Jumatatu, Agosti 15, 2022
Leo ni Jumatatu mwezi 17 Muharram 1444 Hijria sawa na Agosti 15 mwaka 2022 Milaadia.
Siku kama hii ya leo miaka 546 iliyopita Nuruddin Abdulrahman Jami, malenga na mwanafasihi mkubwa zaidi wa Kiirani wa karne ya Tisa Hijria alifariki dunia katika mji wa Harat katika Afghanistan ya leo ambao wakati huo ulikuwa sehemu ya ardhi ya Iran. Alielekea huko Samarqand wakati wa ujana wake na akiwa huko alijifunza masomo ya dini, fasihi na historia. Vitabu muhimu vya malenga huyo ni pamoja na "Silsilatu al Dhahab", Nafahatul Uns, Shawahidu Nubuwah na "Baharestan."

Siku kama ya leo miaka 491 iliyopita alizaliwa Bahauddin al Amili maarufu kwa jina la Sheikh Bahai, faqihi na aalim mkubwa wa Kiislamu huko katika mji wa Baalbek nchini Lebaon. Baba yake Sheikh Bahai alikuwa mmoja wa maulamaa wakubwa wa Lebanon ambaye alisafiri naye nchini Iran akiwa mtoto. Sheikh Bahai alitumia kipaji chake kikubwa na kuweza kufikia daraja ya uanazuoni katika kipindi kifupi. Aalim huyo alipewa jina la Sheikhul-Islam kutokana na kipawa cha kielimu cha hali ya juu alichokuwa nacho. Sheikh Bahai ameacha zaidi ya vitabu 88 alivyoviandika kwa lugha za Kifarsi na Kiarabu. Baadhi ya vitabu vyenye thamani vya msomi huyo wa Kiislamu ni Jame Abbasi na Kashkool kilichojumuisha riwaya na hadithi, Tashrihul Aflak na vingine vingi alivyoviandika kuhusu masuala ya hisabati na kemia. Sheikh Bahai alifariki dunia mwaka 1030 Hijria huko Isfahan, Iran.

Siku kama ya leo miaka 108 iliyopita, mfereji wa Panama ulifunguliwa rasmi kufuatia kupita meli ya kwanza katika kanali hiyo. Ujenzi wa kanali hiyo ulianzishwa na wahandisi wa Kifaransa na baadaye serikali ya Marekani ilinunua kampuni ya Ufaransa iliyokuwa ikijenga mfereji huo na kukamilisha ujenzi wake. Kujengwa mfereji huo wenye urefu wa zaidi ya kilomita 60 kuliunganisha bahari mbili za Pacifi na Atlantic.

Siku kama ya leo miaka 86 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Allamah Mirza Muhammad Hussein Naini, marjaa na faqihi mkubwa na mmoja kati ya wahakiki wa elimu ya usulu fiq’h. Allamah Naini alizaliwa mwaka 1276 Hijiria Qamaria mkoani Nain, huko katikati mwa Iran, katika familia ya kidini. Allamah Naini alisoma na kuhitimu masomo yake ya awali nyumbani kwao na kuendelea na masomo ya juu huko Najaf, Iraq. Akiwa huko, alipata elimu kwa wasomi wakubwa wa zama hizo kama Allamah Mirza Shirazi na kupata daraja ya juu ya elimu za hesabu, falsafa, irfan na fiq’hi. Miongoni mwa athari za Allamah Naini ni pamoja na vitabu vya “Wasiilatun-Najjat” na “Tanbiihul-Ummah wa Tanziihul-Millah” kitabu ambacho kilitoa mchango mkubwa katika mapambano dhidi ya viongozi dhalimu wa zama hizo.

Miaka 62 iliyopita katika siku kama hii ya leo nchi ya Jamhuri ya Congo Brazzaville ilipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Mfaransa. Huko nyuma Congo Brazzaville ilikuwa sehemu ya ardhi ya Congo katika Afrika Magharibi iliyojumuisha Zaire ya zamani na Angola. Kongo Brazzaville iligunduliwa na Wareno katika karne ya 15 na baadaye ilikaliwa kwa mabavu na wakoloni wa Kifaransa kwa miaka kadhaa mfululizo. Kongo Brazaville iko magharibi mwa Afrika ikipakana na Jamhuri ya Afrika ya Kati, Cameroon, Gabon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Angola. Miaka 74 iliyopita, sawa na tarehe 15 Agosti 1948 nchi ya Korea ya Kusini iliundwa baada ya kujitokeza mgawanyiko wa visiwa vya Korea. Visiwa vya Korea vilikabiliwa na uvamizi na kukaliwa kwa mabavu wa madola yenye nguvu katika eneo hilo kama vile China na Japan tokea nusu ya kwanza ya karne ya ishirini.

Miaka 33 iliyopita katika siku kama ya leo, inayosadifiana na tarehe 24 Mordad 1369 Hijria Shamsia, Saddam Hussein Rais wa zamani wa Iraq alimtumia barua Hujjatul Islam Walmuslimin Hashemi Rafsanjani aliyekuwa Rais wa Iran wakati huo, akimjulisha kwamba amekubali kikamilifu vipengee vya makubaliano ya mpaka yaliyotiwa saini 1975 nchini Algeria. Hata hivyo, tarehe 27 Shahrivar 1359 Hijria Shamsia, Saddam Hussein baada ya kushawishiwa na madola ya kibeberu ya Magharibi, alijitokeza kwenye televisheni ya Iraq na kuuchanachana mkataba huo, na baada ya siku chache, alianza kuivamia ardhi ya Iran. Saddam Hussein na waitifaki wake walidhani kwamba, muda mfupi tu baada ya kuivamia ardhi ya Iran wangeliweza kuuangusha mfumo mchanga wa Kiislamu hapa nchini. Hata hivyo kusimama kidete wananchi na mapambano ya wapiganaji shupavu wa Kiislamu wa Iran yalibatilisha njama zao na jeshi vamizi la Iraq likalazimika kurejea nje ya mipaka ya Iran baada ya kushindwa mtawalia.

Miaka 17 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 15 Agosti 2005 Miladia, utawala wa Kizayuni wa Israel ulilazimika kuondoka katika maeneo ya Ukanda wa Gaza, magharibi mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Eneo hilo lilikaliwa kwa mabavu na Wazayuni mwaka 1967, baada ya kutokea vita vya Waarabu na utawala wa Kizayuni wa Israel. Lakini pamoja na hayo utawala huo katili hutekeleza mashambulio ya mara kwa mara dhidi ya Gaza na kuwaua Wapalestina wengi hasa wanawake na watoto.
