Sep 26, 2022 06:16 UTC
  • Jumatatu tarehe 26 Septemba 2022

Leo ni Jumatatu tarehe 29 Safar 1444 Hijria inayosadifiana na tarehe 26 Septemba 2022.

Katika siku kama ya leo tarehe 29 Safar miaka 158 iliyopita, alifariki dunia Mulla Hussein-Ali Tuysirkani, msomi na alimu mkubwa wa Kiislamu katika mkoa wa Isfahani huko katikati mwa Iran. Alikuwa msomi mwenye maoni na mhakiki na alibobea sana katika elimu na taaluma kama fiqhi, na usulul fiqhi. Tuysirkani alijishughulisha na kufundisha na kuelea wanafunzi wengi kwa miaka mingi. Kitabu muhimu zaidi cha msomi huyo wa Kiislamu ni Kashful Asrar chenye juzuu 11. Vitabu vingine vya mwanazuoni huyo ni Asul Aqaaid na Makarimul Akhaq.

Katika siku kama ya leo miaka 134 iliyopita alizaliwa Thomas Stearns Eliot mshairi na mwanafasihi mashuhuri wa Uingereza. Malenga huyo ambaye ni mashuhuri kwa jina la S. T. Eliot alitoa nudhumu yake ya kwanza ya mashairi mwaka 1922 iliyokuwa na jina la "The Waste Land" na kupata umashuhuri mkubwa. Mwanafasihi huyo wa Kiingereza aliaga dunia mwaka 1965.

Thomas Stearns Eliot

Siku kama ya leo miaka 112 iliyopita, inayosadifiana na 26 Septemba 1907, nchi ya New Zealand iliyoko mashariki mwa Australia ilipata uhuru. Visiwa vya New Zealand vilikoloniwa na Uingereza mwaka 1769 na karne ya 19 Miladia, ilishuhudia ukoloni dhidi ya nchi hiyo ukishadidi sambamba na wimbi kubwa la wahajiri wa Kiingereza waliokuwa wakielekea katika nchi hiyo.

Bendera ya New Zealand

Siku kama ya leo miaka 62 iliyopita, inayosadifiana na 26 Septemba 1960, Makamu wa Rais wa Marekani Richard Nixon na Seneta John F. Kennedy wa Massachusetts walikabiliana katika mdahalo wa kwanza wa televisheni wakati wakiwania tiketi ya kuingia ikulu ya White House. John Kennedy aliibuka na ushindi katika uchaguzi wa rais uliofanyika mwaka huo.

Na siku kama hii ya leo miaka 10 iliyopita Maya Nasri mwandishi habari wa Kikristo wa kanali ya televisheni ya Press ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliuawa mjini Damascus nchini Syria wakati alipokuwa akitayarisha ripoti kwa ajili ya kanali hiyo. Maya Nasr alizaliwa tarehe 30 Julai mwaka 1979 nchini Syria na kuhitimu masomo katika Chuo Kikuu cha Kaplan kilichoko New York huko Marekani. Nasr akiwa pamoja na Mkurugenzi wa kanali ya televisheni ya Press nchini Syria, Hussein Murtadha, alishambuliwa kwa kupigwa risasi mbili kichwani na mlenga shabaha wa wapinzani wa serikali ya Damascus wakitayarisha ripoti ya matukio ya Syria. Mwenzake Maya, Hussein Murtadhaa alijeruhiwa katika shambulizi hilo.

Maya Nasri