Jumamosi, Julai 9, 2022
Leo ni Jumamosi tarehe 9 Dhul-Hijja mwaka 1443 Hijria, inayosadifiana na tarehe 9 Julai mwaka 2022 Miladia.
Leo tarehe 9 Dhul-Hijja katika kalenda ya Hijria Qamaria, inasadifiana na Siku ya Arafa. Arafa ni jina la jangwa kubwa linalopakana na mlima wa Jabalur Rahma ulioko kusini mashariki mwa Makka. Tangu adhuhuri ya siku hii mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu, al Kaaba, husimama katika uwanja wa Arafa na hadithi nyingi za Mtume Muhammad (saw) na Ahlibaiti zake watoharifu zimetaja fadhila na utukufu mkubwa wa kisimamo hicho. Hadithi zinasema kuwa Mwenyezi Mungu SW ameifanya ardhi ya Arafa ambayo ilikuwa medani ya matukio mengi muhimu ya kihistoria, kuwa mahala pa kuwapokea wageni wake wanaokwenda Hija na ameweka meza na karamu yake pembeni ya mlima wa Jabalur Rahma. Ni vyema kukumbusha kuwa magharibi ya siku hii ya leo mahujaji wanaondoka uwanja wa Arafa na kuelekea Mash'arul Haram na kujitayarisha kwa ajili na amali nyingine za Hija.

##########
Siku kama ya leo miaka 1383 iliyopita, sawa na tarehe 9 Dhul-Hijja mwaka 60 Hijria, Muslim bin Aqil, binamu wa Imam Hussein bin Ali bin Abi Talib AS aliuawa shahidi mjini Kufa Iraq. Alikuwa mmoja wa shakhsia wakubwa na wacha Mungu katika zama zake. Alielekea mjini al-Kufa, Iraq akiwa na lengo la kwenda kutathmini ni kwa kiwango gani watu wa mji huo walikuwa wakimtii Imam Hussen, baada ya watu wa mji huo kumwandikia maelfu ya barua Imam huyo wakimtaka aende mjini humo na kwamba wako tayari kumuunga mkono katika harakati yake dhidi utawala dhalimu wa Yazid bin Muawiya. Watu wa Kufa walimsaliti Muslim bin Aqil baada ya kuhadaika kwa hila na uongo wa Ubeidullah bin Ziyad, mtawala wa wakati huo wa Kufa na wakamuacha Muslim bin Aqiil peke yake.

##########
Miaka 895 iliyopita, aliaga dunia Fadhl bin Hassan Tabarsi anayejulikana kwa lakabu la Aminul Islam, alimu, mpokeaji wa hadithi na mfasiri mkubwa wa Qur'ani. Fadhl bin Hassan Tabarsi alikuwa mwanazuoni mkubwa na alikuwa akiheshimiwa na makundi mengi ya Kiislamu. Sheikh Tabarsi pia alikuwa miongoni mwa makadhi waadilifu katika zama zake. Kitabu muhimu zaidi cha msomi huyo wa Kiislamu ni tafsiri ya Qur'ani ya Majmaul Bayan yenye juzuu kumi. Vilevile ameandika tafsiri nyingine ya Qur'ani aliyoipa jina la Jawamiul Jamii.

##########
Miaka 20 iliyopita mwafaka na tarehe 9 Julai mwaka 2002 Umoja wa Afrika (AU) ulichukua nafasi ya Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) baada ya kuidhinishwa na wakuu wa nchi za Kiafrika. OAU iliundwa mwaka 1963 ili kusaidia juhudi za kupigania uhuru wa nchi za Kiafrika na kutatua hitilafu miongoni mwa nchi hizo. Hata hivyo siku baada ya siku kulijitokeza hisia kwamba katika mazingira ya ulimwengu wa leo kuna udharura wa kuundwa taasisi yenye nguvu za utendaji na yenye malengo mapya zaidi. Kwa msingi huo katika siku kama ya leo mwaka 2002 wakuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) waliunda Umoja wa Afrika (AU) katika mji wa Durban, Afrika Kusini. Taasisi kama vile bunge, kamisheni ya utendaji, benki kuu, mfuko wa fedha na mahakama zimezingatiwa katika umoja huo kwa ajili ya kuratibu mawasiliano na kusaidia ustawi wa kiuchumi wa nchi za Kiafrika.

##########
Na siku kama ya leo miaka 11 iliyopita Sudan Kusini ilitangazwa rasmi kuwa nchi huru inayojitawala. Nchi mpya ya Sudan Kusini iliundwa baada ya kujitenga na Sudan. Raia wa Sudan Kusini tarehe Tisa mwezi Julai mwaka 2011 walishiriki kwenye kura ya maoni kwa ajili ya kuainisha mustakbali wa eneo la kusini mwa Sudan na lile la kaskazini, kura ambayo hatimaye ilipelekea eneo la kusini mwa Sudan kujitenga na lile la kaskazini na kuundwa nchi inayojitawala ya Sudan Kusini.
