Jun 14, 2022 01:15 UTC
  • Jumanne, Juni 14, 2022

Leo ni Jumanne mwezi 14 Mfunguo Pili Dhulqaad, 1443 Hijiria inayosadifiana na 14 Juni 2022 Milaadia.

Katika siku kama ya leo miaka 286 iliyopita alizaliwa mwanafikizia wa Kifaransa kwa jina la Charles Augustin de Coulomb. Msomi huyo alianza kufundisha masomo katika nyanja za umeme na sumaku baada ya kuhitimu masomo yake na kuandika vitabu vingi katika uwanja huo. Mbali na kufundisha, mwanafizikia Augustin de Coulomb aliendelea pia kufanya utafiti na hatimaye akafanikiwa kubuni kanuni katika sayansi ya fizikia iliyojulikana kwa jina lake. De Coulomb aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 70.

Charles Augustin de Coulomb

 

Siku kama ya leo miaka 202 iliyopita, wanajeshi wa Misri wakiongozwa na Kamanda Muhammad Ali Pasha waliishambulia Sudan na kulikalia kwa mabavu eneo kubwa la ardhi ya kaskazini mwa nchi hiyo. Wakati huo huo Waingereza pia walilishambulia eneo la kusini mwa Sudan na kulikalia kwa mabavu. Hata hivyo wananchi wa Sudan wakiongozwa na Mahdi al Sudani mwaka 1881 walianzisha harakati ya ukombozi dhidi ya uvamizi wa Misri na Uingereza na mwaka 1885 wakafanikiwa kutoa pigo kubwa kwa vikosi vamizi vya Misri na Uingereza na hivyo kuyakomboa maeneo hayo.

Bendera ya Sudan

Siku kama ya leo miaka 192 iliyopita wanajeshi wa Ufaransa waliwasili katika pwani ya Algeria huko kaskazini mwa Afrika. Uvamizi huo ulikuwa mwanzo wa oparesheni za kijeshi za Ufaransa zilizokuwa na lengo la kuikalia kwa mabavu na kuikoloni Algeria. Hata hivyo uvamizi huo wa kikoloni wa Ufaransa nchini Algeria ulikabiliwa na mapambano makubwa ya wananchi dhidi ya maghasibu wa Kifaransa. Mapambano hayo ya kupigania ukombozi ya wananchi wa Algeria dhidi ya ukoloni wa Ufaransa yalipamba moto baada ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia. Hatimaye mwaka 1962 Rais wa wakati huo wa Ufaransa alilazimika kuipatia Algeria uhuru kamili kufuatia mashinikizo ya mapambano ya wananchi wa Algeria na upinzani wa fikra za waliowengi ndani ya Ufaransa kwenyewe na kimataifa.

Algeria

Siku kama ya leo miaka 92 iliyopita mto mrefu na mkubwa zaidi wa Asia wa Yangtze Kiang ulivunja kingo zake na kusababisha mafuriko ya kutisha. Mvua kali za msimu zilizonyesha zilisababisha mawimbi na mafuriko makubwa yaliyovunja kingo na mabwawa yote ya kandokando ya mto huo. Maji hayo yaligubika ardhi ya majimbo 8 ya China. Inasemekana kuwa tukio hilo kubwa liliathiri karibu watu milioni 50 wakiwemo waliopoteza maisha, kupoteza makazi, uharibifu wa mashamba, wale waliofariki dunia kutokana na maradhi ya aina mbalimbali na kadhalika. 

Yangtze Kiang

Tarehe 24 Khordad miaka 41 iliyopita wawakilishi 120 wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) waliwasilisha muswada wa kutokuwa na imani na Bani Sadr aliyekuwa rais wa wakati huo wa Iran. Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya kusambaratika mapambano ya wananchi dhidi ya wavamizi wa chama cha Baath kutoka Iraq katika hujuma iliyofanywa dhidi ya ardhi ya Iran kutokana na kukosa misaada ya dharura kutoka kwa Bani Sadr aliyekuwa Kamanda na Amri jeshi Mkuu, na vilevile hitilafu zilizojitokeza baina ya Rais wa nchi na mihimili mingine miwili ya dola.