Jumapili 17 Julai 2022
Leo ni Jumapili 17 Dhulhija 1443 Hijria inayosadifiana na Julai 17 mwaka 2022.
Siku kama ya leo miaka 109 iliyopita Profesa Roger Garaudy, mwanafalsafa na mwanafikra wa Ufaransa alizaliwa huko katika mji wa Marseille. Garaudy alipata shahada ya udaktari katika taaluma tatu za masomo ya falsafa, fasihi na utamaduni. Roger Garaudy alifungwa jela katika kambi ya mateka wa kivita wa Ujerumani tangu mwaka 1940 hadi 1943 kutokana na mapambano yake dhidi ya ufashisti wa Adolph Hitler wakati Ufaransa ilipokaliwa kwa mabavu na Ujerumani. Profesa Garaudy alikuwa mwanachama wa chama cha Kikomonisti cha Ufaransa kwa miaka 36 na pia mwanachama wa kamati kuu ya chama hicho kwa miaka 25. Hata hivyo mitazamo ya kikomunisti na kiliberali haikuweza kukata kiu ya kutafuta ukweli ya msomi huyo wa Ufaransa na hatimaye alikubali dini ya tukufu ya Uislamu baada ya kufanya utafiti mkubwa. Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran mwaka 1979 ulikuwa na taathira kubwa katika mitazamo ya Profesa Roger Garaudy.
Katika siku kama ya leo miaka 54 iliyopita, chama cha Baath cha Iraq kilichukua hatamu za uongozi kupitia mapinduzi yaliyoongozwa na Ahmad Hassan al-Bakr na kumpindua Rais Abdulrahman Aarif. Baada ya kuchukua madaraka chama cha Baath, Saddam Hussein ambaye alikuwa kiongozi nambari mbili wa chama hicho alianza kuwauwa wapinzani wake nchini Iraq na vikosi vya usalama na vya jeshi la nchi hiyo pia vikaanzisha hujuma kali dhidi ya wapinzani wa Kikurdi, wazalendo, wanaharakati wa Kiislamu na hata Wakomonisti.
Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita Baraza la Kulinda Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lilianza rasmi kazi zake. Baraza hilo liliundwa kwa mujibu wa kipengee namba moja cha Katiba ya Iran kwa shabaha ya kukinda sharia za Kiislamu na Katiba na kuhakikisha kwamba sheria zote zinazopasishwa hapa nchini hazipingani na viwili hivyo. Baraza hilo linaundwa na wataalamu 6 wa elimu ya fiqhi wanaoteuliwa na Kiongozi Mkuu wa Iran na wataalamu 6 wa sheria wanaoteuliwa na Idara ya Mahakama na kupasishwa na Bunge. Kazi kuu ya baraza hilo ni kuhakikisha kwamba, sheria zote zinazopasishwa na Bunge haziendi kinyume na Sheria za Uislamu.

Na miaka 35 iliyopita katika siku kama ya leo kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia uhusiano wa kisiasa wa Iran na Ufaransa ulivunjika wakati wa kujiri vita vya kichokozi vya dikteta Saddam dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Serikali ya wakati huo ya Ufaransa ilitoa himaya na uungaji mkono wa pande zote kwa Iraq wakati wa kuanza hujuma na mashambulio ya jeshi la dikteta Saddam dhidi ya Iran. Aidha wakati wote wa vita hivyo, himaya ya Ufaransa ilichukua wigo mpana zaidi. Hatimaye katika siku kama ya leo Ufaransa ilichukua hatua ya upande mmoja ya kukata uhusiano wake wa kisiasa na Tehran.
