Jumatano tarehe 29 Juni 2022
Leo ni Jumatano tarehe 29 Dhulqaada 1443 Hijria sawa na Juni 29 mwaka 2022.
Siku kama ya leo miaka 109 iliyopita vilianza Vita vya Pili vya Balkan kati ya Bulgaria na umoja wa nchi za Serbia, Ugiriki, Montenegro, Romania na utawala wa Othmania. Karibu mwaka mmoja kabla ya hapo katika Vita vya Kwanza vya Balkan, Bulgaria, Serbia, Ugiriki na Montenegro zilizokuwa sehemu ya utawala wa Othmania, zilianzisha uasi dhidi ya ufalme huo, na kutokana na kudhoofika utawala huo nchi hizo zilifanikiwa kupata uhuru. Kwa msingi huo karibu asilimia 80 ya nchi zilizokuwa chini ya himaya ya Othmania huko Ulaya zikatoka chini ya udhibiti wa dola hilo. Hata hivyo nchi zilizoshinda katika Vita vya Kwanza vya Balkan hazikuweza kufikia makubaliano ya kugawana ardhi zilizokombolewa sababu iliyopelekea kuanza Vita vya Pili vya Balkan. Vita vya Balkan viliandaa mazingira ya kuanza kwa Vita vya Kwanza vya Dunia.
Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita yaani tarehe 29 Juni mwaka 1976, muungano wa visiwa vya Ushelisheli ulipata uhuru na kila siku kama hii huadhimishwa katika visiwa hivyo kama siku ya taifa. Hadi kufikia katikati ya karne ya 18, wakati ambao Wareno walikuwa wakiikalia kwa mabavu ardhi hiyo, visiwa vya Ushelisheli vilikuwa havijagunduliwa na havikuwa na wakazi. Mwishoni mwa karne ya 18 wakati ulipopamba moto wa mapinduzi ya Ufaransa, wanajeshi wa Uingereza waliokuwa katika eneo la Afrika waliivamia Ushelisheli. Mapambano ya kuikomboa nchi hiyo yalipamba moto mwaka 1960 na kuendelea, na miaka 16 iliyofuata visiwa vya Ushelisheli vikawa huru na kuasisi mfumo wa Jamhuri. Ushelisheli inaundwa na visiwa kadhaa vilivyoko katika bahari ya Hindi ikipakana na Madagascar.
Tarehe 29 Juni miaka 30 iliyopita aliuawa Mohamed Boudiaf aliyekuwa Mkuu wa Baraza la Serikali ya Algeria. Mohamed Boudiaf alikuwa rais wa nne wa Algeria tangu nchi hiyo ilipopata uhuru. Alijiunga na harakati za siri za kupinga ukoloni wa Ufaransa akiwa bado kijana na kupanda ngazi katika harakati ya wananchi wa Algeria iliyokuwa ikiendesha harakati za siri dhidi ya wakoloni wa Kifaransa. Baada ya ushindi wa mapinduzi ya wananchi wa Algeria hapo mwaka 1962 Mohamed Boudiaf aliunda serikali ya kisoshalisti akishirikiana na Ahmed Ben Bella. Alikimbilia nje ya nchi kufuatia mapinduzi ya Houari Boumediene dhidi ya serikali Ben Bella na kurejea Algeria baada ya kujiuzulu Chadli Bendjedid na kuunda baraza la uongozi. Kama walivyokuwa viongozi wengi wa baada ya uhuru wa Algeria, Mohamed Boudiaf alikuwa mpinzani mkubwa wa fikra za Kiislamu na baada ya kushika madaraka alivunja harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo iliyokuwa imeshinda uchaguzi wa Bunge na kubatilisha matokeo ya uchaguzi huo. Hatua hiyo ilisababisha machafuko ya ndani nchini Algeria na tarehe 29 Juni 1992 alipigwa risasi na kuuawa na mmoja wa walinzi wake.
Na tarehe 8 Tir kwa mwaka wa Kiirani imetambuliwa kuwa ni siku ya kitaifa ya kupambana na silaha za kemikali na vikidudu. Siku kama ya leo mji wa Sardasht huko magharibi mwa Iran ulishambuliwa kwa mabomu ya kemikali na ndege za kivita za utawala wa zamani wa Iraq. Wakazi wa mji huo wapatao 110 waliuawa shahidi na wengine 530 kujeruhiwa kwenye mashambulio hayo. Utawala wa zamani wa Iraq ambao ulikuwa umepoteza matumini ya kushinda vita ilivyovianzisha dhidi ya Iran, ulidhani kwamba kwa kuendesha mashambulio ya silaha za kemikali ungeweza kuitwisha Iran matakwa yake kupitia mashambulio hayo ya kinyama, lakini haukufanikiwa kufikia lengo hilo.