Sep 29, 2022 02:29 UTC
  • Alkhamisi tarehe 29 Septemba 2022

Leo ni Alkhamisi tarehe Pili Rabiul Awwal 1444 Hijria sawa na tarehe 29 Septemba 2022.

Siku kama ya leo miaka 814 iliyopita, aliaga dunia Ibn Athir Jazari, mwanahistoria, mtaalamu wa fasihi na mpokezi mkubwa wa hadithi. Ibn Athir alizaliwa mwaka 555 Hijria huko Iraq na kujifunza taaluma mbalimbali. Alipata umashuhuri katika masuala ya lugha na fasihi ya Kiarabu. Kitabu maarufu zaidi cha Ibn Athir ni al Kamil fi Tarikh. Kitabu kingine cha mwanazuoni huyo mkubwa wa Kiislamu ni Usdul Ghabah Fi Ma'rifatis Sahabah ambacho kinaeleza wasifu wa masahaba 7500 wa Mtume Muhammad (saw).

Miaka 121 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa mwanafizikia mashuhuri wa Italia, Enrico Fermi katika mji wa Roma. Baada ya kukamilisha masomo ya chuo kikuu alivumbua Kanuni ya Mwendo wa Molekuli ya Gesi. Fermi alifanya uchunguzi kuhusu mabadiliko ya atomu na akafanikiwa kutengeneza betri ya atomu kwa kuipasua na kutoa nje nishati yake. Mwanafizikia huyo wa Italia alifariki dunia mwaka 1954.

Enrico Fermi

Siku kama ya leo miaka 120 iliyopita, alifariki dunia mwandishi wa Kifaransa, Emile Zola. Zola alizaliwa mjini Paris mwaka 1840. Zola alindika vitabu vingi katika elimu tofauti. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya mwandishi huyo wa Ufaransa ni "Therese Raquin” "Nana", "The Belly of Paris na "Germinal."

Emile Zola

Katika siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, mwafaka na tarehe 7 Mehr 1360 Hijria Shamsia, aliuawa shahidi Hujjatul Islam Sayyid Abdul Karim Hasheminejad mwanachuoni na mwanamapambano shupavu wa Iran katika mji wa Mashhad. Sayyid Hasheminejad aliuawa shahidi baada ya kupigwa risasi na mmoja wa wanachama wa kundi la Munafikiin (MKO). Mwanachuoni huyo alikuwa mstari wa mbele katika harakati za mapinduzi nchini Iran dhidi ya utawala wa Shah, na aliwahi kuteswa na kuwekwa gerezani mara kadhaa.

Sayyid Abdul Karim Hasheminejad

Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, makamanda 5 wa ngazi za juu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran waliaga dunia katika ajali ya ndege. Viongozi hao walikuwa wakirejea kutoka katika oparesheni za kuukomboa mji wa Abadan ulioko kusini magharibi mwa Iran. Mji huo wa Abadan ulikuwa umezingirwa na jeshi vamizi la dikteta wa zamani wa Iraq Saddam Hussein. Makanda hao ni Shahidi Fallahi, Shahidi Fakuri, Shahidi Namjuu, Shahidi Kolahduz na Shahidi Jahan Ara aliyekuwa kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu mjini Khoram Shahr. Katika ujumbe wa kusifu na kushukuru mchango wa mashahidi hao baada ya tukio hilo Imam Khomein MA aliwataja kuwa mashahidi wa Uislamu.

Na siku kama ya leo miaka 30 iliyopita, ulifanyika uchaguzi huru wa kwanza nchini Angola. Katika uchaguzi huo chama cha MPLA kilichokuwa kikiongoza nchi hiyo tangu mwaka 1976 kilipata ushindi na kiongozi wake José Eduardo dos Santos akachaguliwa tena kuingoza nchi hiyo. Ni vyema kuashiria hapa kwamba, Angola ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe baada ya kupata uhuru kutoka kwa mkoloni Mreno hapo mwaka 1975. Vita vya ndani nchini humo vilihitimishwa rasmi mwaka 2002 baada ya kuuawa kiongozi wa chama cha upinzani cha UNITA Jonas Savimbi aliyekuwa akiungwa mkono na Marekani.