May 17, 2022 02:29 UTC
  • Jumanne tarehe 17 Mei mwaka 2022

Leo ni Jumanne tarehe 15 Shawwal 1443 Hijria sawa na Mei 17 mwaka 2022.

Katika siku kama ya leo miaka 1440 ilyopita alizaliwa Abu Tufail A'mir bin Wathilah Kinani ambaye alikuwa miongoni mwa washairi na mahatibu mashuhuri za zama za awali za Uislamu. Abu Tufail alikuwa miongoni mwa masahaba wa Mtume Muhammad (saw) na alisuhubiana kwa muda mrefu na Imam Ali bin Abi Twalib (as) na kushiriki katika vita vya Siffin, Jamal na Nahrawan pamoja na mtukufu huyo. Abu Tufail alifaidika sana na elimu na maarifa ya mtukufu huyo. Mashari mengi ya A'mir bin Wathilah yanamsifu Mtume Muhammad (saw). 

Siku kama ya leo miaka 1191 iliyopita inayosadifiana na tarehe 15 Mfunguo Mosi Shawwal mwaka 252 Hijria, alifariki dunia Abdul-Adhim al Hassani. Mtukufu huyu ni miongoni mwa wajukuu wa Mtume Muhammad (saw) kupitia shajara ya Imam Hassan Al-Mujtaba (as). Abdul-Adhim al Hassani alikuwa mashuhuri sana kwa karama zake nyingi. Maimamu watukufu katika kizazi cha Mtume walithibitisha ukweli na uchamungu wake na walikuwa wakinukuu Hadithi kutoka kwake. Baada ya kushadidi dhulma na ukandamizaji wa utawala wa Bani Abbas, Abdul-Adhim al Hassani alilazimika kuhajiri na kuhamia Rey kusini mwa Tehran ya leo. Mtukufu huyo anajulikana pia kama shahidi ambaye aliuawa kwa kupewa sumu. Haram Tukufu ya Abdul-Adhim Hassani ipo katika eneo la Rey na wapezi wa Ahlul Bait (as) kutoka kona mbalimbali za dunia humiminika katika eneo hilo kwa ajili ya kwenda kufanya ziara.

Haram ya Abdul-Adhim al Hassani

Miaka 273 iliyopita, katika siku kama hii ya leo alizaliwa Edward Jenner, tabibu wa Kiingereza aliyegundua chanjo ya ndui yaani (small pox). Tabibu huyo alifanikiwa kugundua chanjo ya ndui tarehe 14 Mei mwaka 1796 akiwa na umri wa miaka 45 wakati alipoelekea nchini India. Baada ya hapo ugonjwa huo wa ndui ulitibiwa kwa kutumia chanjo hiyo. Maradhi hayo ambayo wakati huo yalikuwa yakichukua roho za watu bila ya huruma, yalitokomezwa kabisa duniani mwaka 1979.

Edward Jenner

Siku kama ya leo miaka 195 iliyopita aliaga dunia mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu Seikh Muhammad Taqi Razi katika mji wa Isfahan nchini Iran. Sheikh Taqi Razi maarufu kwa jila la Agha Najafi, alielekea katika mji mtakatifu wa Najaf kwa ajili ya elimu ya juu ya kidini baada ya kukamilisha elimu ya msingi. Alipata elimu kwa wanazuoni mashuhuri kama Mirza Muhammad Hassan Shirazi na Sheikh Mahdi Kashiful Ghitaa. Baada ya kurejea Isfahan, Sheikh Agha Najafi alikuwa marejeo ya Waislamu katika masuala ya kidini na kisheria. Alikuwa mstari wa mbele kupambana na wakoloni kupitia harakati iliyopewa jina la Harakati ya Tumbaku. Vitabu mashuhuri vya mwanazuoni huyo ni pamoja na "Anwarul Arifin", "Asrarul Ayat" na "Al-Ijtihad Wattaqlid".

Miaka 157 iliyopita katika siku kama ya leo, kulitiwa saini mkataba wa kwanza wa kimataifa katika uwanja wa mwasiliano huko Paris Ufaransa. Utiaji saini huo ulihudhuriwa na wawakilishi kutoka nchi 20 duniani. Kwa utaratibu huo kukawa kumepasishwa hati ya kuasisiwa Muungano wa Kimataifa wa Telegrafu. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana siku hii ikapewa jina la Siku ya Kimataifa ya Mawasiliano. Mwaka 1932 kwa mujibu wa maamuzi yaliyofikiwa katika mkutano wa Madrid Uhispania, jina la Muungano wa Kimataifa wa Telegrafu au Internatioanl Telegraph Union lilibadilishwa na kuwa, Umoja wa Kimataifa wa Mawasiliano au  International Telecomunication Union (ITU) na vipengee pamoja na sheria za jumuiya hiyo zikapitiwa upya. Kuanzia mwaka 1947, taasisi hiyo ikawekwa rasmi katika faharasa ya asasi zilizoko chini ya Umoja wa Mataifa.

Katika siku kama ya leo miaka 83 iliyopita, dola la Uingereza ambalo Palestina ilikuwa chini ya mamlaka yake, lilitoa kitabu kilichopewa jina la "Kitabu Cheupe" (The White Paper) na hivyo kukawa kumepigwa hatua nyingine katika njia ya kuasisiwa utawala ghasibu wa Israel. Wapalestina ambao walikuwa wakifahamu vyema himaya ya Uingereza kwa Wazayuni, waliukataa mpango uliokuwa umependekezwa katika kitabu hicho kwa ajili ya kuipatia ufumbuzi kadhia ya Palestina.

Askari wa utawala haramu wa Israel

Miaka 35 iliyopita katika siku kama ya leo, wakati wa vita vya kulazimishwa vya majeshi ya Iraq dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ndege za kivita za Iraq ziliishambulia manowari ya kivita ya Marekani iitwayo Stark katika eneo la Ghuba ya Uajemi, na kupelekea wanajeshi 37 wa Kimarekani kuuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa. Baada ya tukio hilo, utawala wa Saddam uliomba radhi kwa serikali ya Marekani na kutangaza kuwa tayari kulipa fidia za uharibifu huo.

Manowari ya kivita ya Marekani, Stark

Siku kama ya leo miaka 13 iliyopita, alifariki dunia Ayatuhil Udhma Muhammad Taqi Behjat Foumani, mmoja wa Marajii Taqlidi na maurafaa wakubwa wa Kiislamu. Alizaliwa mwaka 1294 Hijria Shamsia katika mji wa Fouman ulioko katika mkoa wa Gilan kaskazini mwa Iran. Baada ya kupata elimu ya msingi ya kidini, mwaka 1308 Hijria Shamsia alielekea katika Chuo Kikuu cha Kidini cha Najaf nchini Iraq. Ayatullah Bahjat alikuwa mashuhuri sana kutokana na uchamungu wake. Kitabus Swalat, Jamiul Masail na Wasilatun Najat ni baadhi ya vitabu mashuhuri vya msomi huyo.

Ayatuhil Udhma Muhammad Taqi Behjat Foumani