Jul 14, 2022 03:19 UTC
  • Alkhamisi tarehe 14 Julai 2022

Leo ni Alkhamisi tarehe 14 Dhulhaji 1443 Hijria inayosadifiana na tarehe 14 Julai 2022.

Siku kama ya leo miaka 233 iliyopita, gereza la kihistoria la Bastille lilitekwa na wakazi wa Paris katika kipindi cha mapinduzi ya Ufaransa na sehemu kubwa ya gereza hilo ikaharibiwa. Jela hiyo ilijengwa mwaka 1369 kwa lengo la matumizi ya kijeshi. Hata hivyo baada ya kupita miaka kadhaa iligeuka na kuwa gereza la kutisha ambapo ndani yake walizuiliwa wafungwa wengi wa kisiasa hususan watu waliokuwa wakiendesha harakati za kudai jamhuri nchini humo. Gereza la Bastille lilidhihirisha udikteta wa wafalme wa Ufaransa. 

gereza la kihistoria la Bastille

Katika siku kama ya leo miaka 161 iliyopita ilitengenezwa bunduki ya kwanza ya rashasha. Bunduki hiyo ilitengenezwa na msomi wa Kimarekani Dr. Richard J. Gatling kwa kutumia uzoefu wa wavumbuzi wa kabla yake wa silaha. Bunduki iliyotengezwa na Gatling haikuwa ya utomatiki lakini baadaye teknolojia ya kutengeneza silaha hiyo ilikamilishwa zaidi na hii leo bunduki ya rashasha inatambuliwa kuwa silaha muhimu sana katika medani za vita.  

Katika siku kama ya leo miaka 83 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sheikh Fayyadh Zanjani, alimu mkubwa wa Waislamu. Ayatullah Sheikh Fayyadh Zanjani alizaliwa mwaka 1285 Hijiria katika moja ya vijiji vya mji wa Zanjan nchini Iran. Awali alisoma kwa baba yake elimu ya dini na kidha akaelekea mjini Tehran kwa wasomi wakubwa wa zama hizo ambapo alifanikiwa kufikia daraja ya Ijtihad. Baada ya kufikia elimu ya juu katika dini alianza kazi ya kufundisha. Aliandika vitabu kadhaa juu ya sheria za Kiislamu ambavyo ni 'Kitaabul-Ijaarah' na 'Dhakhaairul-Ummah.' Ayatullah Sheikh Fayyadh Zanjani alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 75 huku akiwa ni marjaa wa Waislamu wa mji wa Zanjan.

Ayatullah Sheikh Fayyadh Zanjani

Miaka 64 iliyopita katika siku kama ya leo, Jenerali Abdul Karim Qassim alifanya mapinduzi nchini Iraq na kuuondoa madarakani utawala wa Kifalme na kisha kuanzisha mfumo wa utawala wa serikali ya jamhuri. Faisal II mwana wa mfalme na Waziri Mkuu wa Iraq waliuawa katika tukio hilo la mapinduzi. Aidha wafuasi wa utawala wa Kifalme walikandamizwa na kusambaratishwa kabisa. Baada ya mapinduzi hayo, Abdul Karim Qassim aliyekuwa na mirengo ya utaifa alishika hatamu za uongozi nchini Iraq hadi mwaka 1963, wakati alipokuja kuondolewa madarakani kwa njia ya mapinduzi pia na Abdul Salam Arif aliyekuwa muitifaki wake mkubwa na wa karibu. 

Jenerali Abdul Karim Qassim

Miaka 39 iliyopita na katika siku kama ya leo yaani tarehe 23 Tir mwaka 1362 Hijria Shamsia, duru ya kwanza ya Baraza la Wanazuoni Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu na Kusimamia Kazi Zake ilianza shughulki zake. Kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Baraza la Wanazuoni ni moja ya nguzo na asasi muhimu katika mfumo wa Kiislamu unaotawala hapa nchini. Wawakilishi wa baraza hilo ni lazima wawe mafakihi waliotimiza masharti na huchaguliwa moja kwa moja kwa kura za wananchi. Jukumu muhimu la Baraza la Wataalamu ni kumchagua Kiongozi Maudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kusimamia shughuli za utendaji wake. Uchaguzi wa baraza hilo la Iran hufanyika mara moja kila baada ya miaka minane. 

Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, alifariki dunia Mahdi Hamidi Shirazi, malenga, mtafiti na mwandishi mkubwa wa zama hizo. Mahdi Shirazi alizaliwa mwaka 1293 Hijria katika mji wa Shiraz wa kusini mwa Iran na kutunukiwa shahada ya udaktari katika taaluma ya lugha na fasihi ya Kifarsi. Dakta Hamidi ameandika vitabu vingi vya mashairi ya Kifarsi, ambapo vingi vinahusiana na elimu ya mitindo, fasihi, historia na fani mbalimbali za mashairi. 

Mahdi Hamidi Shirazi

Na katika siku kama ya leo miaka 29 iliyopita, alifariki dunia Dakta Abdul-Hadi Hairi, mmoja wa walimu wakubwa wa historia nchini Iran. Dakta Hairi, alizaliwa mjini Qum katika familia ya kidini. Aidha msomi huyo alikuwa mjukuu wa marjaa mkubwa na mwasisi wa hauza ya masomo ya kidini ya mjini hapo, Ayatullah Haj Sheikh Abdul-Karim Hairi.  Baada ya kusoma masomo ya awali ya theolojia, aliendelea na masomo yake huko nchini Canada. 

Dakta Abdul-Hadi Hairi