusini magharibi mwa Iran kwa shabaha ya kuyarejesha nyuma majeshi vamizi ya Iraq. Kwenye operesheni hiyo iliyopelekea kukombolewa miji ya Dezful, Andimeshk, Shush na mamia ya vijiji vya eneo hilo, wanajeshi wasiopungua elfu 25 wa Iraq waliuawa na wengine elfu 15 kukamatwa mateka.

Siku kama ya leo miaka 18 iliyopita aliuawa shahidi Sheikh Ahmad Yassin mwanachuoni na mwasisi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) pamoja na watu wengine 10. Sheikh Ahmad Yassin aliuawa shahidi baada ya kumaliza Swala ya Alfajiri katika msikiti mmoja ulioko eneo la Ukanda wa Gaza, wakati aliposhambuliwa na helikopta za utawala wa Kizayuni wa Israel. Sheikh Ahmad Yasin aliasisi harakati ya Hamas mwaka 1987 akishirikiana na wanamapambano wengine kadhaa wa Kipalestina na miaka miwili baadaye alifungwa jela na utawala ghasibu wa Israel. Mauaji ya mpigania uhuru huyo ambaye alikuwa kiwete na kipofu wakati wa kuuawa kwake, yalidhihirisha tena ugaidi wa kiserikali wa utawala haramu wa Israel.

Leo tarehe 22 Machi ni Siku ya Maji Duniani. Ongezeko la jamii ya wanadamu, kuongezeka kwa matumizi ya maji, kukatwa ovyo miti ya misitu na mabadiliko ya hali ya hewa, kupanuka kwa miji na kuongezeka kwa viwanda vinavyochafua mazingira na vyanzo vya maji, mbinu zisizofaa za kilimo na kadhalika vimechangia uhaba wa maji, suala ambalo linatishia jamii ya mwanadamu. Kwa msingi huo na ili kuwazindua walimwengu kuhusu umuhimu wa maji, mkutano uliofanyika mwaka 1992 katika mji wa Rio de Janeiro nchini Brazil uliitangaza tarehe 22 Machi kuwa Siku ya Kimataifa ya Maji na suala hilo likapasishwa rasmi katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
