Sep 22, 2022 02:15 UTC
  • Jumatano tarehe 21 Septemba 2022

Leo ni Jumatano tarehe 24 Safar 1444 Hijria inayosadifiana na tarehe 21 Septemba 2022.

Katika siku kama ya leo miaka 1059 iliyopita Sahib bin Abbad, mwanafasihi maarufu na msomi wa Kiislamu wa kizazi cha Dailami alifariki dunia. Sahib alikuwa mwandishi hodari na mtu mwenye hadhi na mashuhuri sana katika zama zake. Licha ya kwamba alikuwa waziri katika serikali ya kizazi cha Dailami, lakini alikuwa mtu mnyenyekevu na mwema kwa watu wa chini yake. Sahib bin Abbad ameandika vitabu vingi, na maarufu zaidi ni kile cha "al Muhiit" chenye juzuu saba.

Mahali lilipo kaburi la Sahib bin Abbad

Siku kama ya leo miaka 190 iliyopita, inayosadifiana na 21 Septemba 1832, aliaga dunia Sir Walter Scott, mwandishi wa riwaya, mshairi na mwanahistoria mahiri wa Uskochi. Alizaliwa 15 Agosti mwaka 1771 na baada ya kuhitimu masomo yake katika taaluma ya sheria, alifanya kazi ya uwakili kwa muda wa miaka 14. Hata hivyo, Sir Scott alikuwa na shauku na mapenzi makubwa na taaluma ya fasihi ya lugha.

Sir Walter Scott

Siku kama ya leo miaka 113 iliyopita, yaani 21 Septemba 1909, alizaliwa Dakta Osagyefo Kwame Nkrumah mwanasiasa na shujaa wa uhuru wa Ghana. Nkrumah alishiriki kikamilifu katika harakati za kupigania uhuru za wananchi wa Ghana dhidi ya mkoloni Muingereza. Baada ya kujipatia uhuru, kulijitokeza na kushuhudiwa njama kadhaa za kutaka kumuondoa madarakani na hata kumuua Nkrumah. Mwaka 1966 wakati Dakta Nkrumah akiwa safarini nchini China, Jenerali Joseph Ankrah alifanya mapinduzi na kuiondoa madarakani serikali Nkrumah. Mwanamapinduzi huyo aliaga dunia mwaka 1972 akiwa uhamishoni nchini Romania. Kwame Nkrumah alikuwa na nafasi muhimu katika kuasisiwa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM pamoja Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika OAU.

Kwame Nkrumah

Na siku kama ya leo miaka 28 iliyopita Bunge la Taifa la Ufaransa lilipasisha sheria iliyopiga marufuku vazi la staha la mwanamke wa Kiislamu, hijabu katika shule za nchi hiyo. Ufaransa ilipasisha sheria hiyo inayowazuia wanafunzi wa kike Waislamu kwenda mashuleni wakiwa na vazi la hijabu licha ya kudai kuwa ni kitovu cha demokrasia na uhuru. Baadaye sheria hiyo ilipanuliwa zaidi na kupiga marufuku vazi la hijabu katika vyuo vikuu na idara za umma. Wachambuzi wengi walikosoa vikali sheria hiyo wakisema inapingana na Katiba ya Ufaransa na Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu zinazosisitiza kuwa kila mtu ana uhuru wa kukubali na kutekeleza itikadi zake za kidini maadamu hazina madhara kwa watu wengine.