Qaddoumi: Iran ina haki ya kujibu mashambulizi dhidi yake
-
Khalid Qaddoumi
Mwakilishi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) Tehran amesisitiza kuwa Iran ina haki kamili na ya pande zote ya kukabiliana na mashambulizi ya adui kwa kila njia inayoiona inafaa.
Khalid Qaddoumi amesema katika mahojiano na shirika la habari la Tasnim juu ya msimamo wa karibuni wa Hamas kuhusu mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran kwamba: Msimamo wa harakati ya Hamas uko wazi. “Tumelaani mashambulizi ya kikatili ya utawala wa Kizayuni na Marekani dhidi ya wananchi wa Iran na tunalaani vikali hujuma hiyo,” amesema mwakilishi wa Hamas mjini Tehran.
Ameongeza kuwa: Ukweli wa mambo ni kuwa jibu la Iran kwa uchokozi huo ni kubwa na ni kwa mujibu wa kiwango cha uhalifu na ufidhuli wa adui Mzayuni na Marekani; na kwa msingi huu tunaamini kuwa Iran ina haki kamili na ya pande zote ya kukabiliana na uvamizi wa adui kwa kila njia inayoiona inafaa.
Qaddoumi amesema nchi za Kiislamu zinapasa kuwa na msimamo wa pamoja na kwamba bila shaka kinachohitajika sasa ni msimamo wa pamoja wa Umma wa Kiislamu.