Jun 22, 2022 06:56 UTC
  • Sibtain katika Qur'ani na Hadithi 9

Assalaam Alaykum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran.

Tunakukaribisheni mjiunge nasi kusikiliza sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi, ambayo bila shaka itatunufaisha sote kwa pamoja. Ni wazi kuwa Uislamu hauishii tu katika mijadala ya kiakili na kimantiki hata kama mambo haya yote ni ya msingi katika njia ya imani, bali masuala ya kiroho, nafsi, hisia na maadili ni masuala yaliyo na umuhimu mkubwa katika maisha ya mwanadamu. Mapenzi ni jambo muhimu sana na la msingi katika maisha ya kihoro. Hivyo ni wazi kuwa mtaafikiana nasi wapenzi wasikilizaji tukisema kuwa mapenzi yanapaswa kuelekezwa kwa Mwenyezi Mungu, mtu anayempenda Mungu na Mungu naye akawa anamridhia mtu huyo.

Mapenzi haya yaliinuliwa na kufikia daraja ya juu zaidi kiwango cha kufanywa kuwa ni thawabu na sehemu muhimu katika ujumbe wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, Muhammad al-Mustafa (saw). Hilo hutimia iwapo mapenzi hayo yatadhihirishwa kwa ikhlasi kuwahusu Ahlu Bait wa Mtume (saw) na kwa lengo la kupata ridhaa ya Mwenyezi Mungu. Ahlu Bait hao (as) ni watu maalumu katika Nyumba ya Mtume Mtukufu (saw) ambao Mwenyezi Mungu amewazungumzia katika kitabu chake kitakatifu kwa kusema: Sema: Kwa haya sikuombeni malipo yoyote kwenu ila mapenzi katika ndugu.

***************

Wapenzi wasikilizaji, huenda mulizaji akauliza swali kwamba: Je, ni ndugu gani hawa ambao Mwenyezi Mungu ametaka waja wake wawapende na kuwajibisha mapenzi kwao? Ni ndugu gani hawa ambao Mwenyezi Mungu amemtaka Mbora wa viumbe wake Mtume Mtukufu (saw) awatake wafuasi wa dini ya mbinguni iliyokamilika zaidi wawapende na kuahidi  kuwalipa malipo mema na makubwa zaidi kutokana na jambo hilo?

Tunajibu swali hili kwa njia mbili. Ya kwanza ni kwamba Waislamu wote wameafikiana kwamba Riwaya zinazozungumzia suala hili zinathibitisha kwamba makusudio ya ndugu hawa ni jamaa na watu wa karibu ya Mtume Mtukufu (saw). Miongoni mwa Riwaya hizo ni ile iliyonukuliwa na al-Kanji as-Shafii' katika kitabu chake cha Kifayat at-Talin ambayo imenukuliwa na sahaba mashuhuri na mwaminifu Jabir bin Abdillah al-Ansari kwamba alisema: 'Mwarabu mmoja wa jangwani (bedui) alifika mbele ya Mtume (saw) na kumwambia: Ewe Muhammad! Nifahamishe Uislamu ni nini. Mtume (saw) akasema: Uislamu ni kutamka kwamba: Ninashuhudia ya kwamba hakuna Mungu isipokuwa Allah Mmoja tu asiyekuwa na mshirika na kwamba Muhammad ni mja na Mtume wake. Mwarabu huyo akauliza tena: Je, utanitoza malipo juu ya hili? Mtume (saw) akamjibu: La, isipokuwa mapenzi katika ndugu (watu wa karibu). Mwarabu akauliza: Ndugu zangu au ndugu zako? Mtume (saw) akasema: Ndugu zangu. Mwarabu akasema: Wacha nikupe baia, Mwenyezi Mungu amlaani mtu asiyekupenda na asiyewapenda ndugu zako (watu wa karibu yako)."

Njia ya pili wapenzi wasikilizaji ni ile ambayo maulama na wanazuoni wote wa Kiislamu wanakubaliana nayo. Tabari anasema katika tafsiri yake ya Jamiul Bayaan katika kufafanua Aya ya Qurba au al-Mawadda kwamba Abu Is'haq alisema: 'Nilimuuliza Umratu bin Shuaib kuhusu kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu inayosema: 'Sema: Kwa haya sikuombeni malipo yoyote kwenu ila mapenzi katika ndugu, naye akaseme: Wao ni ndugu (watu wa karibu) wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw).

Na katika kuifasiri Aya hii, As-Shaukani anaandika katika kitabu chake cha Fat'h al-Ghadir: Baada ya Mwenyezi Mungu kubainisha kile alichomfahamisha Mtume wake (saw) katika sheria tukufu za dini kupitia kitabu chake kitakatifu, alimuamuru awaambie watu kwamba hakutaka malipo yoyote kutokana na mafundisho ya dini na ulinganiaji aliowafanyia isipokuwa awaambie: Kwa haya sikuombeni malipo yoyote kwenu ila mapenzi katika ndugu. Yaani sema, ewe Muhammad! Sikuombeni malipo yoyote kutokana na ulinganiaji huu wa ujumbe wa Mwenyezi Mungu isipokuwa kuwapenda watu wa karibu yangu.'

***********

Na sasa wapenzi wasikilizaji, hebu na tubainishe maana halisi ya neno 'ndugu' lililotumika katika Aya hii ili tupate kujua kwamba je, ndugu hao ni ndugu na watu wote wa karibu ya Mtume (saw) au ni watu maalumu katika ndugu hao? Na jibu la swali hili ndugu wasikilizaji pia linatimia kwa njia mbili. Ya kwanza ni kupitia Riwaya ikiwemo hii ambayo imenukuliwa na Muhib ad-Deen at-Tabari as-Shafii' katika kitabu chake cha Dhakhair al-Uqba fii Manaqib Dhawi al-Qurba Kwamba Mtume Mtukufu (saw) alisema: "Hakika Mwenyezi Mungu amejaalia malipo yangu katika nyinyi kuwapenda Ahlu Bait wangu na bila shaka nitakuulizeni kesho (Siku ya Kiama) kuhusiana na hilo."

Jadithi nyingine ni ile iliyonukuliwa na Sheikh Kuleini katika kitabu chake mashuhuri cha al-Kafi ambapo ananukuu Hadithi kutoka kwa Imam Ja'ffar as-Swadiq akifafanua maana ya wanaokusudiwa katika neno 'qur'ba' yaani ndugu katika Aya tunayoihadili kwa kusema: 'Wao ni Maimamu (as).'

Ama njia ya pili ni ya ushahidi ambapo moja ya ushahidi huo ni ule ambao umenukuliwa na al-Hafidh as-Suyuti as-Shafii' katika Tafsiri yake ya ad-Durr al-Manthur katika ufafanuzi wake wa Aya Tukufu ya Qur'ba akitegemea Hadithi ambayo imepokelewa na Abu Dailam ambaye anasema: 'Ali bin al-Hussein (as) alipoletwa mateka katika mji wa Damascus, mmoja wa watu wa Sham alisimama na kusema: Ninamshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amukuueni na kukung'oeni kutoka kwenye nafasi yenu! Ali Bin al-Hussein (as) akamwambia: Je, umeshawahi kusoma Qur'ani? Mtu huyo akasema: Nam. Ali bin Hussein (as) akamuuliza: Je, umesoma Sura ya HaaMeem? Akajibu: Nam. Akamuuliza: Haujawahi kusoma: Sema: Kwa haya sikuombeni malipo yoyote kwenu ila mapenzi katika ndugu? Mtu huyo akawa ameshangaa na kuchanganyikiwa na kuuliza: Je, ni nyinyi ndio watu hao?! Akasema: Nam.' Na ushahidi mwingine ni ule ambao umenukuliwa na al-Hadhrami as-Shafii' kupitia Hadhithi aliyoinukuu katika kitabu chake cha Wasilatul Maal fii Add Manaqibil Aal kutoka kwa Imam Ali (as) ambaye anasema: 'Halindi mapenzi yetu ila kila muumini.' Kisha akanukuu ufafanuzi uliotolewa na Wahidi katika kitabu chake cha As'bab Nuzul akibainisha Hadithi mashuhuri ya Bwana Mtume (saw) inayosema: 'Yule ambaye mini ni Bwana (msimamizi wa mambo) wake basi na Ali ni Bwana wake', na kusema: 'Usimamizi huu wa mambo ambao aliuthibitisha Mtume (saw), kila mtu ataulizwa juu yake, yaani haki ya usimamizi na uongozi wa Imam Ali na Ahlul Bait wa Mtume (saw), Siku ya Kiama kwa sababu Mwenyezi Mungu alimuamuru Mtume wake awajulishe wanadamu kwamba hakuwaomba malipo yoyote kutoka na ujumbe aliowafikishia na ulingajiaji aliowafanyia isipokuwa kuwapenda watu wa karibu yake. Yaani wanadamu wataulizwa, iwapo waliwapa Ahlu Bait hao wa Mtume haki yao ya kuwaongoza na kusimamia mambo yao kama walivyotakiwa kufanya na Mtume Mtukufu (saw), au walipuuza na kukanyaga haki hiyo, na hivyo kustahiki kuwajibishwa na kuadhibiwa?!

Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi ambacho tunataraji kimekunufaisheni vya kutosha. Basi hadi tutakapojaaliwa kukutana tena katika kipindi kingine kama hiki wakati na siku kama hii, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.