Iran yazitaka nchi jirani kuwafukuza wanajeshi vamizi wa kigeni
-
Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran,
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa Iran inaziomba nchi jirani na za kindugu kuwafukuza wanajeshi wa kigeni wanaovamia kutoka katika ardhi zao.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la IRIB, Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, amendika katika ujumbe wake kwenye mtandao wa X kwamba kile kinachoitwa mwavuli wa usalama ambao Marekani imekuwa ikiutangaza kwa miaka mingi sasa umeonekana wazi kuwa na mianya mingi.
Amebaini kuwa mwavuli huo haukuwa kizuizi cha migogoro, bali kinyume chake umechangia kuibuka kwa mvutano na migogoro mipya katika eneo hilo. Kwa mujibu wa Araghchi, Marekani sasa imejikuta katika hali ya kuomba msaada kutoka kwa mataifa mengine , hata kutoka China , ili kusaidia kulinda usalama wa Mlango wa Hormuz.
Katika ujumbe wake, Araghchi amesisitiza kuwa Iran inazisihi nchi jirani na za kindugu kuchukua hatua ya kuwaondoa wanajeshi wa kigeni wanaofanya vitendo vya uchokozi kutoka katika ardhi zao, akiongeza kuwa kipaumbele kikuu cha majeshi hayo ni kulinda maslahi ya utawala wa Israel pekee.